Ndalichako aahidi kupambana na ajali, magonjwa maeneo ya kazi

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako akizungumza na Waandishi wa Habari leo Aprili 26, 2023.

Muktasari:

  • Waziri Ndalichako amesema Serikali inaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa sheria namba tanbo ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003.

Dodoma. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na wenye ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako amesema Serikali inaendelea kuhakikisha maeneo yote ya kazi nchini yanakuwa na mifumo madhubuti ya kuwakinga wafanyakazi dhidi ya ajali na  magonjwa yatokanayo na kazi.

 Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Jumatano,Aprili 26,2023 kuhusu siku  ya kimataifa ya usalama na afya mahala pa kazi duniani ambayo kitaifa  inatarajiwa kufanyika Aprili 28 mwaka huu mkoani Morogoro.

Waziri Ndalichako amesema kupitia Wakala wa Usalama na Afya Mahala Pa Kazi (Osha) Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri ya ufanyaji kazi nchini.

Amesema Serikali inaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa Sheria namba tano ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 miongoni mwa wadau na Watanzania wote kwa ujumla.

“Lengo ni kuhakikisha kwamba maeneo yote ya kazi nchini yanakuwa na mifumo madhubuti ya kuwakinga wafanyakazi dhidi ya ajali na magonjwa yatokanayo na kazi,”amesema

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (Osha), Hadija Mwenda amesema watahakikisha mazingira ya ufanyaji kazi nchini yanakuwa salama huku akiwataka wafanyakazi kujiunga na wakala huo.