Vifo vya wanasiasa vilivyotikisa mwaka 2023

Muktasari:

  • Mwaka 2023, pamoja na mambo mengine, umekuwa wa majonzi na simanzi kwa Taifa baada ya wanasiasa mashuhuri kufariki dunia na kuacha kumbukumbu ya mambo waliyoyafanya katika historia ya siasa za Tanzania.

Mwaka 2023, pamoja na mambo mengine, umekuwa wa majonzi na simanzi kwa Taifa baada ya wanasiasa mashuhuri kufariki dunia na kuacha kumbukumbu ya mambo waliyoyafanya katika historia ya siasa za Tanzania.

Vifo vya wanasiasa hao si tu vimeacha simanzi kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki zao, bali kwa Taifa zima na vimeacha somo kwa wenzao na jamii kwa ujumla, kupitia uamuzi waliowahi kuufanya na aina ya maisha waliyoyaishi.

Watakumbukwa kwa mchango walioutoa kwa Taifa kupitia shughuli zao za kisiasa na kijamii na licha ya kushiriki kwenye shughuli za kisiasa, walikuwa pia na maisha mengine binafsi.

Miongoni mwa wanasiasa maarufu waliofariki mwaka huu ni pamoja na Bernard Membe, Nimrod Mkono, Francis Mtega (mbunge), Jecha Salum Jecha, Mohamed Raza, Zelothe Stephen na Sylvester Masinde.


Bernard Membe

Mei 12, 2023, Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, alifariki dunia akiwa kwenye matibabu ya homa na kifua kwenye Hospitali ya Kairuki Dar es Salaam.

Membe ambaye anatajwa kama shushushu mbobevu, mwanadiplomasia nguli na mwanasiasa makini, aliwahi kugombea nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, akipeperusha bendera ya ACT Wazalendo.

Kabla ya kujitosa na kisha kuenguliwa kwenye kinyang’anyiro cha urais mwaka 2015, Membe alikuwa mbunge wa Mtama kupitia CCM tangu mwaka 2000, alipoingia kwenye siasa na kuteuliwa kuwa Naibu Waziri na baadaye Waziri wa Mambo ya Nje.

Uamuzi mgumu aliowahi kuufanya Membe ni kwenda upinzani baada ya kuvuliwa uanachama Februari 28, 2020 baada ya Kamati Kuu CCM kufikia uamuzi huo baada ya kupitia ripoti ya kamati ya nidhamu ya chama iliyomhoji Membe.

Mchambuzi na mhadhiri wa siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Faraja Kristomus anasema Membe atakumbukwa kwa umahiri wake wa kusimamia kile alichoamini kuwa ni ukweli na hakuwa tayari kujipendekeza kwa sababu za kisiasa.

“Alipata umaarufu mkubwa alipokuwa Waziri wa Mambo ya Nje kwani aling'arisha sana nchi kimataifa wakati wa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete na aliongeza wigo wa diplomasia,” alisema Dk Kristomus.

Maoni ya msomi huyo hayaachani sana na ya Rainery Songea, mchambuzi mwingine wa siasa, anayesema Membe alikuwa kiongozi aliyesimamia alichokiamini na kuwa katika awamu iliyopita baadhi ya viongozi wengi walitetereka au kupata msukumo wa kisiasa lakini yeye alisimama imara.

“Membe alikuwa na ujuzi wa kiuongozi, mfano katika wizara alizosimamia na maendeleo yaliyopatikana, alijipambanua katika kusimamia mambo mbalimbali ili kuhakikisha maendeleo yanapatikana.

“Watu wanapaswa kujifunza suala la ujasiri wa kuhakikisha wanasimamia kile wanachokiamini. Kama unaamini ili kusonga mbele lazima tuwe na elimu, lazima usimame katika msimamo, lakini sio unaamini hivi, upepo ukija unabadilika. Kiongozi mzuri ni yule anayeweza kusimamia kile anachokiamini,” anasema Songea.


Nimrod Mkono

Aprili 18, aliyewahi kuwa mbunge wa Butiama mkoani Mara, Nimrod Mkono alifariki dunia akiwa nchini Marekani alikokuwa akitibiwa tangu mwaka 2018. Familia ilieleza kwamba Mkono alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu.

