Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

VIDEO-Hoja ya Bashe yaibua mjadala mpya

Muktasari:

  • Bashe ambaye katika siku za karibuni amekuwa akiikosoa waziwazi Serikali inayoongozwa na chama chake, juzi alisema vikao vya mikakati vinavyolenga kuweka msimamo wa chama vinaua hoja binafsi zenye masilahi ya wananchi.

Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe alijitwisha ‘gunia la misumari’ alipoeleza bayana kasoro za vikao vya vyama bungeni, lakini kauli yake imeamsha mjadala kwa wabunge, wachambuzi wa siasa na wananchi.

Bashe ambaye katika siku za karibuni amekuwa akiikosoa waziwazi Serikali inayoongozwa na chama chake, juzi alisema vikao vya mikakati vinavyolenga kuweka msimamo wa chama vinaua hoja binafsi zenye masilahi ya wananchi.

Mbunge huyo aliyetaka kuwasilisha hoja binafsi kuhusu kupotea kwa watu na maiti kuokotwa, alishauri Bunge likubali kufanya mabadiliko ya kanuni zake ili mbunge aruhusiwe kuwasilisha hoja binafsi bila ya kulazimishwa kupitia kwenye chama chake.

Alikuwa akishiriki kwenye mjadala wa hotuba ya bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, iliyokosolewa vikali na wabunge wa chama tawala na upinzani, ikiwa ni siku chache baada ya bajeti ya Kilimo kupita kwa masharti baada ya wabunge wa CCM kukutana kimkakati.

Na Bashe, ambaye alishauri bajeti ya Mifugo na Uvuvi irudishwe kwa kuwa haikuwa na majibu ya matatizo ya wananchi, alikuwa akihofu kuwa ingepitishwa kama ilivyokuwa ya Kilimo, licha ya wabunge wengi kuikosoa.

Tukio hilo limepokelewa kwa hisia tofauti na wabunge wenzake, wadau na wananchi.

“Kuendesha siasa kunahitaji mikakati. Si vizuri kuruhusu wabunge wa chama chako kwenda kuyaongelea bungeni mambo ambayo mnaweza kuyamaliza ndani ya chama,” alisema Dk Richard Mbunda, mmoja wa watu waliozungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti jana.

“Ni sawa na kujipiga risasi mwenyewe.”

Lakini aliona kasoro katika kushughulikia hoja za wabunge ndani ya chama.

“Wabunge wako hadi wanakwenda kukusema bungeni si jambo zuri na katika stratergies (mikakati) za siasa, wabunge wanapotoa hoja na kuzileta kwenye chama wanataka kuona zinafanyiwa kazi,” alisema.

“Hata ndani ya chama tu, lakini wanapoona hazifanyiwi kazi ndiyo hayo yanatokea. Yanasemwa bungeni.”

Alisema hadi anaandaa hoja binafsi, mbunge anakuwa ameshaona manufaa na kuamua wabunge wenzake waichambue au kuiboresha ili mwisho wa siku iwe na tija kwa jamii na Taifa, lakini inapokwamishwa inawajengea taswira mbaya.

Hoja za msomi huyo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) zinalingana na za mkazi wa jijini Dodoma, Frank John.

“Ukiona mtu amesema kitu tena kizito, ujue nyuma yake kuna tatizo na anafikisha ujumbe kwa njia nyingine,” alisema John.

“Kwa hiyo viongozi wake wanapaswa kukaa naye na kumuuliza vizuri kulikoni na si kuacha hivihivi.”

Kauli kama hiyo aliitoa mbunge wa zamani wa CCM, Njelu Kasaka ambaye pamoja na wenzake wa Kundi la G55 waliwahi kuwasilisha bungeni hoja ya kutaka kuanzishwa kwa Serikali ya Tanganyika, lakini wakakomea kwenye chama.

