Vyuo vikuu vinne kutafiti athari mabadiliko ya tabianchi

Muktasari:

  • Vyuo vikuu vya Aga Khan, SUA, UDSM Simon Fraser (SFU) Canada na taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela vimeingia makubalianbo ya kushirikiana katika utafiti wa changamoto za mabadiliko ya tabia nchi ili kukabiliana na athari zake.

Arusha. Taasisi nne za elimu ya juu nchini pamoja na Chuo Kikuu cha Canada zimetia saini hati ya makubaliano (MoU) ya ushirikiano ya kufanya mfululizo wa utafiti wa kina kuhusu mabadiliko ya tabianchi ili kukabiliana na athari zake.

Taasisi hizo zinahusisha Chuo kikuu cha Aga Khan, Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Simon Fraser (SFU) cha Canada na taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela ya Arusha.

Makubaliano hayo yaliyoongozwa na Chuo kikuu cha Aga Khan yamefanyika leo Novemba 11 jijini Arusha yakishuhudiwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda.

Akizungumzia makubaliano hayo, Profesa Mkenda amesema kuwa changamoto ya mabadiliko ya tabia ya nchi inahitaji kushirikiana kuendeleza utafiti hasa kuleta mabadiliko kwenye kilimo, kwa ajili ya uhakika wa chakula katika nchi za Afrika.

"Ni wakati mwafaka kwa taasisi zetu za elimu ya juu kuchukua mtazamo wa kimataifa katika mafunzo na utafiti kwani karibu theluthi mbili ya watu wetu wanategemea kilimo, na mabadiliko ya hali ya hewa yanafanya kuwa vigumu kuhakikisha usalama wa chakula na maisha,” amesema Waziri Mkenda.

Amesema kuwa utafiti huo unaweza kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya mazingira na kilimo nchini na kuondokana  kabisa na changamoto ya mabadiliko ya tabia ya nchi na kuwa na uhakika wa chakula cha kutosha kwa matumizi na biashara.

Kwa upande wake, Rais wa Chuo kikuu cha Aga Khan, Dk Sulaiman Shahabuddin alisema kuwa mabadiliko ya hali ya hewa ni jambo kubwa duniani kote na inahitaji juhudi zaidi za makusudi katika kudumisha uendelevu wa mazingira duniani kote.

“Kwa sababu hii Chuo Kikuu cha Aga Khan kupitia Kituo chake cha Utafiti wa Hali ya Hewa na Mazingira cha Arusha (AKU-ACER) kiko mstari wa mbele katika kuanzisha utafiti wa msingi wa kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa,” amesema.

Amesema kwa pamoja, taasisi hizo kwa kubadilishana wanafunzi zitafanya utafiti unaolenga kuendeleza mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kutoa maarifa muhim za maamuzi ya sera nchini ili kutafuta ufumbuzi wa tatizo na uendelevu wa mazingira.

Akizungumzia makubalinao hayo Rais wa Chuo kikuu cha Simon Fraser ‘SFU’ cha Canada, Dk Joy Johnson alieleza kufurahia wanafunzi wa chuo hicho kupata fursa ya kusoma nchini Tanzania.

Kwa upande wake Kansela wa Taasisi ya Afrika ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia (NM-AIST), Profesa Issa Omari amesema kuwa ushirikiano huo tunalenga katika kuwezesha jamii kwa kutoa masuluhisho yanayosaidia idadi kubwa ya watu.