VIDEO: Dovutwa aandikiwa barua kuvuliwa uwenyekiti, uanachama UPDP

Muktasari:

Katibu mkuu wa chama cha UPDP, Hamad Ibrahim amesema wamemuandikia barua Fahmi Dovutwa kumvua uwenyekiti na uanachama wa chama hicho.

Dar es Salaam. Katibu mkuu wa chama cha UPDP, Hamad Ibrahim amesema wamemuandikia barua Fahmi Dovutwa kumvua uwenyekiti na uanachama wa chama hicho.

Wakati Ibrahim akilieleza Mwananchi kuhusu suala hilo leo Alhamisi Desemba 5, 2019, Dovutwa amesema hajapata barua hiyo.

Katika barua hiyo iliyoandikwa jana Desemba 4, 2019 yenye kichwa cha habari, ‘kuvuliwa uenyekiti na kufukuzwa uanachama wa  UPDP’ ambayo Mwananchi imeiona, inaeleza yaliyojiri katika kikao cha Halmashauri kuu ya chama hicho kilichofanyika Desemba Mosi, 2019 kisiwani Zanzibar.

Barua hiyo imetaja makosa ya Dovutwa kuwa ni kushindwa kujaza nafasi ya naibu katibu mkuu kwa zaidi ya mwaka mmoja, kushirikiana na vyama vingine vya siasa  kutoa msimamo wa chama hicho kutoshiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa bila idhini ya kamati kuu ya UPDP.

Ibrahim amesema Dovutwa ana haki ya kukata rufaa katika vikao vya chama hicho kuhusu kuvuliwa kwake uanachama lakini amekimbilia kuzungumza katika vyombo vya habari.

"Dovutwa tumeshamvua uenyekiti na uanachama anaitisha uchaguzi kama nani? Hizo tuhuma anazirusha dhidi yetu ni maneno ya mfa maji.”

“Atuachie chama chetu na tayari tumeshawajulisha  wanachama kuwa sio mwanachama wetu tena na taarifa za uchaguzi zitatangazwa mara baada ya kufanyika vikao halali vya chama," amesema katibu huyo.

Akizungumzia kufukuzwa uanachama na uwenyekiti, Dovutwa amesema hajapata barua huku akiwataka wanachama wa UPDP kujiandaa na uchaguzi wa chama hicho mwishoni wa Desemba, 2019.

"Wanachama wote mjiandae na uchaguzi wa chama mwishoni mwa Desemba utakaofanyika mkoani Dar es Salaam. Maandalizi yake yameshakamilika. Msipokee taarifa mtu mwingine isipokuwa ofisi kuu za Dar es Salaam," amesema Dovutwa.