Wabunge waonyeshwa maeneo hatari ya ulaji
Baadhi ya wabunge waliohudhuria semina Hiyo
Muktasari:
- Ni maeneo hatarishi ambayo wanatakiwa kuyatambua na kuyafanyia kazi
Mkaguzi wa Nje Mwandamizi wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (Naot), Deogratias Kirama amewaonyesha maeneo tata ambayo wabunge wanatakiwa kuyatilia mkazo wakati wa kuangilia matumizi mabaya ya Serikali kuwa ni pamoja uwekezaji, malipo ya kazi za ziada (extra duties) na mikataba.
Kirama amesema hayo wakati akiwasilisha mada kwa wabunge wa kamati nne za bunge kuhusu wajibu wa wabunge na ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za umma.
Semina hiyo imehusisha wajumbe wa Kamati ya Bajeti, Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Hesabu za Serikali (PAC) na Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC).
Kirama amesema katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka wa fedha 2015/16 imeonekana kuwa kuna mifuko ya jamii ambayo imefanya uwekezaji wa majengo wenye mashaka ikiwemo NSSF.
“Haya ni maeneo hatarishi wayatambue na kuyafanyia kazi wakati wa utendaji wao wa kila siku,”amesema.
Amesema eneo la malipo baada ya saa za kazi limekuwa ni mwanya wa matumizi mabaya ya Serikali kwa watu kujiandikia malipo bila kufanya kazi muda wa ziada.
“Mikataba ni eneo la hatari sana linatakiwa kuliangalia kwa umakini mkubwa kwasababu kesi nyingi tunazozisikia hivi sasa zinatokana na mikataba,”amesema.
Alisema hata hivyo kujenga uwezo kwa wataalam wa kuangalia mikataba kabla ya kusaini ili kuhakikisha ina maslahi kwa umma linatakiwa pia kuangaliwa.
Mbunge wa Ileje (CCM) Janeth Mbene alihoji kuwa ni maeneo gani muhimu ya kuangalia wakati waangalia uwekezaji nchini.
Akijibu Kirama aliwataka wabunge kuangalia mauziano ya ardhi kwa kuangalia thamani halisi na fedha zilizotolewa.
Mbunge wa Rombo (Chadema) Joseph Selasini alisema bila kuangalia upya Katiba ili kulipa uhuru bunge wakutekeleza majukumu yake hayo yanayozungumzwa yatakuwa vigumu.
‘’Lazima Katiba iangaliwe ili muhimili wa bunge na serikali utenganishwe kwa kuhakikisha kuwa chombo hiki kinakuwa na mfuko wake wa fedha na si kama sasa,”amesema.
Mbunge wa Busega (CCM) Raphael Chegeni alisema ili kushughulikia mambo hayo ni muhimu bunge likapata raslimali za kutosha.
Mbunge wa Tunduma (Chadema) Frank Mwakajoka alisema bajeti ya serikali ya maendeleo haiendi katika miradi ya maendeleo kwa asilimia 100.
“Bajeti yetu inatekelezwa chini ya asilimia 50 sijui inatoa ishara gani ama taswira gani?”alihoji.