Viongozi kidini, mila watwishwa jukumu vita dhidi ya ukatili

Mkuu wa mkoa wa Mara, Suleiman Mzee. Picha na Beldina Nyakeke

Muktasari:

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Suleiman Mzee ameiomba jamii wakiwemo viongozi wa dini, mila na wazee maarufu mkoani mara kushirikiana na Serikali na wadau wengine kupiga vita vitendo vya ukatili na unyanyasaji kijinsia mkoani humo.

Musoma. Viongozi wa kidini, kimila na watu maarufu mkoani Mara wametakiwa kushiriki vita dhidi ya vitendo ukatili, unyanyasaji wa kijinsia na mmomonyoko wa maadili nchini.

Akizungumza wakati wa Kikao cha Kamati ya Ushauri (RCC) Mkoa wa Mara, Mkuu wa mkoa huo, Suleiman Mzee ametaja ndoa za jinsia moja, ndoa za utotoni na ukeketaji kwa watoto wa kike kuwa miongoni mwa mambo ambayo viongozi wa dini, kimila na wazee maarufu mkoani Mara wanapaswa kushiriki kutapiga vita kwenye jamii.

“Hivi sasa kuna shinikizo duniani kuhusu ndoa za jinsia moja; haya ni miongoni mwa mambo ambayo viongozi wa kidini, kimila na wazee mashuhuri wanatakiwa kushirikiana na wadau wengine kuyapiga vita maani yanakwenda kinyume maadili, mila, desturi na tamaduni za Kiafrika,” amesema Mzee

Akizungumzia elimu, Mkuu huyo wa mkoa amewaagiza viongozi na watendaji wote wa Serikali mkoani humo kufuatilia waliko wanafunzi 6, 500 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mkoani humo ambao hawajaripoti shuleni hadi sasa.

"Kila kiongozi katika eneo lake afuatilia na kufahamu waliko wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza ambao hawajaripoti shuleni,” ameagiza RC Mzee

Katibu Tawala Mkoa wa Mara, Msalika Makungu amesema licha ya Serikali kutumia mabilioni ya fedha kuboresha miundombinu na mazingira ya kujifunzia na kufundishia mkoani humo, tatizo la utoro bado ni kikwazo cha maendeleo ya sekta ya elimu mkoani Mara.