VIDEO: Wapinzani wampongeza Mbowe kuhusu maridhiano

Muktasari:

Baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani nchini Tanzania wamempongeza mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kutoa ombi la kuwepo kwa maridhiano ya kitaifa mbele ya Rais John Magufuli.


Dar es Salaam. Baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani nchini Tanzania wamempongeza mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kutoa ombi la kuwepo kwa maridhiano ya kitaifa mbele ya Rais John Magufuli.

Mbowe alitoa kauli hiyo Jumatatu ya Desemba 9, 2019 katika maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru wa Tanganyika baada ya kupewa nafasi na kiongozi mkuu huyo wa nchi kutoa salamu.

Kauli ya Mbowe ambaye leo Jumatano Desemba 18, 2019 anagombea uenyekiti wa Chadema katika uchaguzi unaofanyika katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, imeonekana kuwakuna viongozi hao waliotumia nafasi ya kutoa salamu katika mkutano huo, kumpongeza mbunge huyo wa Hai.

Mwenyekiti wa chama cha UPDP, Fahmi Dovutwa alianza kwa kusifu mkutano mkuu huo wa Chadema, “mwenyekiti alizungumzia maridhiano akiwa Mwanza kwenye maadhimisho ya siku ya Uhuru. Mimi nasema kwa watu mliopo hapa, endeleeni na kasi yenu.”

“Wale ambao hawajasikia na kujua historia ya Burundi, Prince Rwegasore hakufanya mkutano. “Wakati wa kuelekea uchaguzi wa Burundi, Frodebu haikuwa kwenye vyama vilivyohesabiwa kwa sababu walikuwa chini.”

“Kwa mazungumzo aliyoniambia Mbowe, akasema sasa wanaona ni bora kufanya siasa kuliko mikutano ya hadhara. Mimi namwambia endelea,” amesema Dovutwa.

Dovutwa alimtaka Mbowe kuendelea kukimbia na chama hicho na kuwasikiliza wasiowatakia mema,” kwa mbio mlizopo nadhani mnakaribia Magogoni. Mbowe ana viwango vya kimataifa, kwa mwaka 2020 Chadema ndiyo kinategemewa.”

Mkurugenzi wa habari na mahusiano ya umma wa CUF, Abdul Kambaya amesema, “mwenyekiti alizungumzia maridhiano pale Mwanza watu wengine walimkosoa kwenye mitandao hawajui tulipotoka.”

Kambaya aliwataka wajumbe wa mkutano huo kutosikiliza maneno ya watu kwenye mitandao ya kijamii wakati wa kuchagua viongozi bali waangalie utendaji na katiba inasemaje.

“Watu wanadhani kiongozi anapatikana mitandaoni, wengine wanafikiri kiongozi anapatikana pale Buguruni. Si Buguruni, Lumumba au Ilala bali ni kutokana na katiba yenu na kwa mahitaji yaliyopo,” amesema Kambaya.

Katibu mkuu wa Chama cha Kijamii (CCK), Renatus Muabhi aliwataka wajumbe wa chama hicho kumchagua tena Mbowe kwa kuwa ndiye anayefaa.

“Kwa siasa za Serikali hii ya Awamu ya Tano mnamhitaji Mbowe, sio kwamba nampigia kampeni. Kuwa na kiongozi aliyeongoza miaka 10 sio hoja, hoja ni nani huyo kiongozi? Mbowe ndio mwenye dhamira ya dhati,” amesema Muabhi.

Mwingine aliyetoa salamu ni katibu mkuu wa NCCR-Mageuzi, Elizabeth Mhagama aliyewataka wajumbe kuchagua viongozi bora kwa ajili ya Taifa.