VIDEO: Kariakoo yafurika, wafanyabiashara wasema maisha lazima yaendelee

Dar es Salaam. Wakati ugonjwa wa virusi vya corona ukichukua maisha ya watu wengine wawili, hali katika soko la Kariakoo na maeneo jirani haiakisi kuwepo kwa tishio la ugonjwa huo.

Watu wanaendelea na shughuli zao za kujitafutia riziki kama kawaida na hakuna kupeana nafasi ya kutosha kujikinga na ugonjwa huo zaidi ya baadhi kuonekana wakinawa mikono, ikiwa ni njia mojawapo ya kujikinga na wengine kuvaa barakoa usoni.

Barabara za maeneo hayo zilikuwa zikipitika kwa shida kutokana na uwingi wa watu wanaofanya manunuzi.

Wakati wataalamu wanashauri kutoshikana mikono wakati wa kusalimiana, hali ilikuwa tofauti jana. Wauzaji na wanunuzi walionekana wakishika bidhaa na wakati mwingine kubadilishana mikononi.

“Nisipokuja Kariakoo, nyumbani hawali wala watoto hawatasoma,” alisema mfanyabiashara ndogondogo aliyejitambulisha kwa jina la John Ungando.

“Nafahamu kuhusu corona, lakini nitafanyaje na hii ndio ofisi yangu na lazima nikutane na watu ili maisha yaende?”

Kuhusu namna gani wanajikinga dhidi ya ugonjwa huo ikizingatiwa wanakutana na watu wengi, Ungando alisema hana njia kubwa zaidi ya kumuomba Mungu amlinde asiambukizwe.

Naye Frank Shaban alisema wanalazimika kujiweka katika hatari ya maambukizi kwa sababu biashara ndiyo chanzo chao pekee cha uchumi wao.

Alisema ni vigumu kumwambia machinga asiwe katika mkusanyiko wakati anategemea uwepo wa watu wengi ili aweze kufanya biashara.

“Hakuna machinga anaweza kufanya shughuli zake nyumbani. Tunataka wateja na huku ndiko wanakopatikana kwa wingi, hayo mambo mengine ni ya kumuachia Mungu kama ni corona basi itatukuta hapa,” alisema Frank

Hali imeonekana kuwa mbaya zaidi Mtaa wa Congo ambao siku zote hufurika watu. Wamachinga wameendelea kupanga bidhaa zao chini au mezani huku wateja wakijazana kuchagua.

Pamoja na hilo, suala la kupeana nafasi ya mita moja kati ya mtu mmoja na mwingine limekuwa gumu kuzingatiwa, badala yake wengi hurundikana sehemu moja kuchagua nguo.

Mbali na wanunuzi, wapiga debe wa bidhaa zinazouzwa ni chanzo kingine cha kuongezeka msongamano katika mtaa huo na kusababisha iwe taabu hata kupishana.

Mmoja wa wanunuzi waliofuata bidhaa eneo hilo, Celina Mbaga alisema alikwenda kununua nguo za watoto.

Kuhusu tahadhari ya corona, Celina alisema anajitahidi kunawa mikono kila anapokuta maji kwa kuwa anafahamu anashika vitu vingi.

“Bahati nzuri katika maduka nje kuna maji na sabuni. Najitahidi kunawa kwa sababu najua nipo eneo lenye hatari na pia natembea na sanitizer,” alisema.

Biashara kuelekea Pasaka

Licha ya kwamba kuna watu wengi Kariakoo, wafanyabishara wamelalamika kuwa Pasaka ya mwaka huu si njema kwao.

Kilio ni kikubwa zaidi kwa wamiliki wa maduka waliodai kuwa machinga wanachangia zaidi biashara yao kuwa ngumu.

“Hao unaowaona kuna vitu muhimu wanavyofuata,” alisema mfanyabiashara aliyejitambulisha kwa jina la Issa Shayo.

“Si wengi wanaotaka nguo au viatu wala mapambo na wanaishia kwa wamachinga ndiyo maana nasema mwaka huu kwetu umeanza vibaya mno na sijui uko mbeleni hali itakuwaje.”