VIDEO: Simanzi kifo cha mwanafunzi

Simanzi kifo cha mwanafunzi

Muktasari:

  • Wakati wanafunzi wa darasa la saba wakianza mitihani ya kuhitimu elimu yao ya msingi jana, mwanafunzi mwenzao wa Shule ya Msingi Mtumba, Farida Makuya (16) ameshindwa kufikia hatua hiyo baada ya kudaiwa kuuawa na watu wasiojulikana.


Dodoma. Wakati wanafunzi wa darasa la saba wakianza mitihani ya kuhitimu elimu yao ya msingi jana, mwanafunzi mwenzao wa Shule ya Msingi Mtumba, Farida Makuya (16) ameshindwa kufikia hatua hiyo baada ya kudaiwa kuuawa na watu wasiojulikana.

Mtoto huyo anadaiwa kuuawa usiku wa kuamkia juzi nyumbani kwao Mtumba, wakati mama yake mzazi ametoka kwenda kwenye biashara zake.

Akizungumza na Mwananchi jana kwenye msiba huo, mjomba wa Farida, Anderson Makuya alisema usiku wa kuamkia juzi alipokea simu kutoka kwa ndugu zake wakimjulisha kuwa mpwaye amepigwa na watu wasiojulika na amepelekwa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, lakini alipoteza maisha wakiwa njiani.

“Leo (jana) alipaswa kufanya mitihani yake ya darasa la saba lakini ndiyo hivyo tena, huyu ni mtoto wa dada yangu akiwa ni wa pili kuzaliwa,” alisema Makuya.

Siku ya tukio

Akisimulia hali ilivyokuwa siku ya tukio, Makuya alisema mama wa marehemu alienda kuuza pombe za kienyeji katika klabu kilichopo mtaa wa Mtumba.

Alisema dada yake siku zote hufanya biashara hiyo kuanzia jioni hadi usiku na huwa anarudishia tu mlango wake ili akirudi usiku, iwe rahisi kuingia ndani, asiwasumbue kuwaamsha watoto.

Mjomba huyo alisema dada yake alirudi majira ya saa nane usiku na aliingia moja kwa moja ndani, na alipowasha tochi na kuangalia chini, akakuta kuna michirizi ya damu.

“Alishtuka, akatazama sehemu waliyolala watoto wake akaona wako wanne na mmoja hayupo.

“Akatoka na kuanza kufuatilia michirizi hiyo ilikoelekea hadi alipofika kwenye uwanja wa mpira (ulio jirani), akamkuta Farida ametupwa hapo huku damu zikimtoka kichwani, akapiga kelele watu wakakusanyika.

“Walimchukua na kumpeleka zahanati ambako walielekezwa waende Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, lakini kabla ya kufika mtoto akawa amefariki dunia,” anasimulia mjomba huyo.

Makuya anasema inaonekana Farida alipigwa na kitu kizito kichwani.

“Tunahisi walimpiga na figa, kwa sababu pale nje wanapopikia palikuwa na mafiga matatu, lakini moja lilikutwa ndani ya nyumba likiwa na damu nyingi, hivyo kwa haraka sisi tumehisi hili figa ndilo walilitumia kumpigia,” alidai mjomba mtu huyo.

Hata hivyo, Makuya anasema wakati yote hayo yanafanyika, wadogo zake Farida aliokuwa amelala nao ndani, hawakushtuka, jambo wanalohisi huenda walipuliziwa dawa ya usingizi.

“Hawakujua chochote, hata damu ziliwarukia lakini hawakujua chochote mpaka mama yao alipokuwa akiomba msaada ndiyo waliamka, hatujui labda walipuliziwa dawa,” alisema Makuya.

Alikuwa anazungumzia mtihani

Akisimulia tukio hilo, jirani wa familia hiyo, Ezekia Mwilima alisema mpaka jioni siku ya tukio alikuwa na Farida wakizungumzia mitihani na alivyokuwa amejipanga kufanya vizuri katika mitihani yake.

“Niliachana naye saa moja usiku akaenda nyumbani kwao, lakini mama yake hakuwepo kwa sababu huwa anaenda kuuza pombe.

“Baadaye usiku nikasikia makelele ya mama yake akiomba msaada, nilikuwa mtu kwa kwanza kutoka nikakuta damu nyingi zimetapaa, ikabidi tumchukue kumpeleka hospitali.

