Vijiji 141 mbioni kupata huduma ya maji Mtwara

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanal Ahmed Abbas akiangalia moja ya mashine za kuchimbia visima zilizofika mkoani Mtwara kwaajili ya kuchimbia visima. Picha na Florence Sanawa

Muktasari:

  • Mkoa wa Mtwara una upungufu wa maji wa zaidi ya asilimia 33 ambapo mahitaji ya maji Mkoa wa Mtwara yanatajwa kufikia  zaidi ya milimita milioni 40 ambapo uzalishaji ni zaidi ya lita milioni 27.

Mtwara. Mkoa wa Mtwara unatajwa kuwa na upungufu wa uzalishaji wa maji kwa zaidi ya asilimia 33 ambapo kwa sasa uzalishaji ni zaidi ya lita milioni 40.

Akizungumza katika Maadhimisho ya Wiki ya Maji, Meneja wa Wakala wa Usambazaji wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini  (Ruwasa) Mkoa wa Mtwara, Primmy  Mshihiri amesema kuwa ili kuongeza upatikanaji wa maji wanatarajia kujenga zaidi ya miradi 34 ambapo vijiji 144 vinatarajia kupata huduma ya maji.

Amesema kuwa pia ipo miradi mipya 32 ambayo ikikamilika zaidi ya vijiji 141 vitapata huduma ya maji ikiwemo kuboresha Mradi wa Maji Makonde na miradi mingine katika Wilaya za Newala, Tandahimba na Nanyamba.

Miradi yote ikikamilika tutakuwa tumefikia asilimia 85 vijijini 95 tunaamini kuwa miradi ikikamilika tutavuka hata lengo la upatikanaji wa maji liliwekwa kwenye ilani ya chama cha mapinduzi," amesema.

"Katika upatikanaji wa vyanzo ni shida katika Wilaya ya Nanyumbu mikakati inaendelea jambo la muhimu ni wananchi kutunza vyanzo ili viweze kutusaidia baadaye maji yanaleta vita tunzeni vyanzo vya maji," amesema.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanal Ahmed Abbas amesema kuwa kumekuwa na sintofahamu ya watu kuhurusu maeneo yao kupita miundombinu ya maji hivyo kusasababisha ucheleweshaji wa usambazji wa huduma hiyo.

Akipokea na kuzindua mitambo ya uchimbaji maji  mkoani mtwara ambayo imeletwa mkoani humo kwa ajili ya kukabiliana na changamoto ya maji alisema uchimbaji wa visima ni sehemu ya wizara ya maji kusaidia kupunguza changamoto za maji mkoani humo.

“Nafikiri ni vyema muwe tayari kuruhusu maeneo yenu kupitisha miundombinu ya maji ili iweze kuwafikia kwa urahisi zaidi wananchi wengi zaidi na pia achaneni na dhana ya kupata huduma ya maji bure changieni kiasi kilichopangwa ili kuruhusu ukarabati wa miundombinu ya maji pale inapotokea uharibifu,” amesema.

“Zingatieni utunzaji wa vyanzo vya maji hakikisheni mnazingatia na kuheshimu mipaka ya vyanzo vya maji ili yaweze kutumiwa na sisi na kizazi kijacho,” amesema.

“Nimesikia upatikanaji wa maji ni mkoa asilimia 67 na ilikifiia asilimia 85 kwa vijijini tekelezeni kwa weledi ili kuhakikishau kuongeza kasi ya mabadiliko katika sekta ya maji kwa maendeleo endelevu ya kiuchumi," amesema.

"Mahitaji ya maji Mkoa wa Mtwara yanatajwa kufikia   zaidi ya milimita milioni 40 ambapo uzalishaji ni zaidi ya lita milioni 27 sawa na upungufu wa asilimia 33 ya maji yanayotakiwa kupatikana katika mkoa huu," amesema Kanal Abbas.