Mpango akerwa na vijana wanaochoma mkaa

Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Philip Mpango

What you need to know:

  • Makamu wa Rais Dk Philip Mpango amewataka Watanzania kutunza mazingira katika vyanzo vya maji nchini ili miradi ya maji inawekezwa na Serikali iweze kuwanufaisha.

Dodoma. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amesema vijana wanaochoma mkaa kwenye msitu wa Chinene uliopo katika Kijiji cha Chinene wilayani Bahi mkoani Dodoma wanatishia uhai wa chanzo cha maji kilichopo eneo hilo.

 Dk Mipango amesema hayo leo Jumatatu Juni 5, 2023 wakati akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya siku ya mazingira duniani yaliyofanyika kwenye soko la kisasa la Machinga jijini Dodoma.

“Msitu wa chinene siku hizi wale vijana wakata mkaa wanachengana na polisi au wanawahonga polisi kwasababu unakuta wanabana kabisa au wanaongozana na pikipiki zao hata 20 kila mtu anabeba magunia yake manne hadi matano ya mkaa,”amesema.

Amesema hayo yanafanyika wakati katika eneo la Zamahelo wako Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) na polisi na kuhoji kwanini hawazuu vitendo hivyo.

Amezitaka taasisi hizo kusimamia kero hiyo kwa manufaa ya wakazi wa Dodoma ambao wanategemea maji kutoka vyanzo vya maji vilivyopo katika misitu hiyo na endapo vikikauka hali itakuwa mbaya.

Aidha, Dk Mpango amewapongeza mkoa wa Dodoma kwa hatua walizochukua katika chanzo cha maji cha Mzakwe na kutopa rai kuendelea na juhudi zaidi.

“Hata leo nimepita (Mzakwe) hatujafanya juhudi za kutosha, tusipozingatia tutaiweka nchi yetu katika janga la ukosefu wa maji kwa hiyo,”amesema.

Amesema wakati Serikali inatekeleza wajibu wake wa kusambaza maji safi na salama ni wajibu wa Watanzania kuhakikisha kuwa wanaifadhi vyanzo vya maji na wasipofanya hivyo uwekezaji huo hauna maana yoyote.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema wamepanda miti 9,600 katika chanzo hicho ambapo asilimia 87 iko hai na inaendelea vizuri.

“Asilimia 13 iliyobaki iko hai haifi lakini haiendelei mbele lakini tunaendelea nayo kwahiyo ni hatua kubwa kukuhakikishia chanzo kile kinaendelea kutunzwa,”amesema.

Naye Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Dk Seleman Jafo amesema wiki hiyo ya mazingira imefanyika tofauti mwaka huu kwa viongozi kushiriki katika usafi wa mazingira badala ya kusherekea katika ukumbini.