Mkono, aliyezaliwa Agosti 18, 1948 Busegwe mkoani Mara, alikuwa mwanasheria na mwanasiasa maarufu. Katika kipindi chake cha ubunge, alifanya mambo mengi ya maendeleo hususani kwenye sekta ya elimu.

Mkono amejenga shule za kisasa jimboni Butiama na hadi sasa wapo wanafunzi wanasoma na hata pale kilipo Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius Nyerere cha Kilimo na Teknolojia ni shule aliyoijenga yeye.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Anamringi Macha anasema Mkono alikuwa mwanasheria na mbunge mahiri aliyeongoza jimbo lake katika kuwaletea maendeleo wananchi, atakumbukwa kwa juhudi zote alizozifanya.

“Hakuna binadamu ambaye ni malaika, kila mtu ana upungufu wake na mema pia. Mara nyingi kikitokea kitu hatutazami jambo jema, bali tunaangalia mabaya tu. Tunachotakiwa kubaki nacho baada ya mtu au kiongozi kufariki ni yale mambo mema yake, kwa sababu ndiyo yatakatotusaidia,” anasema Macha.

KKuhusu Mkono, Dk Kristomus anasema atakumbukwa kama mbunge mkongwe aliyetumikia vipindi vingi Jimbo la Musoma Vijijini (sasa Butiama).

Anasema Mkono pia alikuwa ni mwanasheria aliyebobea na miongoni mwa wanasheria wachache wenye ukwasi na moyo wa kujitolea kwa ajili ya watu wake.


Mohamed Raza

Juni 8, 2023, mfanyabiashara maarufu wa Zanzibar na mwanasiasa aliyewahi kuwa mwakilishi wa Jimbo la Uzini, Mkoa wa Kusini Unguja, Mohamed Raza alifariki dunia katika Hospital ya Aga Khan, jijini Dar es Salaam alikokuwa anapatiwa matibabu.

CCM Zanzibar ilimwelezea Raza kama kiongozi aliyelinda na kukipigania chama hicho na alikuwa kada mwadilifu, mchapakazi na mzalendo mwenye maono ya kimaendeleo ndani ya chama na Serikalini.

Raza alizaliwa Julai 8, 1962 katika Mtaa wa Mkunazini, Unguja, hadi anafariki alikuwa kada wa CCM. Aliwahi kuhudumu katika nafasi mbalimbali ndani ya CCM akiwa mwakilishi wa Uzini na serikalini aliwahi kuwa mshauri wa Rais wa Zanzibar wa awamu ya tano, Salmin Amour katika masuala ya michezo.

Akimzungumzia, Macha anasema “Raza alikuwa mfanyabiashara na kiongozi wa siasa, alitumikia vema nafasi yake ya siasa na shughuli za kibiashara na wananchi walipata huduma mbalimbali kutoka kwake.

Pia kupitia yeye Serikali ilipata kodi zilizowezesha kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

Kwa upande wake, Dk Kristomus anasema Raza alikuwa ni mwanasiasa mkongwe wa Zanzibar, alijipatia heshima kubwa kama mfanyabiashara na mwanasiasa aliyekuwa na uchungu na Zanzibar.

“Alisifika sana kwa kutoweka mambo moyoni. Alikuwa na ujasiri wa kuzungumzia lolote aliloona haliendi sawa na lina masilahi kwa Zanzibar,” anasema.

Katibu wa Habari, Uenezi na Mawasiliano na Umma wa ACT Wazalendo, Salim Bimani alisema baadhi ya wanasiasa waliopoteza maisha mwaka huu watakumbwa kwa misimamo yao na namna walivyokuwa wakijitoa katika kuhudumia wananchi wakiwa wabunge au wawakilishi.

“Tutamkumbuka Raza kwa uzalendo wake hasa Zanzibar, pia alikuwa muwazi, akiona jambo halipo sawa hapindishi maneno, alisema haliko sawa, sio kutazama chama chake kwanza,” anasema Bimani.


Francis Mtega

Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Mbarali (CCM), Francis Mtega alifariki Julai mosi, mwaka huu, kwa ajali ya kugongwa na trekta (Power Tiller) shambani kwake, wakati akiendesha pikipiki yake.

