VIDEO: Dobi aliyeishika tasnia ya filamu, mastaa Bongo Tamthilia za Kapuni, Juakali zamuweka juu

Dobi aliyeishika tasnia ya filamu, mastaa Bongo Tamthilia za Kapuni, Juakali zamuweka juu

Muktasari:

  • Kati ya tamthilia zinazofanya vizuri kwa sasa nchini huwezi kuacha kuitaja Juakali, na uzuri wake ni mchanganyiko wa waigizaji zaidi ya 46 wakiwemo mastaa waliweka majina yao juu kupitia sekta mbalimbali.


Kati ya tamthilia zinazofanya vizuri kwa sasa nchini huwezi kuacha kuitaja Juakali, na uzuri wake ni mchanganyiko wa waigizaji zaidi ya 46 wakiwemo mastaa waliweka majina yao juu kupitia sekta mbalimbali.

Licha ya kuwa waigizaji wengi wana taaluma mbalimbali, idadi kubwa ni wageni kwenye uigizaji lakini kutokana na uzoefu wao katika shughuli za kijamii sambamba na vipaji, wamezitendea haki nafasi walizopewa kuigiza.

Mwongozaji na mwandishi wa tamthilia hiyo ni Leah Mwendamseke maarufu Lamata, ambaye anasema kati ya waigizaji 46 kati yao 14 ndio maarufu na wengine 22 ni wageni katika uigizaji na baadhi ndio wanaanza uigizaji.

Tamthiliya hiyo ya Juakali ambayo inarushwa kupitia king’amuzi cha Dstv, ni ya pili kwa mwongozaji huyo kuisimamia ikitanguliwa na ile ya Kapuni ambayo nayo ilibamba kinoma.

Lamata ni nani?

“Safari yangu ilianza 2008 katika kikundi ambacho tamthilia yake ilikuwa ikirushwa na luninga ya ITV, nilijiunga nao kama mwandishi wa stori na niliombwa niigize lakini sikuweza sana.”

“Baada ya siku kadhaa nilichukuliwa na Ray Kigosi na Johari, kazi yangu ilikuwa kuwapigia pasi nguo wasanii, kufanya usafi na mambo mengi huku nikipambana. Kuna mtu alikuwa anaitwa Razaki Fold ni mtu mwingine aliyegundua kipaji changu cha kuwa uongozaji wa filamu,” anasema Lamata.

Huku akitabasamu Lamata anasema, “Huyu bwana alisema ‘huyu dada namuona kama mwongozaji filamu kwa nini usimpe nafasi’. Kwa kauli yake hiyo ndio nikapewa nafasi ya kuwa mwongozaji filamu.”

“Wakati Ray anaigiza mimi ndio nikawa namuongoza, nilifanya hivyo ingawa nilipenda na niliona naweza zaidi kuwa mwandishi wa stori (script).”

Siri ya uigizaji bora

Lamata anasema kati ya vitu alivyokuwa akifuatilia zaidi kwa waigizaji ni kuona wanaigiza kama unavyoeleza mwongozo wa filamu husika. “Nilipenda kuona kama mwandishi na muongozo wa filamu ukimtaka msanii kulia basi alie kweli kweli.”

Anasema jambo hilo ndio lililomfanya aweze kusimamia kwa umakini filamu anayoiongoza. “Kuna vitu vilikuwa vinatokea kipindi cha nyuma yaani baadhi ya watu walikuwa hawapo makini katika kucheza filamu.”

“Baadhi walikuwa wanaigiza ili mradi tu..., ukimwambia alie anasema hajisikii kufanya hivyo. Katika maeneo ya kuonyesha huzuni pia wapo walioshindwa, ukimwambia igiza kama unamkaripia mtu nayo ilikuwa shida kwa baadhi yao.”

Sababu ya kuwatumia hawa

Anatoa siri ya kuwatumia baadhi ya waigizaji katika tamthilia ya Juakali akiwemo Shadee, ambaye ni mtangazaji wa Clouds Media pamoja na mtangazaji mkongwe nchini, Alfred Masako.

