VIDEO-Maajabu ya Elifrida kwa familia ya Mallya

Maajabu ya Elifrida kwa familia hii

Muktasari:

Gazeti la Mwananchi la Juni 8 mwaka huu, lilichapisha habari kuhusu familia ya Edmund Mallya (68), baba wa watoto watano ambaye ameingia kwenye lindi la umaskini baada ya kukatwa mguu kwa sababu ya kuathiriwa na ugonjwa wa kisukari.

Gazeti la Mwananchi la Juni 8 mwaka huu, lilichapisha habari kuhusu familia ya Edmund Mallya (68), baba wa watoto watano ambaye ameingia kwenye lindi la umaskini baada ya kukatwa mguu kwa sababu ya kuathiriwa na ugonjwa wa kisukari.

Hata hivyo, mtoto Elifrida Paul (11), akiwa miongoni mwa wasomaji wa gazeti hili, alionyesha kuguswa na habari hiyo, hivyo kuamua kuchukua hatua bila kujua ni kwa namna gani atafanikisha lengo alilokuwa nalo ili kuisaidia familia ya Mallya.

Awali, katika mazungumza na Gazeti la Mwananchi, Mallya alisema kukatwa kwa mguu huo kumemsababishia ulemavu, hivyo kushindwa kuendelea na kazi ya udereva iliyokuwa ikimuingizia kipato ili kutunza familia yake.

Si Mallya pekee kwenye familia hiyo mwenye ulemavu, mkewe, Amina Hassan na mtoto wake wa mwisho Joachim Mallya pia ni walemavu, hali inayozidi kuongeza umaskini kwenye familia hiyo.

Katika kuonyesha lengo la kutaka kuisaidia familia ya Mallya linatimia, mtoto Elifrida anayesoma darasa la saba Shule ya Keland iliyopo Salasala jijini Dar es Salaam, aliamua kuchangisha fedha kwa ajili ya familia hiyo na kuzikabidhi.

Akizungumza na mwandishi wa makala haya, Elifrida anasema kama ilivyo ada, siku hiyo alikuwa akisoma gazeti kutokana utaratibu wa baba yake kurudi na magazeti nyumbani ndipo alipokutana na taarifa hiyo iliyogusa moyo wake.

“Mdogo wangu ndiye alinishtua kwamba ona hawa watu, ikabidi niangalie kwa makini ule ukurasa na kuisoma kwa kina taarifa ile nikajiona ninaweza kusaidia chochote hata kama kisingetosheleza hitaji la yule baba la Sh253,000 za dawa ili kunusuru mguu wake usikatwe tena,” anasema Elifrida.

“Binafsi huwa ninatunza fedha kwa ajili ya matumizi ya baadaye, hivyo kwenye akiba yangu kulikuwa na fedha kidogo nilizopata kwenye kipaimara changu; nikaona nichukue kiasi ili nichangie maana pale kwenye gazeti kulikuwa na namba ya simu.”

Katika akiba hiyo alichomoa Sh50,000 kwa ajili ya kuchangia, lakini kabla hajafanya hivyo akapata wazo wa kuwashirika watu wa ndani ya familia yake.

Haikuwa ngumu kwake kuwaelezea wazazi wake na ndugu zake wanaoishi nyumba moja, wote wakavutiwa na wazo hilo na kila mmoja akatoa kile alichokuwa nacho.

“Nakumbuka baba na mama walitoa Sh20,000, bibi alitoa Sh30,000, dada angu alitoa Sh1,000 na mdogo wangu aliyenionyesha ile taarifa alichangia Sh800. Nilikusanya fedha zote hizo lakini nikaona bado kuna kitu zaidi naweza kufanya, hebu niwashirikishe na wanafunzi wenzangu shuleni.

“Nashukuru Mungu walimu walinielewa na kuniruhusu kuliwasilisha kwa wanafunzi wenzangu na kwa pamoja tukaweka muda maalumu wa kuchangisha fedha kwa kila mmoja kutoa kile alichokuwa nacho na hatimaye tukatimiza lengo la kupata kiasi ambacho baba huyu alisema anahitaji kwa ajili ya dawa,” anasema Elifrida.

Mbali na moyo wa utoaji na kupenda kusaidia jamii, mtoto huyu ndoto yake ni kuwa daktari na amekuwa akipendelea kuangalia filamu na kusoma vitabu vinavyohusu magonjwa na matibabu yake.

Nje ya hayo Elifrida pia ni msomaji mzuri wa magazeti na anajifunza pia uandishi wa vitabu akiwa na lengo la kuandika kitabu cha hesabu, somo analolipenda licha ya kufanya vizuri kwenye masomo yake yote.

