Vijana 1,000 kupewa elimu ya afya, ujasiriamali

Muktasari:

  • Zaidi ya vijana 1,000 watanufaika na mafunzo ya elimu ya afya, ujasiriamali, uzalendo na masuala ya kiroho mkoani Pwani.

Kibaha. Shirikisho la Umoja wa Makanisa yaliyo chini ya mwavuli wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) na na Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC) mkoani Pwani, wanatarajia kufanya kongamano litakalohusisha zaidi ya vijana 1,000 kwa ajili ya kuwapa elimu ya afya, ujasilimali, uzalendo na masuala ya kiroho.

Kongamano hilo linatarajiwa kufanyika mapema mwakani likihusisha wakufunzi wa taaluma mbalimbali.

Hayo yamebainishwa jana Jumanne Desemba 26, 2023 na Mwenyekiti wa CCT, Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili ya Kilutheri Tanzania (KKKT) usharika wa Tumbi wakati wa ibada ya pamoja iliyofanyika Kanisa la AICT Kibaha mkoani humo.

"Tunataka vijana wa Kibaha wote wafanye kazi za uzalishaji,wawe wazalendo,  watunze afya zao na tunaamini kuwa wakifanya kazi watachangia uchumi wao binafsi na wa Taifa kwa ujumla," amesema.

Amesema lengo ni kuwafikia vijana wote wakiwamo wenye imani za dini mbalimbali, wasiokuwa nayo na  watashirikiana na viongozi wa ngazi za mitaa ili kuwapata na kuwapa elimu hiyo bila  kuchangia gharama yoyote.

“Katika kufanikisha matendo ya huruma mwishoni mwa wiki kabla ya maadhimisho ya Krismasi umoja umoja wetu ulikusanya michango na  kufikisha zaidi ya Sh800,000, ambazo tulinunua mahitaji muhimu vikiwamo vyakula tulivyovisambaza kwa watu wenye mahitaji maalumu  kwenye maeneo mbalimbali,”alisema.

Mgeni rasmi kwenye ibada hiyo ambayo hufanyika Jumatatu ya Pasaka na siku moja baada ya Krismasi, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kibaha, Moses Magogwa amesema kuwa ofisi yake iko tayari kutoa ushirikiano wowote pindi unapohitajika ili kudumisha umoja huo.

Amewataka viongozi wa makanisa hayo na hata wale wenye nia ya kuanzisha mapya kuzingatia sheria za nchi, kwani Serikali haiko tayari kuvumilia wanaozikiuka.

“Ninachopenda kusema kwa wale wanaotaka kuanzisha makanisa wafuate kanuni na wawe wakweli. Unakuta mtu anataka kusajili kanisa lakini ndani yake kuna viashiria vya tabia zisizofaa kwenye jamii au  kichochoro cha kutakatisha pesa, hilo halikubaliki," amesema.

Kwa upande wake Mchungaji mstaafu wa kanisa Anglikana, Daimon Mwegoha amesema umoja huo tangu uanzishwe ni zaidi ya miaka 50 sasa,  na wanajivunia kuwa pamoja na kudumisha upendo na ushirikiano.

Naye, Mchungaji wa KKKT Mlandizi, Fidea Chimtembo amesema kuwa wakati familia zinasherehekea sikukuu za mwisho wa mwaka, kuna umuhimu wa kila mmoja kujitathmini juu ya wajibu wake.

Akizungumza mara baada ya ibada hiyo,  Katibu Msaidizi wa umoja huo, Mchungaji wa Kanisa Anglikana la Mtakatifu  Gabriel Kibaha, Exavia Mpambichile amesema ili kufanikiwa katika mipango mbalimbali kuna ulazima wa wanajamii kujifunza kunyenyekea na kutumia busara.