Viongozi simamieni sheria za mazingira-DC

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabiri Shekimweri.

Muktasari:

  • Maadhimisho ya wiki ya mazingira yameendelea kwa kufanyika kwa shughuli za usafi wa mazingira huku Makamu wa Rais, Philip Mpango akihitimisha wiki hiyo kesho katika Soko la kisasa la Machinga.

Dodoma. Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabiri Shekimweri amesema uchafuzi wa mazingira unaonekana mitaani unashirika hakuna usimamizi wa sheria za mazingira zilizotungwa.

Shekimweri ameyasema hayo Juni 4, 2023 wakati wa shughuli ya usafi katika eneo la Ilazo jijini Dodoma ikiwa ni maadhimisho ya wiki ya mazingira .

Katika shughuli hiyo, Shekimweri alikutana na uchafu wa mifuko ya plastiki, chupa za plastiki, maji machafu yakitiririka katika mifereji iliyopo pembezoni mwa barabara.

Amesema hali hiyo aliyokutana nayo wakati kuna kauli mbiu na sheria inaonyesha kuwa hazisimamiwi.

“Tunao viongozi ngazi zote, uzuri tuna wadau wa mazingira pia nini kimtokea hadi kuna hali kama hii. Tunahitaji tuimarishe usimamizi,”amesema.

Ametaka Watanzania suala la usafi kuwa ni tabia badala ya kuishia kufanya usafi katika maadhimisho kama hayo tu na kupiga picha.

Pia amesema kwake uchafu huo unaweza kutumika kama fursa kwa wasimamizi kutumia sheria ya mazingira ambazo faini yake ni Sh50,000 hadi Sh300,000.

Mkurugenzi wa Mazingira katika Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Dk Andrew Komba amesema licha ya kupinga mifuko la plastiki nchini lakini kumeanza kujitokeza kwa mifuko hiyo katika maeneo mbalimbali nchini.

Naye Mkurugenzi wa Huduma za Kinga katika Wizara ya Afya, Dk Tumaini Haonga amesema taka zikiachwa katika mazingira ni viashiria hatari vya kusababisha magonjwa ikiwemo saratani.