“Wakati mwingine mikutano ya vyama inatumika vibaya,” alisema Kasaka. Alisema mikutano hiyo inapaswa kutumika katika mabunge ambayo idadi ya wabunge wa upinzani na chama tawala inakaribiana, hivyo kutishia Serikali iliyopo madarakani.

Kasaka alisema kwa sasa Tanzania haina tishio lolote kwa kuwa wabunge wa chama tawala ni wengi ukilinganisha na wa upinzani na kwamba, kuwa na hoja tofauti ni jambo zuri linaloweza kuisaidia Serikali na chama chao kujitathmini.

Lakini mbunge wa Mchinga (CUF), Hamidu Bobali alisema vikao vya chama chao ni vya kujipanga kimkakati kwenda kujenga hoja kutokana na wizara au jambo lililopo mbele yao. “Sisi tunafanya kama Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi),” alisema.

“Tunapokutana kule, tunatengeneza makundi kazi ya kushambulia wizara kwa wizara na ndio maana hata tunapochangia bungeni, (huwa) tunajipanga kwa uelewa wa eneo fulani.”

Katika hoja ya Bashe, Bobali alisema Spika Job Ndugai anapaswa kuchukua suala hilo kama changamoto kwani anaweza kuandika historia kwa kuwa spika atakayemaliza muda wake wa kuongoza Bunge bila hoja binafsi kuingia bungeni, kitu ambacho alisema si kizuri.

“Si kwamba wabunge hawazipeleki, hapana. Wabunge wanazindaa na hazipati nafasi hivyo aangalie. Wenzake waliomtangulia hoja binafsi zilipata nafasi na tulishuhudia jinsi zilivyoitikisa Serikali kwa mawaziri kung’oka.”

Kitendo cha Bashe kukosoa vikao vya vyama bungeni, kinaweza kumuweka katika hali ngumu.

Lakini Bobali alisema: “Sidhani, kwa kuwa Bashe anawafanya wananchi waamini kwamba kuwa CCM hakukuzuii kuikosoa Serikali na hata hicho alichokisema Bashe tulipaswa kukifanya sisi.”

Mbunge wa Ukonga (Chadema), Mwita Waitara aliona kuna kitu kimemkera Bashe hadi akaamua kutoa ya moyoni.

Hadi unaona Bashe kasema vile, ujue kimemkera. Kimemkuta akaona bora aseme ukweli. Na ni kweli kwamba hoja za wabunge, hasa wa CCM zinafia kwenye vikao vyao kwani wanaweza kuona baadhi ya hoja zinaweza kuisumbua Serikali,” alisema.

Waitara alisema mbunge anapokuwa ndani ya Bunge anakuwa huru kuwasilisha mawazo yake au ya wananchi anaowawakilisha.

“Lakini inaonyesha kwa sasa wabunge wanabanwa na wanasaidiwa kufikiri. Kitendo cha kuipeleka hoja katika vikao vya chama kinaonyesha kuna tatizo,” alisema.

“Inatakiwa hoja iletwe bungeni, sisi tukiijadili na kuona haina manufaa kwa Taifa au jamii ndio tuiondoe. Lakini kuishia katika hivyo vikao haina manufaa na inawafanya wabunge wasiwe huru kuzungumza na ndio maana Bashe kaamua kuweka hadharani na inaonyesha imemkera kwa kipindi kirefu.”

Waitara anatofautiana na mbunge wa Maswa Magharibi (CCM), Mashimba Ndaki aliyesema kila chama kina utaratibu wake wa kuwasilisha hoja binafsi bungeni. “Na kwetu, hakuna tatizo. Mtu akiwa na hoja yake inayoonekana ina mashiko, mbona inapita tu,” alisema.

“Haina maana kuipeleka katika kikao iwe cha CUF, Chadema au CCM ndiyo inakwenda kufa, ila inategemea kama kwetu CCM ulivyoijengea hoja na wengine wakiona ina manufaa kwa umma inaruhusiwa.”