VIDEO: Makonda ataja sababu mafuriko Dar

Muktasari:

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema shughuli za uchimbaji mchanga kwenye mito, utupaji wa taka na ujenzi wa nyumba mabondeni ni kati ya sababu maeneo mbalimbali ya Mkoa huo kukumbwa na mafuriko.


Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema shughuli za uchimbaji mchanga kwenye mito, utupaji wa taka na ujenzi wa nyumba mabondeni ni kati ya sababu maeneo mbalimbali ya Mkoa huo kukumbwa na mafuriko.

Makonda ametoa kauli hiyo leo Jumatano Desemba 18, 2019  jijini Dar es Salaam katika ziara ya  kamati ya ulinzi na usalama kukagua madhara ya mvua iliyonyesha jana na kusababisha baadhi ya shughuli kusimama.

Mkuu huyo wa Mkoa ametembelea maeneo ya Kigogo, Tandale, Sinza (mto ng'ombe) na Jangwani ambako shughuli za uchimbaji wa mchanga hufanyika.

Makonda amesema Serikali imeanza kukarabati miundombinu ya barabara na madaraja yaliyoharibiwa na mvua.

"Ninatoa wito kwa wananchi kuacha kutupa taka au kuchimba mchanga kwenye mito. Haya ndiyo madhara yake na yanawaadhibu wenyewe. Ninatoa wito kwa mara nyingine, wananchi wanaoishi mabondeni wahame maeneo hayo, mvua hizi zipo na bado zinakuja nyingi," amesema Makonda.

Amesema Serikali ina mpango wa kujenga bonde la Msimbazi ili boti ziweze kupita  sambamba na kuinua daraja la Jangwani.

Akiwa Tandale, Makonda alipokea malalamiko ya wananchi kwamba ujenzi wa  daraja umesababisha wakumbwe na mafuriko kutokana na mkandarasi kuziba sehemu ya mto huo na maji kwenda katika makazi ya watu.

"Miaka ya nyuma hapa hatukuwa na mafuriko lakini tangu ujenzi wa daraja hili ulipoanza, mvua ikinyesha maji yanakuja kwetu. Tatizo mkandarasi kaziba sehemu ambayo inapitisha maji," amesema mkazi wa Tandale, Said Mustapha.

Akijibu malalamiko hayo Makonda amekiri ujenzi huo kusababisha mafuriko, kwamba amekuwa akiwasisitiza makandarasi kufanya kazi zao kwa wakati ili kuondoa kero kwa wananchi.