VIDEO: TRA waanza kumfuatilia Kakobe

TRA YAJITOSA SAKATA LA ASKOFU KAKOBE

Muktasari:

Kichere amemwomba Askofu Kakobe kutoa ushirikiano kwa maofisa wa TRA watakaomtembelea kwa ajili ya shughuli hiyo ya ukaguzi.

Dar es Salaam. Siku chache baada ya kiongozi wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship Askofu Zachary  Kakobe kusema kuwa ana fedha nyingi kuliko Serikali, Mamlaka ya Mapato nchini TRA imejipanga kuanza kufuatilia ulipaji wake wa kodi.

Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kichere amesema mamlaka yake imeipokea kwa furaha kauli ya Askofu Kakobe na inataka kujiridhisha vyanzo vya utajiri huo.

Kichere amesema TRA inafahamu kuwa shughuli za kidini hazitozwi kodi lakini inataka kufahamu kama fedha hizo za Askofu Kakobe zinatokana na sadaka pekee au kuna shughuli nyingine za kiuchumi.

"Tumefuatilia hakuna kumbukumbu za Askofu Kakobe kulipa kodi, sasa tumeona tumfuate maofisa wetu wakajiridhishe kama fedha hizo anazozizungumzia zinatokana na sadaka,"

"Na kama hana shughuli zozote za kiuchumi ikiwa ina maana utajiri huo unatokana na sadaka ni jambo la kushtua kidogo lakini sisi tutaishia hapo,"

Amesema katika taarifa za mamlaka hiyo wapo watu wengi wenye fedha nyingi na kumbukumbu zao za kodi zipo lakini Askofu Kakobe si miongoni mwao.

Kichere amemwomba Askofu Kakobe kutoa ushirikiano kwa maofisa wa TRA watakaomtembelea kwa ajili ya shughuli hiyo ya ukaguzi.

Kuhusu kwanini uhakiki huo umekuja sasa Kichere amesema ni baada ya kusikia ana fedha nyingi kuliko Serikali wakati anafahamika ni kiongozi wa taasisi ya dini.