VIDEO: Walimu saba wanaishi nyumba moja ya vyumba vitatu

Walimu saba wanaishi nyumba moja ya vyumba vitatu

Muktasari:

  • Walimu saba wa Shule ya Msingi Mikocheni iliyopo kata ya Arusha chini Wilaya Moshi mkoani Kilimanjaro wanaishi katika nyumba moja yenye vyumba vitatu.

Moshi. Walimu saba wa Shule ya Msingi Mikocheni iliyopo kata ya Arusha chini Wilaya Moshi mkoani Kilimanjaro wanaishi katika nyumba moja yenye vyumba vitatu.

Walimu hao ambao wanawake ni wanne na wanaume watatu wameeleza hayo leo Jumatano Januari 20, 2021.

Melckizedeck Temba amesema wanafanya kazi katika mazingira magumu na wanaishi kwa hofu kutokana na ubovu wa nyumba hiyo na kuna muda nyoka huingia ndani.

Amesema mazingira ya shule siyo rafiki kwa kufundisha kutokana na darasa moja kuwa na wanafunzi zaidi ya 170 jambo walilodai kuwapa wakati mgumu kusahihisha kazi za wanafunzi hao.

Walimu saba wanaishi nyumba moja ya vyumba vitatu

Mwalimu mwingine, Denis Kisaka amesema mbali na wao saba, kuna walimu  wengine wawili wameongezeka.

"Walimu wa kike ndoa zao zipo hatarini kuvunjika kwa  kuwa wanashindwa kuhamisha familia na kuja kuishi nao katika chumba kimoja tunaomba tusaidiwe kuboresha mazingira ya kuishi  ili tuweze kufundisha  bila mawazo,” amesema Kisaka.

Frida Mtui amesema  nyumba wanayoishi haina choo  wala bafu na kwamba wanalazimika kutumia vyoo vya wanafunzi.

Diwani wa Arusha Chini (CCM), Leonard  Waziri amesema shule hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi na kwamba anaanza kutatua shida ya upatikanaji wa chakula.

"Wanafunzi wa shule hii hawapati chakula cha mchana na nimeanza kutoa tani tano za mahindi kwa ajili ya chakula cha  mchana kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari,” amesema Waziri.