VIDEO: Meya ataja sababu kuwataka wajumbe kikaoni kuvua barakoa
Muktasari:
- Meya wa manispaa ya Moshi, Juma Raibu amesema aliwataka wajumbe waliokuwa wamevaa barakoa katika kikao cha bajeti cha baraza la madiwani manispaa hiyo kuzivua kwa sababu uvaaji huo huongea hofu ya ugonjwa wa corona kwa wananchi.
Moshi. Meya wa manispaa ya Moshi, Juma Raibu amesema aliwataka wajumbe waliokuwa wamevaa barakoa katika kikao cha bajeti cha baraza la madiwani manispaa hiyo kuzivua kwa sababu uvaaji huo huongeza hofu ya ugonjwa wa corona kwa wananchi.
Ameeleza hayo leo Alhamisi Januari 28, 2021 baada ya kupitisha bajeti ya manispaa hiyo, akibainisha kuwa pamoja na kutakiwa kuchukua tahadhari haitakiwi kupeana hofu
"Nimeona katika baraza madiwani karibu thelathini, wapo viongozi wa serikali na viongozi wa vyama walioalikwa wote hawa hawajavaa barakoa hata mmoja, lakini limekuja kundi la watu wamevaa barakoa jambo ambalo wanaamini halmashauri hii ina corona.”
"Nimewaambia wavue waendelee kuamini kuwa corona ipo na tujiendelee kujikinga lakini manispaa ya Moshi haina corona, tuendelee kujikinga katika mambo mengine ila tusitiane hofu, katika baraza langu la manispaa sitaruhusu mtu yeyote kuingia na barakoa katika kikao changu kwani ninaamini tuko salama,” amesema.
Akizungumzia hatua ya kuamriwa kuvua barakoa mmoja wa wajumbe katika kikao hicho, Mwanahawa Amir amesema alipokea agizo hilo na kwamba anaamini Tanzania ipo salama kwa kuwa madiwani wote waliokuwa katika kikao hicho walikuwa hawajavaa barakoa.