Kifo cha mbunge huyo kimelitikisa Bunge mwaka huu, akiwa ndiye mbunge pekee aliyefariki. Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson alimtaarifu mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuhusu kuwepo wa nafasi wazi katika Jimbo la Mbarali.

Atakumbukwa kwa kuanzisha miradi ya maendeleo jimboni kwake licha ya kuwa amekuwa mbunge ndani ya kipindi kifupi cha miaka mitatu, tangu alipochaguliwa mwaka 2020.

Mbunge aliyechaguliwa kujaza nafasi ya Mtega katika Jimbo la Mbarali, Bahati Ndingo anasema mtangulizi wake atakumbukwa kwa namna alivyokuwa muungwana, mpole na mfuatiliaji wa shughuli mbalimbali katika kuhakikisha wananchi wake wanapata maendeleo.

“Nitahakikisha ninayaendeleza yale aliyoyatamani mzee wetu (Mtega) kuhakikisha Mbarali inafanikiwa au kupiga hatua za maendeleo. Alikuwa na mipango mingi ya kurahisisha huduma kwa wananchi ikiwemo miundombonu ya maji, umeme na barabara, yote haya nitaendeleza kuyafanyia kazi.

“Alikuwa mtetezi wa kweli kwa wananchi wa Mbarali, hata pale ambapo alionekana mbaya hakusita kuongea ukweli, nitayaenzi yote kwa ushirikiano na wenzangu,” anasema Ndingo.


Jecha Salum Jecha

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salum Jecha alifariki Julai 18, 2023 katika Hospitali ya Rufaa ya Jeshi Lugalo, jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu.

Jecha alipata umaarufu baada ya kufuta uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 Zanzibar, jambo ambalo si tu liliwashangaza wengi, bali pia ilikuwa ni mara ya kwanza kwa matokeo ya urais kufutwa visiwani humo.

Baada ya kufuta matokeo hayo, ZEC ilitangaza uchaguzi wa marudio ambao CUF, chama kikuu cha upinzani Zanzibar wakati huo, iliususia na mgombea wake, Maalim Seif Sharif Hamad kudai kuwa ameibiwa ushindi wake.

Mchambuzi wa siasa, Ali Makame anasema licha ya kupitia changamoto mbalimbali, Jecha alifanikiwa kusimamia sheria katika utekelezaji wa majukumu yake kama mwenyekiti wa ZEC.

“Unapokuwa kiongozi katika majukumu ya kiserikali au kijamii, jaribu kufuata sheria, usiongozwe na jazba. Nitamkumbuka Jecha kwa namna alivyofanya kazi kwa mujibu wa sheria, hii inatufanya jifunze kuwa sheria ni jambo muhimu sana hata kama unataka kutetea haki, basi jitetea kwa mujibu wa sheria,” anasema Makame.


Sylvester Masinde

Machi mosi mwaka huu, mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamizi ya Chadema, Sylvester Masinde alifariki dunia katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza alikokuwa anapatiwa matibabu.

Masinde alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa bodi hiyo ya wadhamini, Novemba 19, 2021 akichukua nafasi ya Arcado Ntagazwa ambaye pia alifariki.

Masinde ni miongoni mwa waasisi wa Chadema waliko hai ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani ambacho sasa kimekuwa kinatoa ushindani kwa chama tawala nyakati za uchaguzi.


Zelothe Stephen

Oktoba 27, mwaka huu, aliyekuwa mwenyekiti wa CCM mkoa wa Arusha, Zelothe Stephen alifariki katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) alikokuwa akipatiwa matibabu.

Zelothe aliwahi kukitumikia chama na Serikali katika nafasi mbalimbali ikiwemo kamanda wa polisi mkoa wa Dodoma na mkuu wa mkoa wa Rukwa.

Kwa mara ya kwanza Zelothe, alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa CCM mkoa wa Arusha Desemba 2019, akichukua nafasi ya Loota Sanare ambaye aliteuliwa na Rais wa wakati huko, kuwa mkuu wa Mkoa wa Morogoro.

Hata hivyo, Novemba 2022, Zelothe alifanikiwa kuitetea nafasi yake na hivyo kuendelea kuongoza chama hicho mkoani Arusha hadi mauti ilipomkuta.