Wabunge, Meya Dar wamjibu Makonda

Dar es Salaam. Wakati Paul Makonda akidai wabunge wa upinzani mkoani Dar es Salaam hawashiriki shughuli za maendeleo na kueleza shida za majimbo yao, wabunge hao wamemjibu huku Halima Mdee (Kawe) akisema mkuu huyo wa mkoa ndiye anayepaswa kusimamia maendeleo hayo.

Juzi Makonda aliwataja wabunge watatu wa Chadema-- Saed Kubenea (Ubungo), John Mnyika (Kibamba) na Mdee- katika hafla ya kupokea ndege ya Boeing 787-8 Dreamliner katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

Mbele ya Rais John Magufuli, mkuu huyo wa mkoa aliwatuhumu wabunge hao kuwa hawakuwa wanawatumikia wananchi na pia ni ‘wezi’ wanaokula posho bungeni bila kufanya kazi kwa ajili ya wananchi huku akimuomba mkuu huyo wa nchi Sh1.5 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya Ubungo, ombi ambalo liliridhiwa na Magufuli.

Akizungumza jana, Mdee alisema maendeleo ya mkoa yanaletwa kwa ushirikiano kati ya mkuu wa mkoa, wabunge, wakurugenzi wa halmashauri zote kwa kuitisha vikao visivyopungua vinne kwa mwaka kujadili miradi mbalimbali.

“Vikao hivi havifanyiki na pia kuna vikao vya mfuko wa barabara ambavyo anatakiwa akae na Wakala wa Barabara (Tanroads) kuhusu hali ya miundombinu yetu na kuiboresha, lakini hafanyi hivyo, tofauti na wenzake waliomtangulia,” alisema Mdee.

Alisema mkoa hauwezi kuendelea kwa siasa na kudhalilisha wapinzani na kuongeza kuwa hivi sasa miundombinu ya jiji ni mibovu na kila halmashauri inafanya kazi kivyake.

“Mafuriko kila kukicha, lakini kazi yao ni kututupia lawama sisi wapinzani hata kwenye vikao vyao vya ndani wanavyokaa vinalenga kutudhalilisha tu,” alisema.

Kuhusu kutohudhuria mapokezi ya ndege alisema “nilikuwa Dodoma, lakini pia siwezi kuhudhuria sherehe ambayo sijapewa mwaliko.”

Wakati Mdee akieleza hayo, Mnyika alisema madai ya Makonda hayana ukweli bali ni propaganda za kisiasa na kumtaka alinganishe majimbo yao na yale ya wabunge wa CCM ya Mbagala, Ukonga, Temeke, Ilala na Segerea.

“Hilo ombi alilotoa Makonda jana kuhusu Hospitali ya Ubungo nilishampatia Rais John Magufuli tangu Desemba 2018... lakini pia niliwasilisha bungeni kwa mawaziri wanaohusika. Manispaa ya Ubungo iliingiza suala hilo kwenye bajeti yake Februari, mwaka huu na Julai ikapitishwa hivyo Makonda kusema hatujafanya kazi za wananchi ameudanganya umma na Rais,” alisema Mnyika, ambaye alimtuhumu Makonda kuwa anahamisha mjadala kutoka watu kuhoji manunuzi ya ndege badala ya fedha kuelekezwa kwenye miradi na Katiba mpya.

Kwa upande wake, Kubenea alisema kuwa siyo kweli kwamba hawashiriki shughuli za maendeleo na kwamba hakwenda kupokea ndege kwa kuwa alijua yatazungumzwa maneno ya kumdhalilisha.

Akizungumzia kuhusu Makonda kuomba Sh1.5 bilioni za ujenzi wa hospitali ya Ubungo, Meya wa Ubungo, Boniface Jacob alisema, “Angekuwepo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala na Serikali za Mitaa, Seleman Jafo angetusaidia kulifafanua hili mbele ya Rais Magufuli kwa sababu anajua ukweli na ndiye aliyepitisha fedha hizi, ambazo tunasubiri ziingie kwenye akaunti ili tuanze ujenzi.”

Akijibu hoja ya fedha hizo, mkurugenzi mtendaji wa Manispaa ya Ubungo, Beatrice Dominic alisema katika kipindi cha miaka miwili iliyopita hawakuwahi kutenga Sh1.5 bilioni za ujenzi wa Hospitali ya Ubungo na akamshukuru Magufuli kwa kutoa kiasi hicho cha fedha.

“Hatujawahi kuweka Sh1.5 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa hospitali, kwetu kupokea kiasi hiki cha fedha ni faraja kubwa kwa sababu hatukuwahi kutenga kiasi hiki mwaka jana wala mwaka juzi,” alisema.

“Nimeona si vyema kukaa kimya kwa sababu jambo hili ni kubwa..”