Vita ya Lema, wateule wa Rais yafika pabaya

Muktasari:

Kihamia alitoa ‘mashtaka’ hayo jana katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Arusha (RCC) alipoomba nafasi ya kufafanua hoja zilizotolewa na Lema na Meya wa jiji la Arusha, Calist Lazaro kuwa hawezi kutoa uamuzi hadi apate ushauri kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa.

Arusha. Vita ya kisiasa kati ya Godbless Lema na wateule wa Rais imefika pabaya baada ya Mkurugenzi wa Jiji, Athuman Kihamia kudai kuwa mbunge huyo wa Arusha Mjini kwa tiketi ya Chadema amemdhalilisha kwa kudai ‘ameolewa na mkuu wa mkoa huo’, Mrisho Gambo.

Kihamia alitoa ‘mashtaka’ hayo jana katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Arusha (RCC) alipoomba nafasi ya kufafanua hoja zilizotolewa na Lema na Meya wa jiji la Arusha, Calist Lazaro kuwa hawezi kutoa uamuzi hadi apate ushauri kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa.

Katika kikao hicho ambacho Lema, Lazaro na Gambo walihudhuria, Kihamia alisema mbunge huyo alimdhalilisha Oktoba 19 katika kikao cha kamati ya mipango miji.

Mkurugenzi huyo alisema kauli hiyo ilimdhalilisha sana mbele ya watumishi wake, lakini ameamua kuwasamehe na ataendelea kufanya kazi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu.

Mbali ya tukio hilo, Mkurugenzi huyo alisema amekuwa akidhalilishwa kwenye vikao na viongozi hao lakini kamwe hawezi kuacha kutekeleza wajibu wake na akakiri kwamba ni kweli amewazuia wakuu wa idara kuwasiliana moja kwa moja na madiwani.

Akifafanua hoja hiyo, Mkurugenzi huyo alisema kanuni ya 70 (i-v) na kanuni ya 71 zinaeleza wazi kuwa madiwani katika masuala ya utendaji wanapaswa kuwasiliana na mkurugenzi na siyo mtendaji mwingine.

Japo Kihamia alisema amesamehe alimtaka Mbunge Lema amwombe radhi kwa kudai kuwa mkurugenzi huyo anaongoza halmashauri mbili; moja ni ya jiji la Arusha na nyingine ni ya mkoa jambo ambalo alisema siyo sahihi.

Pia, Mkurugenzi huyo alimlalamikia Meya Lazaro kuwa alimtukana kwenye kikao cha Alat kilichofanyika mkoani Mara hivi karibuni na kwamba hawezi kuyataja matusi mengine mbele ya kikao hicho.

“Mheshimiwa Mwenyekiti uligusia kwamba Meya amenitukana kule Musoma ni kweli na matusi mengine hayatamkiki, lakini nina uwezo wa kuvumilia matusi yao na ndiyo maana jiji linaenda bila ngumi,” alisema Kihamia.

Malalamiko hayo yalikuwa majibu ya Mkurugenzi huyo dhidi ya kauli ya Lema ambaye awali alisema katika kikao hicho kwamba shughuli zote za maendeleo zimesimama katika jiji la Arusha kutokana na mgongano wa viongozi jambo ambalo linapaswa kutatuliwa.

Lema alisema Baraza la madiwani liliagiza kuondolewa kwa wamachinga katikati ya mji, kubomolewa nyumba zilizojengwa katika maeneo yaliyovamiwa eneo la Block J, lakini hakuna utekelezaji.

Pia, alisema viongozi wa wilaya hiyo, wanashindwa kufanya maamuzi kwa kumuogopa mkuu wa mkoa jambo ambalo siyo sahihi. “Hadi sasa tusema hatutashiriki vikao vyote vya baraza la madiwani hadi mwafaka upatikane,”alisema Lema.

Awali, Meya Lazaro alilalamikia serikali kushindwa kulisaidia jiji kufanya kazi kwa kushindwa kuwaondoa machinga na gereji bubu katikati ya mji.