“Wakati tupo njiani ndio mjukuu wangu huyu akafariki, nimeumua sana, alikuwa mtu mzuri sana, alikuwa akinisaidia kufanya usafi hapa pamoja na kunifulia nguo zangu,” alisema jirani huyo.

Jirani mwingine, Jumanne Mkoyi alisema baada ya tukio walifika kwake kuomba gari kwa ajili ya kumpeleka hospitali majeruhi.

“Nilimpakia kutokea katika zahanati lakini damu zilikuwa zinamtoka nyingi, bahati mbaya hatukifika hospitali ya rufaa Dodoma akawa amekufa, nimeumia sana,” alisema Mluvya.

Ni tukio la nne

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mtumba, Nathan Mlunya alisema tukio hilo la mauaji ni la nne kutokea katika kipindi cha miaka mitatu katika mtaa huo.

“Mbaya zaidi, Mkuu wa Wilaya ameshafika, OCD ameshafika, lakini wahusika bado hatujawapata. Tukio la huyu mtoto linasikitisha sana, leo (jana) alikuwa afanye mtihani wa darasa la saba, lakini tunamzika, watu waliofanya wapo tu, tunasikitika sana,” alisema mwenyekiti huyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Martin Otieno alipotafutwa kwa simu kuzungumzia tukio hilo simu yake iliita bila majibu.

Mwananchi pia lilimtafuta Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule ambaye naye simu yake haikujibiwa.

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri alipopigiwa aliomba atumiwe ujumbe.

“Hellow tafadhali tuwasiliane baadaye. Ikiwa ni dharura naomba utume message,” ulieleza ujumbe huo. Alipotumiwa ujumbe wa kuulizwa kuhusu tukio hilo, hadi tunakwenda mitamboni hatukupata majibu.

Maziko ya mwanafunzi huyo yalifanyika jana saa 9 alasiri katika makaburi ya Mtumba, baada ya mwili wake kusaliwa katika Kanisa la Anglikana la Mtakatifu Thomas, Mtumba.

Waomba kituo cha Polisi

Katika hatua nyingine, Mlunya alisema kutokana na matukio kuzidi, wanaiomba Serikali iwajengee kituo cha polisi.

“Watu wanakabwa mchana na usiku, kituo kipo mbali na hapa, kipo Mji wa Serikali, tunaomba tuangaliwe na sisi, watu wanakufa wanaumizwa,” alisema.

Uwezo mkubwa darasani

Akimzungumzia Farida, Mwalimu wake wa darasa, Paulo Sudai alisema wamepokea kwa masikitiko kifo cha mwanafunzi huyo.

Sudai ambaye ni mwalimu wake somo la maarifa ya jamii, alisema Farida alikuwa na uwezo mkubwa darasani na miaka yote alikuwa hatoki katika nafasi 10 za juu.

“Alikuwa mstaarabu sana, ilifika mahali tukampa ukiranja wa afya na mazingira, kimsingi tumehuzunika kwa kifo hiki. Hata mitihani ya mwisho ya shule alifanya vizuri, naye tulijua anakwenda sekondari,” alisema mwalimu huyo.

“Alikuwa anajiamini sana katika utendaji kazi wake na sisi walimu tulikuwa tunamtegemea kwenye kuzungumza na wenzake na alikuwa mwakilishi wa klabu mbalimbali shuleni. Alikuwa msafi muda wote, ndiyo maana tukampa ukiranja wa kitengo cha afya.”

Kutokana na kifo cha mwanafunzi huyo, uongozi wa shule hiyo kwa kuwatumia viongozi wa dini na madaktari, jana walizungumza na wanafunzi ili kuwaweka vizuri kisaikolojia kabla ya kuingia kwenye chumba cha mtihani.

“Mwalimu wetu mkuu mapema kabisa tulifanya kikao tukalijadili hili, tukaona kuna haja ya kuwaandaa watoto kisaikolojia, tunaamini kwa kufanya hivyo, tutakuwa tumewasaidia kufanya mitihani yao kwa utulivu,” alisema Paulo.

Tukio lingine

Mwalimu huyo alisema kuna tukio lingine linalofanana na hili lililotokea mwaka jana kwa mwanafunzi aliyekuwa darasa la saba, Mariamu Madumba aliyevamiwa na kujeruhiwa mkono wa kulia kwa panga na mtu ambaye hakumfahamu.

“Hali ile ilimfanya mwanafunzi yule ashindwe kuandika na alifanya vibaya katika mtihani wake wa Taifa,” alisema.