Vyama vya upinzani vyapigwa ‘stop’ kampeni Tarime

Muktasari:

Badala yake ofisi hiyo imetangaza kampeni hizo kuendelea kwa chama kimoja tu cha CCM.


Dar es Salaam. Ofisi ya msimamizi msaidizi wa uchaguzi Kata ya Turwa wilayani Tarime imesitisha kampeni za vyama vyote vya upinzani kwa siku mbili jana na leo ambayo ni siku ya mwisho ya kampeni.

Badala yake ofisi hiyo imetangaza kampeni hizo kuendelea kwa chama kimoja tu cha CCM.

Kwa mujibu wa barua ya msimamizi msaidizi wa uchaguzi Kata ya Turwa, Peter Julius, uamuzi huo unatokana na vyama hivyo kukiuka kifungu cha 124A cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, sura ya 343, Maadili ya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani ya mwaka 2015.

Msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Tarime Elius Mtiruhungwa alipoulizwa kuhusiana na hilo alisema; “Barua hiyo ni halali na inajieleza yenyewe sababu ya kamati ya maadili ya kata ndiyo iliyofikia uamuzi huo.”

Alisema kamati iliyotoa adhabu hiyo ina mamlaka yote, “Kamati imekaa na kuona adhabu hiyo ndiyo inastahili licha ya sheria kuruhusu adhabu nyingine kama kulipa faini ya fedha taslimu lakini wao wameona hiki ndicho wanachostahili kwa hiyo mimi sina mamlaka ya kupingana nao.”

Mbatia, Zitto wanena

Akizungumzia hatua hiyo, Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi James Mbatia alisema mambo yanayofanywa na watu wenye mamlaka yanatia hasira.

“Ukishaweka utaraibu usipofuata ni tatizo, suala la kampeni siyo hisani lipo kisheria sasa watu wachache wenye mamlaka katika nchi wanajitwalia madaraka na kuvunja sheria hii siyo sawa,” alisema mbunge huyo wa Vunjo.

“Tumefika mahali kazi iliyofanywa kwa zaidi ya miaka 20 kuwa na mfumo wa vyama vingi imekuwa bure kila mtu analalamika,” alisema.

Zitto aliitupia lawama CCM akisema hiyo ni dalili kwamba wameishiwa pumzi hivyo wanataka wafanye kampeni peke yao.

“Jana nilihutubia jukwaa la NCCR-Mageuzi ndio maana CCM imekasirika. Juzi walinizuia kuongea jukwaa la Chadema.

Alisema CCM haikubaliki kwa sababu masuala ya demokrasia yanadidimia nchini.

CCM yaeleza chanzo

Katibu wa CCM Wilaya ya Tarime, Hamis Mkaruka alisema sababu ya kuandika barua ya malalamiko ni baada ya cha NCCR Mageuzi kuwaruhusu Chadema kumnadi mgombea wao.

Alisema Chadema walizuiliwa kufanya kampeni lakini cha kushangaza, mkutano wa juzi wa NCCR waliwakaribisha na kuanza kumnadi mgombea wao badala ya kumnadi wa NCCR Mageuzi pekee.

“Eti wanajiita Ukawa! Ukawa haijasajiliwa rasmi na wangekuwa Ukawa wangesimamisha mgombea mmoja sasa wao wakanadi wagombea wote, hii siyo haki tumelalamika kwa kuwa hatujatendewa haki mkutano mmoja unanadi wagombea wawili wa vyama tofauti.”

Mkaruka pia aliitaka Tume ya Taifa ya uchaguzi (NEC) kubadili sheria itakayotaka mawakala wawe ni wa kutoka chama kimoja kwa madai kuwa mawakala wa NCCR ni wafuasi wa Chadema.

Kata 77 na Jimbo la Buyungu zinafanya uchaguzi mdogo kesho.

zinaingia katika uchaguzi wa marudio ambako tayari CCM imeshajihakikishia ushindi katika kata 40 baada ya wagombea wake kupita bila kupingwa.

Kwazaidi ya wiki mbili vyama vya upinzani pamoja na chama tawala hivyo vimekuwa vikichuana katika kampeni kwa lengo la kunadi sera ya vyama vyao ili kujihakikishia ushindi.

Hata hivyo, kampeni katika Kata ya Turwa zilionekana kuwa tofauti na kata nyingine kufuatia kuzuka kwa vurugu na kusababisha Jeshi la Polisi wilayani Tarime kutumia mabomu ya machozi katika mkutano wa Chadema.

Katika vurugu hizo viongozi kadhaa wa chama hicho walikamatwa akiwamo mbunge wa Esther Matiko na mwandishi Sitta Tuma. Hata hivyo kwa sasa jeshi hilo limewaachilia na kuwataka kuripoti kituo hapo.