Vipipi mahaba gumzo, madaktari waonya

Vipipi mahaba gumzo, madaktari waonya

Muktasari:

  • Wakati matangazo ya vipipi vya kuongeza uwezo na hamu ya kushiriki tendo la ndoa yakizidi kushamiri mitandaoni, madaktari wameonya matumizi ya bidhaa hizo na nyingine zinazodaiwa kuwasaidia wanawake.

Dar es Salaam. Wakati matangazo ya vipipi vya kuongeza uwezo na hamu ya kushiriki tendo la ndoa yakizidi kushamiri mitandaoni, madaktari wameonya matumizi ya bidhaa hizo na nyingine zinazodaiwa kuwasaidia wanawake.

Madaktari waliohojiwa na Mwananchi walionya kutokana na pipi hizo kutojulikana kutengenezwa na kitu gani ndani yake, wameonya matumizi hayo kwa wanawake.

Pia madaktari hao wametahadharisha wanawake hao juu ya matumizi ya dawa na bidhaa nyingine ambazo huziweka ukeni, wakieleza kuwa ni chanzo cha magonjwa, yakiwamo fangasi na saratani.

Siku za karibuni kumekuwapo na matangazo yanayonadi pipi hizo maarufu kama ‘pipi mahaba’ ambazo pia zinauzwa kwenye maeneo yenye mikusanyiko ya wanawake, zikiwamo saluni.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili hivi karibuni umebaini kuwa wanawake wanazichangamkia pipi hizo zinazodaiwa kusaidia kuongeza uwezo, hamu ya kushiriki tendo la ndoa na kumfurahisha mwanaume.

Gazeti hili lilizitafuta mamlaka za Serikali, ikiwamo Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Baraza la Tiba Asili na Tiba mbadala na taasisi hizi zote zimeeleza kutozifahamu pipi hizo wala zinavyotengenezwa.

Pipi hizo zenye rangi nyeupe mithili ya maji zimekuwa habari ya mjini kwa sasa, kuanzia mitandaoni hadi katika maeneo yenye mikusanyiko ya wanawake.

Kulingana na wauzaji, pipi hizo ni suluhisho la matatizo ya kimwili yanayoweza kumletea vikwazo mwanamke katika ushiriki wake kwenye tendo la ndoa.

Pipi hizo ambazo huuzwa kati ya Sh5,000 hadi Sh10,000 zinatumiwa kwa kuchanganywa kwenye maji ya moto yenye tangawizi kwa pipi nne au tano, kisha mtumiaji anakoroga kabla ya kunywa na kusubiri zifanye kazi baada ya saa mbili.

Hawa Mbega, anayezunguka kuuza pipi hizo mitaa ya Kariakoo anazinadi akieleza kuwa licha ya kumuongezea mwanamke hamu ya tendo, huongeza joto na kubana sehemu za siri. “Shoga angu shoo ya vipipi sio ya kitoto, yaani kama ndio umeamua siku hiyo unachemsha chai ya tangawizi, ukiweka kwenye kikombe unaviweka vinayeyuka unakunywa.

“Baada ya saa mbili vinajibu, shemeji lazima akuulize, shoo yake sio ya mchezo, unakuwa na nguvu, huchoki na kama uke umelegea, utakaza utakuwa vizuri tu, havina madhara vimetengenezwa na miwa vinatoka nje ya nchi,” alisema na kuongeza: “Pia, nina mazagazaga kibao ambayo ukiyatumia nakuhakikishia mwanaume hakuachi, hela yake utaipata na kama ana uwezo atakufanyia kila unachotaka hata ukihitaji gari atakupa,” alijigamba Hawa ambaye pia ni kungwi.

Mwananchi ilishuhudia wanawake wakichangamkia vipipi hivyo vilivyokuwa vikiuzwa kama njugu, huku wakionyesha nia ya kwenda kujaribu kuvitumia.

Mmoja wa watu ambao wameshatumia vipipi hivyo aliyefahamika kwa jina la Suzi alithibitisha uwezo wake: “Mimi nimewahi kuvitumia, nakushauri kama kweli unahitaji kuweka mambo yako vizuri chukua hizo pipi, shoo yake si mchezo.”

Kauli hiyo ya Suzi iliwafanya wanawake watatu waliokuwa katika eneo hilo kununua pipi hizo kwa ajili ya kwenda kuzitumia ili kupata matokeo waliyoelezwa.


Mamlaka zinasemaje?

Mwananchi lilizungumza pia na Mkuu wa kitengo cha uhusiano wa TBS, Rhoida Andusamile aliyeeleza: “Kiukweli sizifahamu hizo pipi na kama unasema mtu akila zina matokeo hayo hizo sasa ni dawa, jaribu kucheki na watu wa TMDA na pia nitafuatilia”.

Akizungumzia suala hilo, Meneja na Uhusiano na Mawasiliano kwa umma wa TMDA, Gaudensia Simwanza alikiri kuna changamoto ya udhibiti wa uuzaji wa dawa katika mitandao ya kijamii. “Nashindwa kuzizungumzia dawa hizo kwa kuwa sina uhakika kama zipo kwenye kundi la dawa tunazosimamia sisi, maana inaweza kuwa ni dawa zinazoangukia kwenye tiba asili, ila wito wetu dawa hazitakiwi kuuzwa wala kutumiwa kiholela, wananchi wawe makini,” alisema Simwanza.

