VIDEO: Rais Samia ahesabiwa Sensa, atoa ujumbe kwa Watanzania
Muktasari:
- Sensa ya Watu na Makazi nchini Tanzania imeanza kuanzia saa 6:01 usiku leo Jumanne, Agosti 23, 2022 ikiwemo makarani wa sensa kufika Ikulu ya Chamwino, Mkoa wa Dodoma kumhesabu Rais Samia Suluhu Hassan.
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amekuwa miongoni mwa Watanzania waliohesabiwa katika Sensa ya Watu na Makazi iliyoanza saa 6:01 usiku wa leo Jumanne, Agosti 23, 2022.
Mkurugenzi Mkuu wa ofisi ya Takwimu Tanzania (NBS), Albina Chuwa na Kamishna wa Sensa ya Watu na Makazi mwaka 2022, Anne Makinda wameongoza timu kwenda Ikulu ya Chamwino, Mkoa wa Dodoma kwa ajili ya kumhesabu Rais Samia.
Mara baada ya kumaliza kumhesabu, kazi iliyodumu si zaidi ya nusu saa, Rais Samia amezungumza na waandishi wa habari akisema, “nimemaliza kuhesabiwa, ni kweli maswali ni mengi kidogo lakini yanajibika, ombi langu kwa wananchi ni kuweka taarifa zetu mapema.”
“Kwa wale ambao hawajapata maswali yale yaliyotolewa na ofisi yetu ya NBS, wayatafute na kuyaandaa ili karani akifika akiuliza mnakwenda tu na majibu, ikiwemo unatumia bima gani, una namba ya NIDA au Mzanzibar,” amesema
Rais Samia amemaliza kuzungumza kwa kusema, “niitakie nchi yetu sensa njema, makarani wetu wafanyekazi kwa ufanisi na wananchi wajitokeze kutoa majawabu yanayotakiwa.”