Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wachambuzi waonya hatari ya dunia kubaki bila ICC

Picha na Mtandao.

Muktasari:

  • ICC imekuwa nguzo muhimu ya haki ya kimataifa licha ya ukosoaji kutoka baadhi ya mataifa.

Dar es Salaam. Wakati Marekani ikiendelea kuikosoa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), wachambuzi wa sheria na siasa za kimataifa wanaonya kuwa, shinikizo la kuifuta kunaweza kuiacha dunia bila chombo muhimu cha kuwawajibisha watuhumiwa wa uhalifu.

Onyo hilo linakuja huku mjadala kuhusu mustakabali wa ICC ukiibuka upya katika majukwaa ya kimataifa, miaka 24 tangu ilipoanza kazi rasmi kwa lengo la kuhakikisha hakuna mtu aliye juu ya sheria za kimataifa.

Mjadala huo umechochewa na hatua za Marekani kuendelea kuikosoa Mahakama hiyo, ikiwamo vikwazo vilivyowahi kuwekwa dhidi ya baadhi ya maofisa wake na kupinga uchunguzi unaowahusisha washirika wake wa kimataifa.

Wachambuzi wanaeleza kuwa licha ya upungufu unaotajwa dhidi ya ICC, kuondolewa kwake kunaweza kuwapa baadhi ya viongozi nafasi ya kutenda makosa bila hofu ya kuwajibishwa.


Kampeni ya Trump, uwezo wa ICC

Rais wa Marekani Donald Trump ameanzisha kampeni ya kuipinga Mahakama hiyo, hata hivyo Marekani na nchi zingine za Russia, China, India, Israel, Iran, Korea Kaskazini na Syria siyo wanachama wa ICC,

Hata hivyo, ICC inaweza kuchunguza na hata kutoa hati ya kukamatwa dhidi ya raia wa nchi ambayo si mwanachama wa Mahakama hiyo, iwapo masharti ya kisheria yaliyoainishwa katika Mkataba wa Rome yatatimizwa.

Tofauti na dhana iliyozoeleka, uanachama wa nchi si kigezo pekee kinachoipa ICC mamlaka ya kushughulikia kesi.

ICC inaweza kuwa na mamlaka ikiwa uhalifu unaodaiwa kutendeka ulifanyika katika eneo la nchi mwanachama wa ICC au nchi iliyokubali mamlaka ya Mahakama hiyo kwa kesi husika.

Mfano unaojulikana ni wa Rais wa Russia, Vladimir Putin.

 Ingawa Russia si mwanachama wa ICC, mwaka 2023 Mahakama hiyo ilitoa hati ya kukamatwa dhidi yake kwa tuhuma za uhalifu wa kivita unaohusiana na uhamishaji wa watoto kutoka maeneo ya Ukraine.

Hilo liliwezekana kwa sababu Ukraine ilikubali mamlaka ya ICC kuchunguza uhalifu unaodaiwa kutendeka katika eneo lake.

Mbali na hilo, nchi ambayo si mwanachama wa ICC inaweza kuwasilisha tamko maalumu la kukubali mahakama hiyo ichunguze uhalifu uliotokea katika eneo lake, hata kama haijaridhia Mkataba wa Rome.

Njia nyingine inayoiwezesha ICC kupata mamlaka ni kupitia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Chini ya Mkataba wa Rome, baraza hilo linaweza kupeleka hali yoyote ICC kwa ajili ya uchunguzi, hata kama inahusu nchi isiyo mwanachama.

Utaratibu huo uliwahi kutumika katika migogoro ya Darfur nchini Sudan mwaka 2005 na Libya mwaka 2011.

Katika nyakati hizo, Sudan na Libya hazikuwa wanachama wa ICC, lakini Mahakama ilipata mamlaka ya kushughulikia kesi hizo kupitia maamuzi ya Baraza la Usalama.

