VIDEO-Dk Mpango atoa maagizo matumizi ya Kiswahili

Dk Mpango atoa maagizo matumizi ya Kiswahili

Muktasari:

  • Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango ametoa maagizo kwa Wizara na taasisi za Serikali ya matumizi ya lugha ya Kiswahili nchini.
  • Dk Mpango ametoa maagizo hayo leo Alhamisi Julai 7, 2022 wakati wa maadhimisho ya kwanza ya Siku ya Kiswahili Dunia yaliyofanyika katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.


Dar es Salaam.  Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango ametoa maagizo kwa Wizara na taasisi za Serikali ya matumizi ya lugha ya Kiswahili nchini.

Dk Mpango ametoa maagizo hayo leo Alhamisi Julai 7, 2022 wakati wa maadhimisho ya kwanza ya Siku ya Kiswahili Dunia yaliyofanyika katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.

Akihutubia katika maadhimisho hayo, ameziagiza Wizara na Taasisi za Serikali kutekeleza maagizo yaliyotolewa juu ya matumizi ya Kiswahili.

“Napenda kuelekeza kama ifuatavyo, jambo la kwanza Wizara na taasisi za Serikali ziendelee kutekeleza maagizo yaliyotolewa kwamba nyaraka za mawasiliano za wizara na idara zake ziwe kwa Kiswahili, mikutano, warsha na dhifa ziendeshwe kwa Kiswahili

Lakini pia majina ya barabara, mitaa, mabango, fomu za usaili maelekezo ya matumizi ya dawa zote, bidhaa na huduma pia ziandikwe kwa Kiswahili” Amesema Dk Mpango

Jambo lingi ambalo Dk Mpango ameagiza ni taarifa za miradi na mikataba inayowahusu wananchi ziwe kwa lugha ya Kiswahili ili kuwawezesha wananchi kuelewa.

“Jambo la pili, taarifa za miradi na mikataba inayohusu wananchi ni lazima ziwe kwa lugha ya Kiswahili, zisiwe kwa lugha ya kigeni pekee lengo ni kuwawezesha wananchi kuelewa kila jambo muhimu katika utawi wa maisha yao” amesema Dk Mpango.