Vikwazo kwa Zimbabwe vyazua mengine mapya

Muktasari:

Waziri wa usalama Zimbabwe azuiwa kuingia Marekani akidaiwa kuhusika katika ukiukaji wa haki za binadamu na utekaji wa raia.

 

Washington. Marekani imewekea vikwazo Waziri wa Usalama wa Zimbabwe, Owen Ncube kwa ilichoeleza kuwa ina ushahidi wa kutosha kwa kukiuka haki za binadamu.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imesema itamzuia Ncube kuingia nchini Marekani.

“Tumesikitishwa sana na Serikali ya Zimbabwe kwa kutumia vurugu kuzuia maandamano ya amani na asasi za kiraia, viongozi wa vyama vya wafanyakazi na viongozi wa upinzani, alisema Mike Pompeo, waziri wa Mambo ya nje wa Marekani.

“Tunaitaka serikali iachane na vurugu, ichunguze na kuwajibisha maofisa wanaohusika na ukiukaji wa haki za binadamu nchini Zimbabwe,” alisema.

Zimbabwe imeshuhudia maandamano ya kuipinga serikali mwaka huu, mengi yakihusu kushindwa kwake katika uchumi na kusababisha takriban watu milioni tano kuishi kwa kutegemea misaada.

Kumekuwa na taarifa za kuwapo mateso na utekaji katika harakati za serikali kutaka kutuliza maandamano hayo.

Hata ripoti ya mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa anayehusika haki za kukusanyika na kujumuika iliyotolewa Septemba mwaka huu, inazungumzia hatua ya Zimbabwe kutumia nguvu kubwa.

Mwezi uliopita, madaktari waliandamana baada ya kiongozi wa chama chao cha wafanyakazi, Peter Magombeyi na mwandaaji mwingine katika hatua za kudai maslahi zaidi walitoweka.

Ncube alisema wakati huo kuwa tukio la Magombeyi lilikuwa linachukuliwa kama “kutoweka” na siyo “kutekwa” kama ilivyokuwa inadaiwa.

Vikundi vya kutetea hakai za binadamu vinaeleza kukusanya matukio zaidi ya 20 ya wanaharakati kutekwa na vyombo vya usalama tangu Januari. Serikali ikana kuhusika na matukio hayo.

Hatua za Marekani dhidi ya Ncube imekuja wakati maelfu ya Wazimbabwe wanaandamana jijini Harare kuitikia wito wa Rais Emmerson Mnangagwa kuitaka Marekani na Umoja wa Ulaya kumwondolea vikwazo vilivyowekwa dhidi yake na watendaji wengine kutokana wizi wa kura na ukiukaji wa haki za binadamu.

Mnangagwa analaumu vikwazo hivyo vilivyowekwa tangu 2001 kuwa vinalenga kukiondoa chama chake madarakani.

Miaka miwili tangu kuondolewa madarakani  Robert Mugabe, mfumuko wa bei bado uko katika tarakimu tatu na upungufu wa bidhaa muhimu kama mafuta.