Kwa upande wake, Mfamasia katika Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala, Ndahani Msigwa alisema, “Hizo pipi hatuzifahamu na inawezekana kuna vitu vingi vinatumika, lakini kwa kuwa havijaja ofisini na kuvithibitisha basi mtu atakuwa anatumia kwa uamuzi wake na maisha yake.”

Kando na vipipi hivyo, kuna bidhaa kadhaa ambazo zinatumiwa na wanawake zikihusisha viungo vyao vya uzazi, jambo ambalo linaweza kuleta athari kiafya.

Kuna dawa inaitwa gusa unase ambayo ni majani yaliyoviringwa kwenye umbo la duara dogo ambayo huwekwa ukeni na kuachwa kwa muda, kisha hutolewa ikidaiwa kuongeza ladha ya tendo kwa mwanaume. Pia yapo mafuta yanaitwa misk ambayo nayo huwekwa ukeni kwa kazi hiyo hiyo ya kuongeza ladha na mvuto.

Zipo pia dawa za unga ambayo matumizi yake inaelekezwa kuwekwa kwenye maji ya moto yaliyochemka (steamer) kisha mwanamke kuchuchumalia maji hayo ili mvuke umuingie kwa dakika tano hadi 10. Imedaiwa kuwa dawa hiyo inasaidia kuondoa harufu ukeni, kupunguza ukubwa wa uke, kuondoa ukavu pamoja na kukaza misuli ya uke.

Wapo pia ambao hutumia udi kufukiza sehemu za siri ili ziwe na harufu nzuri.


Kauli ya madaktari

Baadhi ya madaktari waliozungumza na gazeti hili wameeleza kuwa, mwanamke anaweza kujiweka kwenye hatari kwa kutumia vitu visivyofaa kwenye viungo vyake vya uzazi na kujisababishia magonjwa, ikiwamo saratani.

Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake, Ali Said alisema sehemu za siri za mwanamke zina bakteria walinzi hivyo, kutumia dawa na kemikali inaweza kuwaua bakteria hao na kuacha sehemu hizo zikiathiriwa kutokana na kukosa ulinzi wa kutosha.

“Uke ulivyoumbwa tayari una bakteria ambao kazi yao ni ulinzi, hivyo usafi wake unahitaji maji pekee, hakuna haja ya kuweka sabuni za kemikali, dawa wala mvuke wa maji ya moto ni hatari sana kiafya,” alisema.

Daktari huyo alieleza kuwa hakuna dawa ambayo imethibitishwa kuwa ina uwezo wa kumwongezea mwanamke hamu au nguvu ya kushiriki tendo la ndoa, kinachofanywa na wafanyabishara hao ni kutafuta pesa.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

“Hata mimi nimewahi kuzisikia hizo pipi, lakini siwezi kuzungumzia, ninachofahamu mapenzi ni mawasiliano, mkiwasiliana utajua mwenzio anataka nini na wewe unataka nini, mtafika mahali pazuri. “Kama hamzungumzi ni vigumu kufurahia tendo ndio hapo inapokuja kwenye kutafuta dawa na njia nyingine ambazo zinaweza kumuweka mtumiaji hatarini na kumekuwa na ongezeko la wagonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi huenda vitu kama hivi vinachangia,” aliongeza.

Hilo linaelezwa pia na Dk Berno Mwambe, anayesisitiza mapenzi yanahusisha hisia na homoni, hivyo kutumia dawa na kemikali hakusaidii kwenye viungo vyao vya uzazi, bali huishia kuwaletea madhara makubwa kiafya.

Alisema kuzifusha sehemu za siri kunaweza kuathiri vijidudu hivyo na kusababisha kuwashwa, athari nyingine kupata maumivu pia ngozi laini pembezoni mwa sehemu za siri inaweza kuungua au kubabuka.

“Unaweza ukaweka dawa au ukafukisha ukaishia kuvimba, kubabuka na kuungua. Ukiungua itakusababishia makovu ambayo yatakufanya uzichukie sehemu zako. Hapa ndipo athari za kisaikolojia hutokea. “Pia kwa kuweka vitu vya aina hiyo unaweza kupata maambukizi yakiwamo fangasi, miwasho. Ukijihisi una shida yoyote sijui ukavu, maumivu wakati wa tendo ni vema kwenda hospitali ukapate ushauri wa kitaalamu na tiba na sio kuweka vitu ukeni,” alisema Dk Mwambe.

Kuhusu tatizo la kulegea uke, mtaalamu huyo alisema mazoezi ndiyo tiba inayoweza kusaidia kuviweka viungo hivyo katika mwonekano wa kuvutia na salama na sio vitu vingine.

“Ili kuimarisha misuli inayozingira uke, wanawake wanashauriwa kujaribu mazoezi ya sehemu ya chini ya tumbo (pelvic) ya sakafuni yanayoweza kusaidia kuboresha na kuimarisha misuli na uwezo wa kupata shauku ya kushiriki tendo hilo,” aliongeza Dk Mwambe.

Kwa maoni na ushauri kuhusu habari hii tuandikie kupitia 0658376444