VIDEO: Askofu Shoo akemea kiburi, binadamu kutesa wenzao

Muktasari:

Mkuu wa kanisa la kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Fredrick Shoo amewaasa Watanzania kuacha kiburi na mateso dhidi ya binadamu wenzao, kwa kuwa kufanya hivyo ni kumtesa Mungu.


Moshi. Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Fredrick Shoo amewataka Watanzania bila kujali nafasi, vyeo na mali walizonazo, kubadilika na kuacha kiburi na mateso dhidi ya binadamu wenzao.

Askofu Shoo ameyasema hayo leo Jumatano Desemba 25, 2019, katika kanisa la KKKT usharika wa Moshi Mjini mkoani Kilimanjaro wakati akihubiri kwenye ibada ya Krismasi.

Amesema Yesu aliyefanyika mwili anatambua maana ya mateso na inapotokea binadamu anawatesa binadamu wenzake, anamtesa Mungu.

Amesema cheo kinaweza kumfanya mtu kujisifu na kuwa na kiburi, lakini kwa wale ambao wamempokea Yesu moyoni, kiburi hakipo na hakuna sababu ya kuwa na kiburi wala kujivuna.

"Yesu Kristo akatuguse dhamiri na mioyo yetu, tubadilike, tuache kiburi, tuache kuwatesa binadamu wenzetu na tuache kufurahia kuwatesa wenzetu wasio na hatia, kwani kuna watu wanateseka hata kwenye nyumba zetu na kuna watu wanateswa, sasa baraka ya kuzaliwa Yesu, ikatuletee amani," amesema Askofu Shoo

"Amani ya Kristo, ituongoze, tusiwatese binadamu wenzetu, kwani tunapomtesa mwingine, tujue kwamba Yesu anapata uchungu kwa maana  tukimtesa mwanadamu mwenzetu kwa namna yoyote ile, tunamtesa Mungu, sasa tukawe wajumbe wa amani ya Mungu, ikaingie katika nyumba zetu, jamii na mahali popote."

Aidha amewatia moyo wale wote ambao wanapitia na wako kwenye mateso mbalimbali, kutoogopa wala kukata tamaa kwa kuwa mateso wanayopitia leo, yana mwisho wake.

"Katika kuteseka kwenu, kwa namna yoyote ile, hata tunapoteswa bila hatia, tujue kwamba Mungu yupo pamoja nasi, hivyo usiogope na usikate tamaa wala kuondoa tumaini lako kwa Mungu,  kwani mateso unayokutana nayo kwenye maisha, jua hakika yana mwisho wake"