Vifo vya wafanyabiashara vyatikisa

Muktasari:

  • Tanzania imepoteza wafanyabiashara kadhaa katika siku za hivi karibuni ambao wamejizolea maarufu katika sekta mbalimbali.

Dar es Salaam. Tanzania imepoteza wafanyabiashara kadhaa katika siku za hivi karibuni ambao wamejizolea maarufu katika sekta mbalimbali.

Kifo cha Mwenyekiti wa Kampuni za Asas Group, Alhaj Faraj Ahmed Abri kilichotokea jana Ijumaa Agosti 13, 2021  jijini Dar es Salaam kimeongeza pigo kwa jumuiya ya wafanyabiashara Tanzania baada ya kufikisha idadi ya watu maarufu sita waliofariki dunia katika kipindi cha wiki mbili zilizopita.

Taarifa kutoka katika familia hiyo, Mzee Abri ambaye ni baba mzazi wa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Salim Abri Asas, ziliwataka watu wasikusanyike mkoani Iringa bali watumie teknolojia za habari.

Maziko  yamefanyika jana baada ya swala ya adhuhuri katika makaburi ya Kisutu, jijini Dar es Salaam.

Wakati mzee Abri akizikwa, wengine waliofariki katika kipindi hicho ni pamoja na mfanyabiashara maarufu wa madini ya Tanzanite, Mathias Manga aliyewahi kuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), akiwa nchini Afrika Kusini.

Pamoja na umiliki wa mgodi wa Tanzanite wa Manga Gems uliopo kitalu D, marehemu Manga aliyefariki dunia juzi pia alikuwa anaendesha Hoteli za Gold Crest zilizopo jijini Arusha na Mwanza na alikuwa anamikiki majumba kadhaa ya kifahari jijini Arusha.

Mwingine ni mfanyabiashara maarufu Tanil Kumar Chandulal Somaiya aliyefariki dunia siku tatu zilizopita jijini Dar es Salaam na miongoni mwa biashara zake ni Mawasiliano kupitia Kampuni ya Shivacom na Ulinzi (Ultimate Security).

Wengine ni aliyekuwa mmiliki wa hoteli ya Peacock, Joseph Mfugale aliyefariki dunia Julai 31, mwaka huu jijini Dar es Salaam. Mfugale ni miongoni mwa wamiliki wa hoteli wazawa aliyepata mafanikio katika biashara hiyo, akifungua hoteli Dar es Salaam na nyingine mkoani Iringa.

Pia kuna mmoja wa wanafamilia wa mfanyabiashara maarufu wa mabasi ya Sumry, Hamoud Sumry aliyefariki dunia Agosti 9, mwaka huu jijini Dar es Salaam ikiwa ni siku chache baadaye kabla ya kifo cha John Lamba ambaye ni mfanyabiashara na mmiliki wa Hoteli ya Travertine jijini Dar es Salaam.