Baadaye, akizungumza katika kikao hicho, Gambo alisema hata yeye amekuwa akitukanwa lakini ameamua kukaa kimya na kufanya kazi na akaonya kuwa yupo tayari kupambana na yeyote kwa maslahi ya wananchi.

Alisema kuna taswira ambayo inataka kujengwa sasa kuwa Arusha haitawaliki jambo ambalo siyo sahihi na kwa kushirikiana na vyombo vingine atahakikisha Arusha inaendelea kuwa shwari na ambaye analeta vurugu atashughulikiwa kwa mujibu wa sheria na taratibu.

“Ukija kistaarabu tutamaliza mambo kistaarabu lakini ukija kimjinimjini basi na sisi tutafanya mambo kimjinimjini,” alisema.

Kuhusu tishio la madiwani wa jiji la Arusha kususia vikao, alisema kufanya hivyo hakutaathiri shughuli za maendeleo ya wananchi kwani tayari walipitisha bajeti ambayo itaendelea kutekelezwa na watendaji.

Mkuu wa mkoa alisikitishwa na taarifa ya kudhalilishwa mkurugenzi wa jiji na akamhoji kama yeye si “riziki” na mkurugenzi akajibu yeye ni mwanaume rijali na haelewi kama kuna mwanaume ambaye anaolewa.

Kauli ya Gambo kwamba yupo tayari kupambana na yeyote kwa maslahi ya wananchi itakuwa tahadhari kwa Lemba aliyejipambanua kuwa mbuyu wa siasa katika jiji hilo baada ya kuthubutu kuzima juhudi za wakuu watatu wa mkoa wa Arusha waliotaka kumfifisha.

Lema ni nani

Lema amejijengea umaarufu tangu akiwa mwanachama na kiongozi ngazi wa mkoa wa Arusha katika chama cha Tanzania Labour Party (TLP). Mwaka 2005 aligombea ubunge kupitia TLP lakini aliangushwa na Felix Mrema (CCM) aliyeibuka mshindi.

Mwaka 2009 alihamia Chadema na moto wake na mwaka 2010 aligombea Arusha Mjini na kumshinda Dk Batilida Buriani wa CCM. Tangu mwaka huo, Lema anatajwa kuwa mmoja wa viongozi waliotoa mchango mkubwa wa kuijenga Chadema katika Kanda ya Kaskazini.

Mapambano yake ya kwanza yalikuwa kumpata meya wa jiji hilo. Maandamano ya kitaifa yaliyofanyika Januari 5, 2011 kupinga utaratibu uliotumiwa na halmashauri ya jiji kumpata meya Gaudence Lyimo yalisababisha vifo vya watu watatu na majeruhi kadhaa.

Lema pamoja na viongozi wa kitaifa; Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na aliyekuwa Katibu Mkuu, Dk Wilbrod Slaa walifunguliwa kesi ya kufanya mkusanyiko usio halali. Kila Lema na viongozi wa kitaifa walipofunguliwa kesi kadhaa kwa madai ya kufanya mikusanyiko isiyo ya halali, aliendelea kuungwa mkono na wafuasi wengi hasa vijana.

Baadaye Lema na Chadema yake walishiriki vikao kadhaa vya majadiliano kutafuta suluhu ya suala la umeya na majadiliano yaliposhindikana, huo ukawa mwanzo wa maandamano nchi nzima kulaani walichoita ubakaji wa demokrasia.

Septemba 2011, Shirima alistaafu na nafasi yake ilichukuliwa na aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Magessa Mulongo. Ilikuwepo misuguano ya chini kwa chini lakini mkubwa ulitokea mwaka 2014.

Katika msuguano huo, Mulongo alimtuhumu Lema kumtolea lugha ya kumdhalilisha mbele ya wanafunzi wa Chuo cha Uhasibu Arusha, viongozi hao walipokwenda kuwasikiliza na kuwazuia wasiandamane baada ya mmoja wao kuuawa na watu wasiojulikana.

