Vikwazo vya biashara EAC vyawaliza wafanyabiashara
Muktasari:
Akizungumzia hali hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye alisema miongoni mwa vikwazo vinavyokera wafanyabiashara ni pamoja na tozo zisizokuwa za kikodi katika mipaka ya nchi hizo wakati wa kupitisha mizigo.
Arusha. Nchi za Afrika Mashariki, zimetakiwa kuondoa vikwazo vya kibiashara baina ya nchi wanachama ili biashara ziweze kufanyika vizuri na hivyo kuinua uchumi wa nchi hizo.
Mwenyekiti wa Baraza la Biashara la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EABC), Nicholas Nesbitt alitoa kauli hiyo juzi usiku katika mkutano wa 20 wa wakuu wa nchi za Afrika Mashariki (EAC) uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).
Nesbitt alisema kwa sasa ni rahisi bidhaa kuingizwa kutoka nje ya Afrika ya Mashariki kuliko bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi wanachama.
“Kama tunataka kukuza biashara kwa nchi za Afrika Mashariki, tuondoe vikwazo vilivyopo mipakani baina ya nchi na nchi,” alisema Nesbitt.
Alisema ili kufikia shabaha ya kujenga uchumi wa viwanda wa nchi hizo, kuna haja ya kupunguza au kumaliza utegemezi wa bidhaa kutoka nje kama nguo za mitumba na badala yake vijengwe viwanda vya ndani vitakavyotengeneza nguo.
Nesbitt alisema nchi za EAC zinaweza kushirikiana katika kuanzisha viwanda na kuuziana malighafi kuliko kutegemea malighafi kutoka nje ya nchi hizo.
Akizungumzia hali hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye alisema miongoni mwa vikwazo vinavyokera wafanyabiashara ni pamoja na tozo zisizokuwa za kikodi katika mipaka ya nchi hizo wakati wa kupitisha mizigo.
Simbeye alisema kero ya tozo hizo inahitaji kufikia tamati. “Lakini pia, kumekuwa na tabia ya wafanyabiashara wa nchi hizi kushawishi serikali zao ili kuongeza kodi kwenye bidhaa zinazotoka ndani ili wapate soko la ndani, hili limekuwapo kwa muda mrefu ila kwa Tanzania sijaliona,” alisema Simbeye aliyeshiriki mkutano huo.
Mwenyekiti mstaafu wa Umoja wa Maofisa Watendaji Wakuu wa Kampuni Binafsi nchini (CEOrt), Ali Mufuruki alisema tatizo kubwa linalohitaji ufumbuzi katika Jumuiya hiyo ni kila nchi husika kuondoa dhana ya ushindani na kuwa timu moja itakayokuwa na uwezo wa kuhimili ushindani na China inayopaa kila kukicha kiuchumi.
“Nakubaliana naye (Nesbitt) kwa sababu tunayo nafasi ya kuteka soko la uwekezaji wa EAC, mfano Kenya ikianzisha kiwanda cha magari siyo tena nchi nyingine ijenge, itauza soko la EAC, lakini haitawezekana kama nchi nyingine hazitatoa ushirikiano,” alisema.
Mufuruki aliguswa na ujumbe wa mwenyekiti huyo aliyependekeza kila nchi iweke mezani ni changamoto gani zinazotakiwa kuondolewa ili iweze kuruhusu raia wa nyingine kuingia na kufanyabiashara.
Alisema nchi hizo zinatakiwa kujiona kama watu wa timu moja inayotakiwa kuimarisha uchumi wa nchi zao kupitia fursa za masoko ya jumuiya, vinginevyo itapotea endapo itaendeleza ushindani wa masoko ya ndani.