Vifaa vya Tehama vyakabidhiwa kwa wakuu wa shule ya sekondari Mtwara
Muktasari:
- Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani imekabidhi vifaa vya Teknolojia, Habari na Mawasiliano, (Tehama) kwa wakuu wa shule za Sekondari na Kituo cha Walimu Majengo.
Mtwara. Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani imekabidhi vifaa vya Teknolojia, Habari na Mawasiliano, (Tehama) kwa wakuu wa shule za Sekondari na Kituo cha Walimu Majengo.
Afisa elimu Msingi kutoka Manispaa hiyo, Flora Alloyce amevitaja vifaa hivyo kuwa ni Mashine ya photocopy na kompyuta 30.
Amesema Manispaa ilipokea vifaa hivyo kutoka Serikali Kuu kupitia Waziri wa ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mtaa, (Tamisemi), Innocent Bashungwa April 25, 2022 jijini Dar es Salaam.
"Serikali imetoa vifaa hivi ili kurahisisha ujifunzaji na ufundishaji kwa kutumia teknokojia ya Tehama pamoja na kusaidia katika mafunzo endelevu kwa walimu kazini (MEWAKA) ikiwemo mada ngumu na maandalizi ya miitihani" amesema Afisa elimu Msingi wakati akikabidhi vifaa hivyo leo Alhamisi Aprili 28, 2022.
Amesema matumizi ya vifaa hivyo yamegawanyika katika sehemu mbili ikiwemo photocopy mashine ambayo itawekwa katika kituo cha walimu kilichopo shule ya Msingi Majengo lengo kusaidia shughuli za kitaaluma ndani ya Manispaa.
Kwa upande wa kompyuta, Flora amesema zinapelekwa katika shule zenye maabara ya Tehama ambazo ni shule ya sekondari ya Mtwara, Ufundi Shangani (10) pamoja na Shule ya Sekondari ya wasichana Mtwara (10).
Baada ya kupokea kompyuta hizo, Mratibu wa kituo cha Majengo, Paul Kaji ameishukuru Serikali kwa kuwezesha vifaa hivyo kwani vitasaidia kuongeza ufanisi katika shughuli za kitaaluma kwa shule za Msingi na Sekondari.