VIDEO: Mtihani mama adai kutakiwa kuwakamata wanaodaiwa kumlawiti mtoto wake

Muktasari:

  • Mtoto alifanyiwa unyama huo Jumapili Februari 18, 2024 saa 12:30 jioni na mzazi wake akaenda kuripoti Kituo cha Polisi Buhongwa.

Mwanza. Katika hali isiyo ya kawaida, mkazi wa Mtaa wa Buguku Kata ya Mkolani jijini Mwanza, (jina linahifadhiwa) amelalamikia kutakiwa kuwakamata watuhumiwa wanne wanaodaiwa kumlawiti mtoto wake wa kiume (16) baada ya kutoa taarifa za tukio hilo katika Kituo cha Polisi Igogo jijini humo.

Hata hivyo, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, Gideon Msuya amekanusha taarifa ya jeshi hilo kumtaka mama wa mtoto huyo awakamate watuhumiwa badala yake maofisa walimtaka atoe ushirikiano kwa jeshi hilo pale atakapohitajika.

Msuya amesema baada ya kumtia mbaroni kijana mmoja anayetuhumiwa, jeshi hilo lilifanya paredi ya utambuzi ndipo mwanafunzi huyo alipodai kwamba aliyekamatwa siyo miongoni mwa waliomfanyia unyama huo, hivyo, akaachiwa kwa dhamana.

“Huyo aliyelawitiwa alikamatwa mtu mmoja lakini alivyofanyiwa paredi la utambuzi yeye mwenyewe akasema siyo huyo, kwa hiyo akapatiwa dhamana hata taarifa ambazo ninazo hata leo ameenda kituoni kuripoti.

“Taarifa za kwamba aliambiwa akawatafute siyo za kweli, yeye aliambiwa atoe ushirikiano kwa sababu yeye ndiye anayewafahamu. Kwa hiyo nimemuagiza mkuu wa kituo cha Igogo na OC-CID (Ofisa upelelezi wilaya ya Nyamagana) waendelee kuwasaka watuhumiwa,” amesema Msuya.

Awali, akizungumza na Mwananchi, mama wa mtoto huyo amesema baada ya mtoto wake kufanyiwa unyama huo Jumapili Februari 18, 2024 Saa 12:30 jioni, alienda kuripoti Kituo cha Polisi Buhongwa na kutakiwa kwenda Kituo cha Igogo jijini humo ambako anadai alielekezwa na askari kwenda kuwakamata watuhumiwa.

Amesema katika Kituo cha  Igogo alifungua jalada (RB) namba IGO/RB/918/2024 lenye shtaka la kulawiti kisha kupatiwa fomu namba tatu (PF3) ili mtoto wake akatibiwe.

Amesema alimpeleka mwanawe Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana (Butimba) na kufanyiwa uchunguzi na usafi na daktari, aliyemtaja kwa jina moja la Dk Pahicia ambaye alimthibitishia mwanaye ameingiliwa sehemu ya haja kubwa kisha, hivyo alimwandikia dawa za kutumia.

Amedai baada ya majibu ya vipimo kutolewa walirejea nyumbani, siku iliyofuata alienda naye Kituo cha Polisi Igogo kujua hatua zilizochukuliwa dhidi ya watuhumiwa na afande (jina linahifadhiwa)  alimtaka kuwakamata watuhumiwa kisha kutoa taarifa polisi ili wakawachukue.

“Afande akaniambia wamemkamata (jina linahifadhiwa) lakini amekana kumuingilia, hivyo kinachotakiwa ‘mjitahidi sana kwa hali na mali wale watuhumiwa uwakamate utakapowakamata unipigie simu mniambie,” amedai mama huyo.


Tukio lilivyotokea

Akisimulia ilivyokuwa, mwanafunzi huyo (16) amesema ilikuwa Jumapili akitokea nyumbani kwenda Mtaa wa Utemini Kata ya Mkolani jijini humo, kuazima daftari kwa rafiki yake, ndipo alipozingirwa na vijana hao wanne huku akimzonga na kumtaka kufanya wanachokitaka.

Amesema majeraha aliyopata kwa kufanyiwa ukatili huo yamemsababishia maumivu sehemu zake za siri, mgongoni jambo linalosababisha akalie sehemu ya mgongo na siyo makalio huku mtihani mkubwa anaopitia ni pamoja na unyanyapaa na kuchekwa na wanafunzi wenzake shuleni.