“Cha kwanza ni kipaji, na sio kuangalia jina, miaka hiyo tulikuwa tunapenda kuwatumia watu wanaojulikana hasa mitandaoni, lakini nikasema tukija kufanya sanaa ya kweli lazima tuzingatie aina ya watu.”

“Nimemchukua Shadee katika tamthilia ya Juakali na kweli ameweza kucheza vizuri katika nafasi aliyopewa. Mimi hata nikimchukua mwigizaji maarufu sharti awe anajua kuigiza,” amesema Lamata.

Anasema wakati anajitosa katika tasnia hiyo wasanii wa kike na kiume walikuwa hawaamini kama ana kipaji cha kuongoza filamu au tamthilia.

“Moyoni nilijipa nguvu nikasema ipo siku mtanisikiliza nilipambana sana kumbuka wao ni maarufu na sisi ni waongozaji na tupo nyuma yao,” anasema Lamata huku akikaa vyema kwenye kiti.

“Kwa sasa hakuna msanii anayekuja kwenye kampuni yangu ya Lamata akanipangia la kufanya..., hayupo wote wananisikiliza nini ninawaelekeza. Ninawaruhusu washauri na mazuri napokea na ambayo naona yana changamoto basi huwa tunakubaliana kuyaacha.”

“Nazingatia zaidi kipaji huwa sijali sana urembo au utanashati wa mwigizaji. Ukiwa mwongozaji lazima uwe na jicho la tatu, wapo wenye vipaji lakini hawajulikani, sasa hawa kipaji chao ndio huwafanya wanakua katika uigizaji,” anasema.

Kwanini Masako

Anasema katika tamthilia ya Juakali waigizaji ni zaidi ya 46 na kati yao 14 ndio maarufu na wengine 22 ni wageni katika uigizaji na baadhi ndio wanaanza uigizaji.

“Masako yeye anaigiza kama profesa, unajua nilipata shida sana kumpata mtu wa kuigiza nafasi hii na kuweza kuimudu.

“Kimsingi Masako si profesa ameigiza tu nafasi hiyo ila kabla ya kumpata tulichukua maprofesa halisi waliosoma vyuo vikuu mbalimbali, watu wa kawaida na kutaka waigize nafasi hiyo lakini wote walishindwa kwenye usahili.”

“Nakumbuka msanii (wa Bongo fleva) Quick Rocca alikuwa ananitumia picha mbalimbali sasa alivyotuma ya Masako nikasema sahihi kabisa huyu atatufaa. Nikawa najiuliza kama amewahi kuigiza au la, lakini niliamini stori yetu inamfaa na angeweza,” anasema.

Amesema walikwenda nyumbani kwa Masako na mwandishi huyo wa habari mkongwe aliwaeleza kuwa aliwahi kuigiza miaka ya nyuma, “alituambia aliwahi kuigiza yale maigizo ya kanisani, tukamueleza aina ya stori ya tamthilia akafurahi sana.”

“Siku ya kwanza anacheza kwenye kipengele cha kwanza sikutegemea, kipengele hakikutaka azungumze ilikuwa ni vitendo kwa kuweka sura kinamna fulani hivi na alifanikiwa tulifurahi sana.

“Kwa kweli Masako ni wa kimataifa si wa kwetu hapa Tanzania yaani jinsi anavyoigiza, alivyo na uwezo mkubwa, mtanashati..., kuanzia anapokuja siku tunarekodi hadi ukaaji wake kambini ni wa kimataifa kwa kweli. Sijawahi kukutana na msanii wa kiume kama yule ni wa kwanza ni mtu, ambaye amepita katika mistari yake yote anajua anafanya nini,” anasema.

“Muda wote anasoma mwongozo wa tamthilia hadi siku anayokwambia anarudi nyumbani.”

“Ili soko letu la filamu likuwe tunabidi wote tuwe kama Masako kuzingatia nidhamu ya kazi, na siyo lazima uwe umesoma sanaa hapana nidhamu ya kazi kila msanii anatakiwa awe nayo,” anasema Lamata.