Viongozi mashuhuri duniani wammwagia sifa Dk Salim
Muktasari:
- Viongozi mashuhuri waliowahi kuongoza mashirika ya kimataifa na mamlaka za nchi wametaja Dk Salim Ahmed Salim katika sura tano zitakazosaidia kuwa alama, mafunzo kwa kizazi kijacho.
Dar es Salam. Viongozi mashuhuri waliowahi kuongoza mashirika ya kimataifa na mamlaka za nchi wametaja Dk Salim Ahmed Salim katika sura tano zitakazosaidia kuwa alama, mafunzo kwa kizazi kijacho.
Wamesema Dk Salim anayezindua tovuti ya hifadhi ya nyaraka zake leo Septemba 30, mwaka huu ni Mtanzania mwaminifu aliyejali utaifa, mwanamajumui wa Afrika, mwanadiplomasia wa Dunia, mtunza amani na kiongozi mzalendo aliyekuza mahusiano ya Tanzania na Dunia.
Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk Tedros Ghebreyesus amesema tovuti hiyo itaelezea mafanikio yake pekee bali itaitangaza pia Tanzania kuhusu mchango wake Afrika.
Rais wa zamani wa Ireland, Dk Mary Robinson amesema Dk Salim alikuwa ni rafiki wa kipekee katka taifa hilo na alifanikiwa kushughulikia migogoro mingi ya Afrika kwa njia ya majadiliano.
Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian amesema katika kipindi cha uongozi wake akiwa Katibu Mkuu wa Nane wa Jumuiya ya Muungano wa Nchi za Afrika (OAU), mwaka 1989 – 2000 alifanikiwa kuonyesha uwezo mkubwa wa diplomasia Afrika na urafiki mwezi na China.
“Ni Mtanzania wa kweli kweli, katika jambo lolote lililokuwa na mtazamo wa Zanzibar na Tanzania bara, alilizungumzia kwa mtazamo wa kitaifa, huyo ndio Salim,” amesema Waziri mkuu Mstaafu Jaji Joseph Warioba.
Balozi Khamis Kagasheki aliyewahi kufanya kazi pamoja na Dk Salim amesema umahiri wake ulionekana baada ya kuwaunganisha makundi mawili ya yaliyotofautiana Afrika chini ya utawala wa kikoloni wa mwingereza na mfaransa.
“Alionyesha uwezo mkubwa wa kuwaleta pamoja waafrika , waliokuwa Anglophone(utawala wa kiingereza) na Francophone(utawala wa kifaransa), kuwa wamoja, ilikuwa ni kazi kubwa mkubwa sana,”amesema Balozi Kagasheki.
Rais wa zamani wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf ameipongeza Tanzania kwa kuandaa tovuti hiyo ya mwanamajumui kuhusu mchango wake Afrika na Tanzania.
Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki amesema tovuti hiyo itakuwa kichocheo kikubwa cha mabadiliko ya vijana wa Afrika watakaojifunza na kufuata njia za uongozi wake.
Kuhusu tovuti
Rais Samia Suluhu Hassan amezindua rasmi tovuti hiyo iliyoandaliwa na familia ya Dk Salim kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na ndugu, jamaa na marafiki.
Tovuti hiyo inajumuisha video, picha na nyaraka mbalimbali kama vile hotuba, nakala za mawasiliano ya kimaandishi na machapisho ya kitafiti za Dk Salim.
Pili, inatoa ujuzi wa kipekee juu ya safari yake ya utumishi wa umma, na mchango wake katika mahusiano ya kimataifa na jitihada za ukombozi barani Afrika.
Tatu, inaangazia mchango wa nchi za Afrika katika siasa za kimataifa katika kipindi cha miaka ya 1960 hadi mwaka 2000.
Aidha, tovuti hiyo ambayo ni hifadhi ya matukio yaliyotengeneza maisha ya Dk Salim na muhimu zaidi hifadhi ya nukuu na nyaraka zake mwenyewe, inalenga kuimarisha historia ya Tanzania na ile ya Afrika.
Nyaraka za tovuti hii zitawavutia wale wanaotaka kuelewa mchango wa Tanzania na wa nchi nyingine barani Afrika katika historia ya dunia na siasa za kimataifa.