Wabunge wataka wezi mali za umma kunyongwa, kukatwa vichwa

Muktasari:

  • Ni Mapendekezo ya wabunge wakati wkaichangia Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya mwaka 2021/22 ambapo wanasema wizi umekithiri maeneo ya umma.

Dodoma. Ni wazi kuwa wabunge wamelipuka, sasa wanataka wabadhirifu wa mali ya umma kunyongwa.

Mbali na kuwanyonga wabadhirifu, wabunge wanapendekeza mawaziri wanaolea uovu nao waondolewe kwenye nafasi hizo kwa kuwa hata wakiondolewa watakaoingia watakuwa ni wana CCM.

Mbunge wa Tarime Vijijini (CCM) Mwita Waitara ameibua hoja hiyo leo Alhamisi Novemba 3, 2023 wakati akichangia kwenye Taarifa za Wenyeviti wa Kamati za Bunge kuhusu ripoti ya Ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka 2021/22.

Katika mchango wake leo Waitara amesema hakuna namna nyingine ambayo inaweza kuwa nzuri kama siypo kutoa adhabu ya kuwayonga watu waliohusika ili iwe fundisho

Hata hivyo kumekuwa na mgongano ambapo wanaharakati wanataka adhabu ya kifo iondolewe nchini Tanzania na badala yake uwa na adhabu zingine mbadala ambazo zitatolewa hata kwa wenye hatia za mauaji.

“Nchi ya Korea wenzetu wanatoa adhabu kali ya kuwanyonga watu wanaohusika na ubadhirfu, tunataka kuona watu hao wakinyonga ili kutoa fundisho lakini huu mpango wa kupokea taarifa na kuacha kama ilivyo umekuwa ni mazoea, ikiwa hivi mwakani mimi nikiwa hao sitachangia chochote kama hali ni haii,” amesema Waitara.

Mbunge huyo amesema kuwa kuwanyonga watu wa aina hiyo haitakuwa wameonewa bali watabeba wanachostahili kwa kuwa wanasababisha watoto wa masiki kukaa chini na wananchi kukosa huduma muhimu huku wengine wakiwa wamevimbiwa.

Amesema kabla ya kupokea ripoti hiyo kwenye vikao vya bunge, walitegemea kuona waliotajwa wakiwa wametapika fedha hizo, wengine wawe mahakamani  au wakiwa wamefungwa badala yake wanajadili huku watu wakiwa maofisini.

Hoja ya mbunge huyo imeungwa mkono na Mbunge wa Songwe (CCM), Philip Mulugo ambaye ameomba mwongozo wa Spika ni kwa nini Waitara alipokuwa anachangia mambo ya msingi lakini Mawaziri walikuwa wanachati na simu zao.

Mulugo amesema amesema kitendo cha wizi hakikubariki lakini inapotokea wanaohusika na usimamizi wa mali wanakuwa na mambo mengine ni aibu. Yeye aliomba bunge liunge mkono hoja ya Waitara kwa wahusika wanyongwe.

Mbunge wa Makambako (CCM), Deo Sanga amesema ili kupunguza wala rushwa hakuna namna nyingine yoyote itakuwa nzuri kama si kuwanyonga wahusika kwenye wizi huo.

Sanga amesema ni jambo baya kuona namna ambavyo Rais anahangaika kutafuta fedha lakini wachache wapo kwa ajili ya kula fedha hizo na zinashindwa kwenda kwa wanyonge.

Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka amesema wakati umefika kwa CCM kujitenga na waharifu hivyo mawaziri wachukue hatua kwa watu waiotajwa kwa kuwashughulikia bila kuweka huruma na ikishindikana kufanya hivyo hoja yake ya kutaka Mawaziri wawajibike itabaki kama ilivyo.

Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Kilumbe Ng’enda yeye amesema adhabu nzuri kwa wabadhirifu ni kuwakata vichwa wezi wa mali za umma bila huruma yoyote.