Vijana 200 kuanza ufugaji nyuki Shinyanga

Muktasari:
Vijana zaidi ya 200 kutoka vijiji vya Mwamanyuda, Chona, Nyika na Imesela Kata ya Imesela Halmashauri ya Shinyanga wanatarajia kuanza utekelezaji wa mradi wa ufugaji nyuki ambao pamoja na kuwanufaisha kiuchumi, utawaepusha kukaa vijiweni na kujiunga na makundi maovu.
Shinyanga. Vijana zaidi ya 200 kutoka vijiji vya Mwamanyuda, Chona, Nyika na Imesela Kata ya Imesela Halmashauri ya Shinyanga wanatarajia kuanza utekelezaji wa mradi wa ufugaji nyuki ambao pamoja na kuwanufaisha kiuchumi, utawaepusha kukaa vijiweni na kujiunga na makundi maovu.
Wakizungumza kwenye bonanza la michezo ambalo limefanyika Kata ya Imesela ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa vijana kutumia fursa zilizopo kujiongezea kipato wamesema mradi huo utaongeza kipato kwa vijana ambao wengi wao wamejikita kwenye kilimo pekee.
“Kutokana na vijana wengi kutegemea kilimo pekee ambapo kupitia ufugaji huu wa nyuki utatuongezea kipato zaidi kwani tutauza asali na uchumi wetu utakuwa tofauti na awali,”amesema Elizaberth Mkende mkazi wa Kijiji cha Chona
Amesema kutokana na juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali kuweka miundombinu mizuri wanashukuru wameanza kupata fursa pamoja na jitihada za viongozi wao akiwemo Diwani na Mbunge kuhamasisha maendeleo.
Diwani wa Kata ya Imesela, Seth Msangwa amewataka vijana kufanya kazi kama timu ili kufikia lengo la kukuza uchumi wao.
“Tutaanza na mizinga ambayo ni ya kawaida tutatumia miti yetu ambayo ni ya asili baada ya hapo tutaangalia namna ya kuwezeshwa na wadau wengine katika kutushika mkono"amesema Msangwa
Amesema kupitia mradi wa ufugaji nyuki wapo vijana ambao wamefanikiwa kupitia fursa hiyo ambayo wakiitumia vizuri watapiga hatua kubwa.
Naye mdau wa Maendeleo Kata ya Imesela, Richard Nyanda amesema Shughuli za ufugaji nyuki zinahitaji nguvu zaidi kutoka kwa vijana ili kufikia lengo walilokusudia licha ya kuhitaji msaada kutoka kwa wadau wengine ili kutimiza lengo lao.