VIDEO: Nyuki wawatawanya waombolezaji makaburini

Muktasari:

  • Ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu Daudi Mohamed wakazi wa kata ya Kileleni wilayani Handeni mkoani Tanga wametimua mbio na kuacha jeneza lenye mwili wake baada ya eneo la makaburi kuvamiwa na nyuki.

Handeni. Ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu Daudi Mohamed wakazi wa kata ya Kileleni wilayani Handeni mkoani Tanga wametimua mbio na kuacha jeneza lenye mwili wake baada ya eneo la makaburi kuvamiwa na nyuki.

Tukio hilo limetokea leo mchana Jumanne Februari 16, 2021 na hadi saa 11 jioni mazishi yalikuwa hayajafanyika

Mmoja wa shuhudia wa tukio hilo, Abdallah Mchakato amesema nyuki hao walikuwepo tangu saa 8 mchana walipofika makaburini kuchimba kaburi lakini walizidi baada ya ndugu na jamaa kufika eneo hilo.

"Mwili tumeuacha imebidi tutimue mbio wale nyuki si wa kawaida, kuna watu wamezidiwa na kudondoka sijui hali zao huko..., mtaa mzima wamejifungia ndani,” amesema.

Mganga mkuu wa hospitali ya mji Handeni, Hudi Shehedadi amesema amepokea watu tisa waliojeruhiwa na nyuki na kwamba wawili walikuwa na majeraha zaidi, “wengine saba walitibiwa na kuruhusiwa.”

Nyuki wawatawanya waombolezaji makaburini

Msemaji wa familia, Rashid Kilagula  amesema tukio hilo halina uhusiano na imani za kishirikina na kuwataka ndugu, jamaa na marafiki kutokuwa na hofu.