Viongozi wa kijiji wakamatwa kwa tuhuma za mauaji

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Janeth Magomi
Muktasari:
- Jeshi la Polisi mkoani Songwe linawashikilia watu watano wakiwemo viongozi wa kijijini na kitongoji kwa tuhuma za mauaji ya watu wawili wa familia moja katika Kijiji cha Mpuwi wilayani Momba
Songwe. Jeshi la Polisi mkoani Songwe linawashikilia watu watano wakiwemo viongozi wa kijijini na kitongoji kwa tuhuma za mauaji ya watu wawili wa familia moja katika Kijiji cha Mpuwi wilayani Momba.
Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi Januari 27, 2022 Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Janeth Magomi amesema wanaoshikiliwa ni pamoja na viongozi wa kitongoji cha Ntekwe na Kijiji Cha Mpuwi.
Amesema Waliokamatwa wanatuhumiwa kuchangia, kushiriki au kuwaua watu wawili ambao ni Juma Sekesi Silwimbwa na mtoto wake, Yohana Juma Sekesi katika tukio lililotokea usiku wa kuamkia Januari 24, 2022.
Kamanda Magomi amesema uchunguzi wa awali unaoonyesha chanzo cha mauaji ni tuhuma za kishirikina zilizotokana na mke mkubwa wa marehemu Juma kuugua na hatimaye ndugu kumtuhumu marehemu na mke mdogo kwamba wanamloga.
Amesema tuhuma hizo zilichochewa na wapiga ramli pamoja na wachonganishi wa jamii wanaojiita lambalamba.
"Nasisitiza agizo la Mkuu wa Mkoa Omary Mgumba kupiga marufuku vitendo vya lambalamba mkoani hapa, Polisi wataendelea kuwasaka wahusika na pia itawakamata viongozi wa vijiji kila kukitokea mauaji yenye chanzo cha ushirikina'" amesema.
Mapema wiki hii, Mkuu wa Mkoa wa Songwe akizindua Wiki ya Mahakama mjini Tunduma alitoa taarifa za baba na mtoto kuuawa Momba na kuagiza wahusika wote wakamatwe.