Hata hivyo, ICC haina jeshi la polisi wala mamlaka ya kufanya ukamataji wake yenyewe.

Utekelezaji wa hati za kukamatwa hutegemea ushirikiano wa nchi wanachama na mataifa mengine.



Maoni ya wachambuzi

Mchambuzi wa sheria za kimataifa, Dk Mark Keteshi amesema uwepo wa ICC ni muhimu kwa sababu mara nyingi Serikali zinazotuhumiwa kwa ukatili hushindwa kujichunguza zenyewe.

“Ukiondoa ICC bila kuweka mbadala wake, unatengeneza pengo kubwa la uwajibikaji duniani. Waathirika wengi watakosa mahali pa kutafuta haki,” amesema.

Kwa mujibu wake, historia inaonesha mifumo ya ndani si mara zote huwa tayari kuwafikisha mahakamani viongozi au maofisa wanaotuhumiwa kwa makosa makubwa.

Amesema katika mazingira ambayo baadhi ya Serikali zinatuhumiwa kuhusika moja kwa moja na ukiukwaji wa haki za binadamu, uwepo wa Mahakama ya nje huwa muhimu zaidi.

Mchambuzi wa siasa za kimataifa, Dk Leila Nadya Sadat, amesema dunia ilijifunza kutokana na maafa ya karne ya 20 kwamba haki haiwezi kutegemea mipaka ya Taifa moja.

“Mahakama si kamilifu, lakini kutokuwa nayo ni hatari zaidi kuliko kuiboresha. Taasisi hiyo bado ni nguzo muhimu ya haki za kimataifa,” amesema.

Amesema kufutwa kwa Mahakama hiyo kunaweza kudhoofisha mfumo mzima wa sheria za kimataifa ulioundwa kuhakikisha makosa makubwa hayabaki bila adhabu.

Ameonya kuwa mataifa madogo na wananchi wanaoathiriwa na migogoro ndio watakaopoteza zaidi iwapo hakutakuwa na jukwaa la kimataifa la kutafuta haki.

Mwanasheria Philippe Sands, amesema nguvu ya ICC haipaswi kupimwa kwa kasi ya hukumu pekee bali kwa uwezo wake wa kuweka rekodi rasmi za uhalifu.

“Ukifuta ICC, unadhoofisha wazo kwamba hakuna mtu aliye juu ya sheria za kimataifa,” amesema.

Amesema hata pale kesi zinapochukua muda mrefu, uwepo wa Mahakama hiyo huwafanya viongozi na makamanda wa kijeshi kufikiria mara mbili kabla ya kufanya maamuzi yanayoweza kuleta madhara makubwa.

Amesema changamoto zilizopo ndani ya ICC zinapaswa kuwa sababu ya kufanya mageuzi yatakayoongeza ufanisi, uwazi na usawa badala ya kuiondoa kabisa.


Historia ya ICC

Wazo la kuanzisha Mahakama ya kudumu ya kimataifa lilikuwepo kwa miongo kadhaa, lakini lilipata msukumo mkubwa baada ya mauaji ya kimbari nchini Rwanda mwaka 1994 na vita vya Balkan katika miaka ya 1990.

Mwaka 1998, nchi mbalimbali zilikutana mjini Rome na kupitisha mkataba unaojulikana kama Rome Statute, ambao uliweka msingi wa kuanzishwa kwa ICC. Mkataba huo ulipitishwa Julai 17, 1998 na kuanza kutumika rasmi Julai 1, 2002 baada ya nchi zaidi ya 60 kuuridhia.

Tangu kuanza kazi mwaka 2002, ICC imefungua uchunguzi katika nchi mbalimbali, ikiwamo Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Sudan (Darfur), Libya, Kenya, Mali, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Ukraine na Palestina.

Kwa mujibu wa taarifa za mwaka 2026, ICC ina nchi wanachama 125 ambazo zimeridhia Mkataba wa Rome na hivyo kutambua mamlaka ya Mahakama hiyo.