Waajiri watakiwa kulinda usalama na afya za wafanyakazi

Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako wa tatu kulia akipiga makofi wakati akipokea maandamano ya wafanyakazi wa taasisi na makampuni mbalimbali yaliyoshiriki katika maadhimisho ya siku ya usamala na afya mahali pa kazi yaliyoandaliwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), pembeni yake ni Mkurugenzi wa OSHA, Hadija Mwenda. Picha Hamida Shariiff.

Morogoro. Waziri nchi ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu, Profesa Joyce Ndalichako amewaagiza waajiri kutekeleza jukumu lao la msingi la kulinda usalama na afya za wafanyakazi kwa kuwa ni takwa la kisheria.

 Profesa Ndalichako ametoa agizo hilo jana mjini hapa katika Viwanja vya Tumbaku wakati akifungua maadhimisho ya siku ya usalama na afya mahali pa kazi yaliyoandaliwa na wakala wa usalama na afya mahali pa kazi Osha kwa kushirikiana na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) na Shirika la Kazi Duniani ILO.

Amesema kuwa yapo magonjwa na ajali nyingi zinazotokea mahali pa kazi ambazo kama kungekuwa na mifumo thabiti ya usalama na afya mahali pa kazi zingeweza kuepukika hivyo wizara itaendelea kusimamia masuala ya usalama na afya ili kulinda nguvu kazi ya Taifa.

Aidha ameitaka Osha kuendelea kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa sekta isiyokuwa rasmi wakiwemo waendesha bodaboda ili wajue namna ya kulinda usalama na afya zao wakati wakitekeleza majukumu yao na kusisitiza mafunzo hayo kuwa endelevu.

Katika hatua nyingine Profesa Ndalichako amesema kuwa hadi sasa bado dawa ya kutibu virusi vya Ukimwi haijapatikana hivyo waajiri wanapaswa kuweka mifumo itakayowasaidia wafanyakazi wanaoishi na VVU badala ya kuwanyanyapaa.

"Hawa wafanyakazi wenzetu ambao kwa bahati mbaya wamepata maambukizi ya VVU muwape vipaumbele katika masuala mbalimbali katika maeneo ya kazi yakkwemo matibabu ili waweze kulitumikia Taifa," amesema Prof. Ndalichako.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Osha, Hadija Mwenda amesema kuwa hapa nchini sekta ya uzalishaji inaongoza kwa ajali zinazosababisha vifo na majeraha yanayotokea mahali pa kazi huku ikifuatiwa na sekta ya ujenzi na madini huku vijana wakiwa ndio waathirika wakubwa wa madhara hayo.

Hata hivyo amesema kuwa katika kusimamia afya na usalama mahali pa kazi Tanzania imekuwa ni nchi ya kuigwa na hii ni kutokana na mifumo iliyopo pamoja na mafunzo yanayotolewa kwa makundi mbalimbali wakiwemo wajasiriamali ambao wamefikiwa na kupewa mafunzo.

Amesema kuwa katika kipindi hiki ambacho Serikali imeongeza ajira viashiria vya madhara yatokanayo ya kazi nayo yanaweza kuongezeka hivyo lazima waajiri wazingatie viwango vya usalama na afya mahali pa kazi vilivyowekwa kisheria.

Naye Rais wa Tucta, Tumaini Nyamhokya ameiomba serikali kuhakikisha wawekezaji wanaokuja kuwekeza hapa nchini wanafuata miongozo na sheria za usalama na afya mahali pa kazi na kuunda kamati za usalama na afya mahali pa kazi na kwa watakaoshindwa kufuata sheria za usalama na afya mahali pa kazi wapewe adhabu kali.