Viongozi DCPC watumbuliwa, wachaguliwa wapya

Mwenyekiti wa Umoja wa Vyama vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Deo Nsokolo akizungumza na waandishi wa habari mkoa wa Dar es Salaam

Muktasari:

Viongozi watano na wajumbe wa kamati ya utendaji wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam (DCPC) wamevuliwa nyadhifa zao kwa kushindwa kutimiza wajibu wao.

Dar es Salaam. Viongozi watano na wajumbe wa kamati ya utendaji wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam (DCPC) wamevuliwa nyadhifa zao kwa kushindwa kutimiza wajibu wao.

Viongozi hao wamevuliwa nyadhifa zao katika Mkutano Mkuu Maalumu wa Wanachama wa DCPC, uliofanyika leo Jumatatu 9 Mei 2022, jijini Dar es Salaam.

Kamati tendaji iliyovuliwa madaraka ni Irene Mark ambaye alikuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Chalila Kibuda aliyekuwa Makamu Mwenyekiti, Hussein Syovelwa ambaye alikuwa Katibu Mkuu, Fatuma Jalala aliyekuwa Katibu Msaidizi pamoja na Patricia Kimelemeta aliyekuwa Mweka hazina.

Wajumbe waliovuliwa madaraka ni Tausi Mbowe,  Shabani Matutu, Cecilia Jeremiah, Selemani Msuya, Kamugisha Mchunguzi na Christina Galaluhanga.

Hata hivyo mkutano huo uliokuwa na wajumbe zaidi ya 50 ulifanya uchaguzi na kuwachagua viongozi wapya ambapo kwa nafasi ya Mwenyekiti wa DCPC amechaguliwa Samson Kamalamo, Makamu Mwenyekiti Salome Gregory, Katibu Mkuu Fatuma Jalala, Katibu Mkuu Msaidizi Chalila Kibuda na mweka hazina Kimelemeta. 

Wajumbe wapya waliochaguliwa ni Ibrahim Yamola, Salehe Mohamed, Tausi Mbowe, Janet Josiah, Shabani Matutu na Njumai Ng'ota.

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi huo, Rais Umoja wa Vyama vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Deo Nsokolo amesema umoja huo upo tayari kufanya kazi na uongozi uliyochaguliwa ndio maana wamefika katika mkutano huo kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa.

"Nina imani na Kamalamo kwamba atafanyakazi kwa kufuata katiba na sheria, ila nataka atambue kwamba DCPC hakuna chochote yaani hakuna mshahara au posho bali kuna ruzuku kwaajili ya wanachama wote," amesema na kuongeza 

"Viongozi pia wanapaswa kufahamu kuwa mtu wa kwanza kuwasiliana na UTPC ni Mwemyekiti, unapopokea barua unaisoma na kuzifanyia kazi na si unaipeleka nyumbani kwako. DCPC kama mwemyekiti wenu atasimama mjue mtapata haki zote ikiwamo fedha za kutosha na tunataka Dar iwe kiongozi kwa Tanzania," amesema

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu Katibu aliyevuliwa madaraka, Syovelwa amesema hatambui mkutano wowote uliyofanyika leo hivyo amewataka wanachama kutulia wakati wanajiandaa kutoa tamko lao.

"Suala la kuvuliwa uongozi wewe ndo unaniambia mimi sitambui chochote na kama kuna mkutano umefanyika wamefanya kwa kujifurahisha tu, mkutano hauwezi kuitishwa kwa notes ya siku mbili, nasisitiza kuwa DCPC haikuwa na mkutano leo," amesema