Waandishi wapewa mbinu za kuandika habari za utunzaji wa mazingira

Mkurugenzi wa Shirika linalojihusisha na utunzaji wa Mazingira la Good Harvest Organization, Filibert Chundu akizungumza na waandishi wa habari namna ya kuandika habari zinazohusu utunzaji wa  mazingira, wanyamapori pamoja na mabadiliko ya tabianchi. Picha na Hadija Jumanne

Muktasari:

  • Katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na utunzaji wa mazingira katika vyanzo vya maji, wadau wa mazingira wamewataka waandishi wa Habari kujikita kuandika habari za kuelimisha jamii kuhusiana na athari zinayotokana na uharibifu wa mazingira,  kuliko kutumia muda mwingi katika mitandao ya kijamii kuandika vitu ambavyo havina tija kwa jamii.



Katavi. Katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na utunzaji wa mazingira katika vyanzo vya maji, wadau wa mazingira wamewataka waandishi wa Habari kujikita kuandika habari za kuelimisha jamii kuhusiana na athari zinayotokana na uharibifu wa mazingira,  kuliko kutumia muda mwingi katika mitandao ya kijamii kuandika vitu ambavyo havina tija kwa jamii.

Pia, wadau hao wameomba kuwepo kwa juhudi za pamoja baina ya Mamlaka za Uhifadhi wa Mazingira, Serikali, Wanasiasa na vyombo vya habari ili kunusuru mabadiliko ya tabia nchi yasilete kwa kutoa elimu endelevu kwa wananchi na namna ya kukabiliana na tatizo hilo, ambalo linatishia ukame dunia.

Mkurugenzi wa Shirika linalojihusisha na utunzaji wa Mazingira la Good Harvest Organization, Filibert Chundu alisema mwanzoni mwa wiki,  wakati akitoa mafunzo ya kuwajengea uwezo, waandishi wa habari namna ya kuandika habari zinazohusu utunzaji wa  mazingira, wanyamapori pamoja na mabadiliko ya hali ya tabianchi.

Chundu alisema iwapo waandishi wa Habari watapewa mafunzo ya namna ya kuandika habari zinazohusu utunzaji wa mazingira, watapeleka elimu nzuri kwa jamii na hivyo jamii itapata uelewa mpana wa kutunza mazingira.

" Niviombe vyombo vya habari vitoe fursa ya kuona umuhimu wa kuandaa, kurusha vipindi na habari mbalimbali zianazohusu utunzaji wa mazingira, kwani kwa kufanya hivyo vitakuwa vinasaidia jamii kupata uelewa wa kutunza mazingira na namna ya kutunza mazingira katika maeneo yao" alisema Chundu na kuongeza

Awali, Mkufunzi wa mafunzo hayo, Prosper Kwigize alisema lengo la kutoa mafunzo hayo kwa waandishi wa habari ni kuwafanya wawe mabalozi wa mazingira kupitia vipindi na habari mbalimbali watakazoandika ambazo zitakwenda kuelimisha jamii juu ya uhifadhi wa mazingira katika jamii zao.

" Tumeona kuna changamoto kubwa kwani  jamii inakabiliwa na tatizo la uharibifu wa mazingira unasabishwa na shughuli za kibinadamu kama kulima katika vyanzo vya maji, kukataji miti ovyo, kufuga mifugo hifadhini, uchimbaji wa mchanga pembezoni mwa vyanzo vya maji ni miongoni mwa vitu vinavyochangia kuwepo kwa athari ya mabadiliko ya tabia nchi, ambayo kwa sasa yametikisa dunia" alisema Kwigize

Kwigize aliwataka waandishi wa habari kujikita katika kuandika habari za mazingira, kuibua changamoto zinazotokana uhalibifu wa mazingira na na kuzipatia ufunguzi, jambo ambalo litaisaidia jamii kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.


Kwa upande wake, Silesi Malli Malli,  ambaye ni mwenyekiti asasi ya Umoja wa Mataifa inayoangalia Utekelezaji wa matamko ya umoja huo katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, alisema licha ya Serikali kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya madhara ya uharibifu wa mazingira katika vyanzo vya maji, bado juhudi za makusudi zinahitajika kukabiliana na tatizo hilo.


Malli alisisitiza kuwa jamii inao wajibu mkubwa wa kutunza mazingira kama itapewa elimu ya kutosha kukabiliana na uharibifu wa mazingira.


"Tuendelee kutoa elimu ya mazingira endelevu lakini tukumbushane kwa pamoja kutunza na kuhifadhi mazingira ikiwemo vyanzo vyetu vya maji" alisema Malli.


Akizungumza kwa niaba ya waandishi wa habari waliopatiwa mafunzo, Rais wa umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari nchini,  Deogratias Nsokolo, aliwaasa waandishi kuandika habari za kuelimisha wananchi kuhusu madhara ya uharibifu wa mazingira, jambo ambalo litaondokana na uharibifu wa mazingira.


Jumla ya waandishi wa habari 20 kutoka mkoa wa Kigoma, Katavi, Tabora, Rukwa  na  Dar es Salaam waalipatiwa mafunzo hayo ambayo yatakuwa endelevu, lengo ni kuungana na Serikali katika kupiga vita uharibifu wa mazingira unaofanywa na jamii.