Ilidaiwa kwamba Lema alimwambia Mulongo kuwa alikwenda chuoni kama vile kwenye kitchen party. Kauli hiyo ilidaiwa kumuudhi Mulongo.

Lema alikamatwa na Polisi akafunguliwa kesi ambayo baadaye ilifutwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP). Hata hivyo, msuguano uliendelea hadi Mulongo alipohamishiwa Mkoa wa Mwanza.

Desemba 2014 nafasi yake ilichukuliwa na Daudi Felix Ntibenda. Hakukuwa na msuguano mkubwa kati ya Ntibenda na Lema na jiji lilionekana kuwa shwari hali iliyoonekana kuipa nafasi Chadema kujijenga vizuri na kufanikiwa kushinda kata 24 kati ya 25 katika uchaguzi mkuu 2015 na hivyo kufanikiwa kuongoza halmashauri ya jiji.

Agosti 2016 Ntibenda aliondolewa na nafasi yake ilichukuliwa na Mrisho Gambo aliyepandishwa kutoka ukuu wa wilaya ya Arusha. Siku moja tu baada ya uteuzi wa Gambo kuwa mkuu wa mkoa wa Arusha, Lema alieleza kusikitishwa akisema anaona Arusha ikirejea kuwa katika migogoro isiyo na sababu.

Gambo ni nani

Gambo amekuwepo katika halmashauri ya Arusha tangu mwaka 2009 alipoajiriwa kama mchambuzi wa mifumo ya kompyuta. Baadaye alikuwa mjumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Jumuiya ya Vijana wa CCM (UVCCM) mkoa wa Arusha na iliingia kwenye mgogoro mkubwa na aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa na kambi yake.

Mwaka 2012 aliteuliwa kuwa mkuu wa wilaya ya Korogwe. Utumishi wake wa muda mfupi ulisababisha kufikishwa katika Baraza la Maadili kwa ukiukwaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Gambo alifikishwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa matumizi mabaya ya uongozi yakiwemo matumizi ya lugha chafu, kukiuka sheria mbalimbali pamoja na ubabe wakati wa kutekeleza majukumu yake kama Mkuu wa wilaya ya Korogwe.

Februari 18, 2015 alipumzishwa ukuu wa wilaya, lakini Mei 10, 2015 aliteuliwa tena kuwa Mkuu wa wilaya ya Uvinza, Kigoma alikokaa hadi Julai 2016 alipohamishiwa kuwa Mkuu wa wilaya ya Arusha. Gambo alilumbana na Lema Agosti Mosi mbele na Naibu Waziri wa Tamisemi, Suleiman Jafo.

Katika tukio hilo, Lema alisema Gambo haheshimu mipaka ya kazi zake, akimtuhumu kuingilia maamuzi ambayo tayari yameshajadiliwa kwenye vikao halali vya halmashauri na kupitishwa na ofisi ya mkuu wa mkoa katika kikao cha wakuu wa idara, maofisa tarafa, waratibu wa elimu kata watumishi wa Mamlaka ya Maji Safi na Mazingira (Auwsa) jijini hapo.

Siku chache baadaye Gambo alipandishwa kuwa mkuu wa mkoa wa Arusha kuchukua nafasi ya Ntibenda. Gambo akatangaza kufutwa baadhi ya posho za madiwani na kupunguza nyingine licha ya kwamba zilipitishwa tangu mwaka 2008 halmashauri hiyo ilipokuwa inaongozwa na CCM.

Mapema wiki hii Gambo aliingia katika mapambano na Lema binafsi wakati mkuu wa mkoa huyo alipoalikwa kuzindua ujenzi wa hospitali ya mama na mtoto, itakayojengwa kwa ufadhili wa taasisi ya Martenity Africa. Mzozo huo ulizuka baada ya Gambo kueleza historia ya kiwanja cha jengo hilo, maelezo ambayo Lema aliyapinga kwa sauti na kusababisha shughuli hiyo kuvurugika.