Uongozi wa shule

Geofrey Shanjila ambaye ni mwalimu wa darasa wa Elifrida, anasema mtoto huyo alimfuata kumueleza nia yake ya kuchangisha fedha, lakini akamuelekeza awasilishe wazo hilo kwa uongozi wa shule kwa kuwa wanafunzi hawaruhusiwi kwenda na fedha shuleni.

“Wanafunzi hapa hawaruhusiwi kuja na fedha, lakini alipokuja na wazo na kuona ni zuri nikamshauri aende mwenyewe kwa meneja na kweli akaruhusiwa basi utekelezaji wake ukaanza,” anasema mwalimu Shanjila.

Anasema mtoto huyo, aliomba kuwasilisha hilo kwa wanafunzi wenzake wa darasa la saba tu na akaruhusiwa hata kubandika matangazo darasani, akawa anapata muda wa kuzungumza na wanafunzi wenzake.

“Aliwahamasisha na wakahamasika hasa wakaanza kuchangia, hili suala limenipa faraja kwamba, kumbe kuna watoto wanaweza kuwa na uelewa mpana wa mambo maana sio rahisi kwa mtoto anayesoma shule nzuri anatoka familia bora akakumbuka kuwasaidia wenye uhitaji,” anasema Shanjila.

Mwalimu huyo alieleza kuwa licha ya moyo wa kupenda kujali ya wengine, ana uwezo mkubwa darasani na mara zote amekuwa akiuliza maswali ambayo yako juu ya upeo wa mtoto mwenye umri kama wake.

Akimzungumzia mtoto huyo, mwalimu mkuu wa Shule ya Keland, Julius Nyamsangya anasema, “nimefurahi, sikujua kama kuna watoto wanaweza kusoma gazeti na kuona uhitaji wa mtu mwingine na kuguswa. Ameonyesha mfano mzuri kwa kuguswa na changamoto iliyopo kwenye jamii. Ametushangaza moyo wake, kwanza hana kazi, lakini ameguswa hadi kuwahamasisha wenzie kuchanga.

“Yuko vizuri kitaaluma, pia ni mwanafunzi anayefanya vizuri darasani, akishika namba moja siku zote, tulifanya mtihani wa Mock wa Wilaya ya Kinondoni, yeye ndiye alishika namba moja, tulishiriki pia kwenye mtihani unaoratibiwa na Shule ya Feza aliweza kuingia kwenye 10 bora na kutuletea medali shuleni kwetu. Kwa kifupi ni mtoto mwenye akili ya darasani na sasa ametuonyesha pia hata jamii, Mungu aendelee kumuongoza,” alisema mwalimu mkuu huyo.


Kauli ya wazazi

Mama wa mtoto huyo, Edwardina Karugendo anasema Elifrida anapenda kusaidia na siku zote amekuwa akijitoa kwa wengine.

“Sisi ni wanunuzi wa Gazeti la Mwananchi kila siku, kwa hiyo siku hiyo mdogo wake ndiye aliona habari na kumuonyesha dada yake ambaye aliichukulia kwa uzito, aliguswa akaja kuniambia atatoa fedha kwenye kibubu chake ili kunusuru mguu wa huyo baba usikatwe,” anasema mama mzazi wa Elifrida.

“Huyu ni mtoto anayependa kusaidia, hata kanisani ni mtoto pekee ambaye amekuwa akichangia michango mbalimbali kwenye harambee; ana ule uthubutu wa kunyoosha mkono na kusema atachangia kiasi gani. Alishawahi kuchangia mfuko wa saruji kwenye ujenzi wa kanisa.”

Baba mzazi wa mtoto huyo, Emmanuel Paul anasema, “suala hili nimelichukulia kwa uzito mkubwa, ukiangalia umri wake haulingani na anayofanya, naweza kusema ni uzalendo wa hali ya juu. “Tunamshukuru Mungu na tunazidi kumtia moyo azidi kuendelea hivi, ameonyesha mfano wa aina yake na tunapaswa kumhamasisha azidi kuguswa na matatizo ya wengine.”


Familia ya Mallya yashukuru

Amina ambaye ni mke wa Mallya alimshukuru mtoto huyo kwa kuguswa na tatizo la familia yake huku akimuomba aendelee kuyagusa maisha ya wenye uhitaji na matokeo yake atayapata.

“Kiukweli nimeshangazwa kusikia mtoto wa miaka 11 ameyafanya haya, nafahamu watu wazima wengi ndio wanasoma magazeti lakini aliyeguswa na changamoto inayotukabili ni mtoto huyu, nina kila sababu ya kuwashukuru wazazi wake kwa uzao huu na malezi waliyompatia, wamemuwekea misingi mizuri.

“Sina la kusema zaidi ya kumuombea kwa Mungu amzidishie pale alipopunguza na azidi kugusa maisha ya wenye uhitaji, malipo yake atayapata siku moja maana dua zetu tunazielekeza kwake,” anasema Amina.