VIDEO: CCM yatia neno tuhuma dhidi ya Gekul
Dar es Salaam. Kufuatia tuhuma za udhalilishaji dhidi ya Mbunge wa Babati mjini, Pauline Gekul, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kitakachobainika chama kitachukua mkondo wake kwa kuwa kanuni na taratibu.
CCM imetoa kauli hiyo, wakati mbunge huyo akidaiwa kutoa maelekezo kwa kundi la vijana kumdhalilisha kwa kumpiga na kumwingiza chupa sehemu ya haja kubwa na kumtishia kumpiga mfanyakazi wake risasi, Hashim Ally.
Tuhuduma dhidi ya Gekul zilisambaa mitandaoni hivi karibuni na video yenye urefu wa takribani dakika 4: 03 zilimuonyesha kijana Ally akielezea unyama aliofanyiwa huku akiomba msaada.
Hata hivyo, Gekul aliyekuwa Naibu Waziri wa Katiba na Sheria uteuzi wake ulitenguliwa kupitia taarifa iliyotolewa kwa umma na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu Zuhura Yunus, ingawa sababu za utenguzi huo hazijawekwa wazi.
Leo, Novemba 27,2023 jijini Dar es Salaam, Katibu wa NEC itikadi na Uenezi CCM, Paul Makonda akizungumza na waandishi wa habari kuhusu sakata hilo amesema chama hicho kina kanuni na taratibu.
“Kuanzia ngazi ya tawi kwenda wilaya mpaka mkoa hadi kufikia ngazi ya Taifa, tunaweza kutoa taarifa nini kilitokea kikubwa kanuni zipo na mamlaka za nidhamu zipo lakini pia wapo watu wanaohusika na maadili na kama kutakuwa na jambo litakalobainika taratibu zitafuata mkondo wake,” amesema.
Kwa upande wa Polisi, Kamanda wa polisi wa mkoa wa Manyara, kamishna msaidizi George Katabazi, amewataka wakazi wa mjini Babati kuwa watulivu wakati wao wakiendelea na uchunguzi wa tukio la kijana huyo.
"Tunawaomba watu watupe nafasi tufanye kazi yetu, hakuna mtu yetote aliye juu ya sheria hapa nchini, wasijali tunasimamia upatikanaji wa haki kwa mujibu wa sheria zilizopo,"amesema.
Ofisi ya mbunge ilisemaje?
Juzi kupitia taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Katibu Ofisi wa Mbunge Hussein Abrima na baadae kufutwa, ilieleza kuwa, ofisi hiyo imeona video hiyo kwenye mitandao ya kijamii ikimtuhumu Pauline kwa matukio mbalimbali ambayo hayana ukweli wowote,
Kupitia taarifa hiyo ilielezwa kinachoendelea ni mbinu za wahutumiwa kutaka kuwatoa watu kwenye agenda ya msingi ya tuhuma zao zinazowakabili na kuhama kwenye agenda isiyokuwa ya msingi.
Taarifa hiyo imefafanua kuwa, Ofisi ya mbunge imefuatilia kwa kina jambo hilo na kubaini Hashimu Ally alikuwa mtumishi wa PALEII LIKE VIEW GARDEN na alikuwa akijitambulisha kwa jina la Jonathan baada ya kuacha kazi Keni park alipokuwa anafanya kazi (Paleii) zote pamoja zilikuwa zinafanya kazi inayofanana (Biashara ya chakula)
“Novemba 11.11.2023 saa nne asubuhi ndugu aliyejitambulisha Maiko alienda PALEII akiomba kazi kwa madai kuwa alipokuwa akifanya kazi awali (kwa mama Keni Park) amefukuzwa,
Kijana huyo aliposikilizwa na uongozi wa Palei, alielezwa hakuna uwezekano wa kupata kazi jambo ambalo hakukubaliana nalo na kutaka kuonana na Pauline mwenyewe ili aweze kumueleza yaliyomsibu,”imeandikwa kwenye taarifa hiyo.
Baada ya kiongozi huyo kurejea akitokea msibani mkoani Arusha, amekutana na taarifa ya kijana huyo kuomba kazi na kuhusika na vitendo vya kishirikina (kuchota mchanga) akitokea kwa Mama Keni park ndipo alipompa nafasi ya kumsikiliza.
Wakati wa maelezo ya kijana huyo, ilibainika alitumwa kimkakati kuchota mchanga yeye na vijana wenzake wawili kwa lengo la kupeleka ikatumike kishirikina.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kijana huyo alikiri kuwepo kwa mganga aliyekuwa akisubiri mchanga huo hotel ya Kenny park akitokea Iringa.