Huku akiwataja baadhi ya watuhumiwa kwa jina moja, mwanafunzi huyo anasema walimshika kwa nguvu na kumfunga kitambaa mdomoni kisha kumpeleka mlimali na kumfanyia unyama huo.

“Wakanishika huku wamenifunika kitambaa mdomoni wakanipeleka mlimani wakaniambia vua nguo, nikakataa wakanipiga makofi kisha wakanivua kubazi zangu na shati. Mmoja akaniambia kwamba lazima tukufanyie kitendo cha ukatili (kulawiti) huku wakinipiga fimbo.

 “Walipomaliza wakaniambia chukua shati lako sisi tunaondoka wakaondoka ndiyo nikaondoka kurudi nyumbani, nilipofika sikusema kwa sababu walinitishia kwamba wataniua ndiyo maana nilipokuwa naulizwa nilikuwa najibu hawajanifanyia kitu,” amesema mwanafunzi huyo huku akibubujikwa machozi.

Amesema kutokana na hofu ya kuuawa aliyopewa na watuhumiwa hao, alipofika nyumbani alimficha mama yake, hata hivyo, siri ilifichuka kutokana na kitendo alichofanyiwa kugunduliwa na dada yake ambaye alianika ukweli wote mbele ya mama yake. 

Kwa huzuni, mwanafunzi huyo amesema amesikitishwa na kitendo cha Jeshi la Polisi kumwachia kwa dhamana mtuhumiwa aliyekamatwa miongoni mwa waliomfanyia ukatili huo huku akisema uwepo wake mtaani unamfanya ahofie usalama wa maisha yake.

“Mama alivyokuja akawa anataka kunichapa ndiyo nikasema ukweli akanipeleka polisi baadaye tukaenda hospitalini, walikuwa vijana wanne akiwamo …. mmoja wao alikamatwa na polisi kisha wakamwachia. Walikuwa wananifanyia kitendo hicho kwa awamu,” amesema.

Mtihani mama adai kutakiwa kuwakamata wanaodaiwa kumlawiti mtoto wake

“Najisikia vibaya sana kwa sababu waliyemkamata wamekuwa wepesi sana kumwachia, naomba Serikali na Rais Samia anisaidie wachukuliwe hatua za kisheria kwa sababu wengine ninapowaona mtaani ninaogopa sana. Hata shuleni ninaposoma wenzangu wanakuwa wananiuliza wewe ndiyo umelawiti ninakataa,”


Wananchi walaani

Mkazi wa Mtaa wa Buguku jijini humo, Selestine Batinagwa amesema tukio hilo ambalo linafedhehesha limesababishwa na mmonyoko wa maadili katika jamii huku akiomba Serikali na mamlaka za usalama kufanya operesheni maalumu katika eneo hilo ili kutokomeza makundi ya vijana wanaojihusisha na uhalifu.

“Haya yote yanasababishwa na uwepo wa vijana ambao wanafanya uhalifu maeneo haya ikiwamo kuvuta bangi bila kuchukuliwa hatua, matokeo yake wameanza kwa kumfanyia ukatili mtoto huyu wa kiume, hatujui kesho itakuwaje na hatujui mamlaka za kisheria wakiwamo polisi wanafanya nini,” amehoji Batinagwa.

 Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Buguku jijini humo, Maduhu Sultani pamoja kukiri tukio hilo kutokea katika mtaa wake amesema jitihada za kuwasaka watuhumiwa zinaendelea huku akidokeza kwamba mitego imewekwa kuwanasa.

“Tukio lilifanyika kwa mtoto wa mtaa wangu na baada ya kufahamika tulitoa taarifa kituo cha polisi Buhongwa, mmoja wa vijana alikamatwa lakini akasema siyo yeye kwa hiyo akaachiwa. Kwa hiyo kupata taarifa sahihi zaidi nenda kituo cha polisi ndiyo wahusika kwa hiyo ukienda pale watakupa,” amesema Sultani.

Takwimu zilizopo kutoka Jeshi la Polisi zinaonyesha kwamba watoto 537 walilawitiwa nchini Tanzania kwa mwaka 2016, idadi ambayo imepanda hadi kufikia watoto 1,114 kwa mwaka 2021, ikiwa ni mara mbili ya ile iliyorekodiwa mwaka 2016.