VIDEO: Fredy asimulia alama aliyoacha Lowassa kwa familia


Muktasari:

  • Fred ambaye pia ni Mbunge wa Monduli amesema familia imepokea kifo chake mwanasiasa huyo kwa moyo wa shukrani.

Dar es Salaam. Fredrick Lowassa, mtoto wa Waziri Mkuu mstaafu, hayati Edward Lowassa amesema baba yake aliugua muda mrefu na hadi umauti unamkuta alikuwa amepambana na maradhi kwa muda mrefu.

Akitoa salamu za familia wakati wa shughuli ya kuaga mwili wa Lowassa, Fredrick ambaye pia ni Mbunge wa Monduli amesema familia imekipokea kifo chake kwa moyo wa shukrani.

“Kama ambavyo mmemzungumzia baba alikuwa mpambanaji na alipambana hadi dakika ya mwisho. Baba aliugua kwa muda mrefu na hata mauti yake yalipotokea tulipokea na kusema acha baba akapumzike,” amesema Fredrick.

Fred amemtaja Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mtu aliyekuwa karibu zaidi na familia katika kipindi cha kumuuguza kiongozi huyo anayekumbukwa kwa mchango mkubwa katika uanzishaji wa shule za sekondari za kata nchini.

Alichosema mtoto wa Lowassa kuhusu Rais Samia

“Kama asingekuwa Rais Samia, baba asingefika hata hiyo juzi. Rais Samia alikuwa mama, ndugu na mlezi. Siku anayoondoka kwenda Italia, hali ya baba ilikuwa imeshabadilika, lakini alimuagiza Mkuu wa Majeshi (Jenerali Jacob Mkunda) akawa anampa taarifa ya kila kinachoendelea hadi ule mchana baba anafikwa na umauti,” amesema Fredrick.

Kabla Fredrick hajazungumza, viongozi mbalimbali wa kitaifa walipata nafasi ya kutoa salamu ambapo, Jaji Mkuu wa Tanzania akiwakilishwa na  Jaji Jacob Mwambegele amesema Mahakama inamtambua Lowassa kama mwanasiasa mwenye ngozi ngumu.

Akitoa salamu za mahakama, Jaji Mwambegele amesema uvumilivu aliokuwa nao Lowassa ni funzo kubwa kwa Mahakama na wataendelea kuishi mtazamo huo.

 “Mahakama ya Tanzania inaungana na Watanzania wote kuomboleza msiba huu mzito. Mahakama inamfahamu marehemu Lowassa kama mwanasiasa mwenye moyo wa uvumilivu.

“Ni mwanasiasa ambaye alikuwa na ngozi ngumu ya kisiasa, sisi watu wa mahakama tulimuona Lowassa akiuishi usemi ‘silence is golden’ hili tunalichukua kama funzo,”amesema.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu CCM Bara, Anamringi Macha amesema kila mtu kwa nafasi yake ana la kujifunza kutoka kwa Lowassa, hivyo ni muhimu kuyachukua mazuri yake na kuliendeleza taifa.

“Yote yaliyosemwa ni mengi na tumeyasikia, tunaomba kila mmoja wetu kwa nafasi yake aone ni kipi anaweza kukichukua na kulijenga Taifa.

“Sehemu kubwa ya maisha ya Lowassa yalikuwa CCM, hivyo tuna vingi ambavyo tumejifunza kutoka kwake,” amesema Macha.