Vituo bubu vya kulea watoto Shinyanga mtegoni
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, akizungumza na wamiliki wa vituo vya kulea watoto mchana katika Manispaa ya Shinyanga.
Muktasari:
- Serikali imetoa siku 10 kwa kamati maalumu kubaini vituo bubu vya kulea watoto mchana na ambavyo havijasajiliwa kutokana na kuanzishwa kiholela.
Shinyanga. Vituo 25 vya kulea watoto mchana katika Wilaya ya Shinyanga vimebainika kufanya shughuli zake bila usajili, hali inayokiuka sheria na miongozo ya uendeshaji wa vituo hivyo.
Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, ameagiza kuundwa kwa timu maalumu ya kufuatilia na kufanya uhakiki wa vituo hivyo ili kubaini hali halisi na hatua stahiki zichukuliwe.
Akizungumza leo Julai 21, 2026, katika kikao na wamiliki wa vituo vya kulea watoto mchana, walezi, watendaji wa kata na wenyeviti wa mitaa, Mtatiro amesema uendeshaji wa kituo cha kulea watoto bila usajili ni ukiukwaji wa sheria na miongozo ya Serikali.
Amesema Wilaya ya Shinyanga ina jumla ya vituo 76 vya kulea watoto mchana, ambapo 25 havijasajiliwa.
Mtatiro ameitaka timu hiyo kukamilisha kazi yake na kuwasilisha ripoti ya kina ndani ya siku 10.
Kwa mujibu wa Mtatiro, timu hiyo itafanya tathmini ya kila kituo ili kubaini vile vinavyoendeshwa kinyume cha utaratibu, vinavyokosa sifa za msingi na vile vyenye mapungufu yanayoweza kurekebishwa.
Baada ya kupokea ripoti hiyo, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya itatoa maelekezo ya hatua zitakazochukuliwa.
"Kazi yangu ni kutoa maelekezo na kusimamia utekelezaji wa sheria za nchi. Ripoti iliyowasilishwa imeonyesha mafanikio yaliyopo katika malezi ya watoto, lakini pia imebaini uwepo wa vituo vinavyoendelea kufanya kazi bila kufuata maelekezo yaliyotolewa awali,"amesema Mtatiro.
Ameagiza uchunguzi huo ukamilike ifikapo Julai 30, 2026, na kuongeza kuwa baada ya hapo vituo vyote vitakavyobainika kuwa na changamoto vitapewa muda wa wiki tatu kurekebisha mapungufu yao kabla ya hatua zaidi kuchukuliwa.
Mwenyekiti wa Wamiliki wa Vituo vya Kulea Watoto Mchana katika Manispaa ya Shinyanga, Damari Molles, amesema uwepo wa vituo visivyosajiliwa umekuwa changamoto kwa kuwa vinatoza ada ndogo na hivyo kuvutia wazazi, jambo linalosababisha vituo vinavyofuata taratibu kupoteza watoto.
Molles amesema umoja wa wamiliki wa vituo hivyo ulianzishwa mwaka 2022 kwa lengo la kuwaunganisha wamiliki, kuhamasisha usajili wa vituo na kuhakikisha huduma za malezi zinatolewa kwa kuzingatia Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 na miongozo ya Serikali.
Kwa upande wake, Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Shinyanga, Lydia Kwesigabo, amesema baadhi ya wamiliki wamekuwa wakikaidi kusajili vituo vyao licha ya kuwatoza wazazi ada.