Wachimbaji washauriwa kusajiri biashara zao

Chunya. Wachimbaji wa madini ya dhahabu wilayani Chunya mkoani Mbeya pamoja na wafanyabiashara wa madini wameshauriwa kusajiri biashara zao ili waweze kuendesha shughuli zao bila usumbufu.

Ushauri huo umetolewa na Ofisa Leseni Wakala wa Usajili Biashara na Leseni (Brela),  Saada Kilabula katika  maonyesho ya kwanza ya teknolojia ya madini na uwekezaji Wilaya ya Chunya Mkoa wa Mbeya.

Amesema wachimbaji watambue kuwa wakisajiri  kampuni zao na biashara zao za madini ya dhahabu ni rahisi kuaminika na kupewa mikopo na taasisi za kifedha.

Akizungumza katika Maonyesho hayo yanayoendelea wilaya ni hapa  amesema mwamko wa wanachi kujitokeza katika banda hilo kufanya usajili umekuwa mkubwa watu wamekuwa na nia ya kujua wanachokifanya na wengine kuomba wasaidiwe kusajili biashara.

Ameendelea kueleza kuwa  kwasasa wameboresha huduma mtu anaweza kujisajili kwa njia ya mtandao akiwa mahali popote  ambapo BRELA imekuwa ikitoa huduma hiyo kwa haraka na ufanisi na pindi wanapokamilisha wamekuwa wakipatiwa cheti.

"Mteja akishasajili jina la biashara au kampuni na kulipia na kutimiza matakwa ya kimsingi anapatiwa cheti ambapo tayari anakuwa amerasimisha biashara yake,” amesema Kilabula.

Aidha aliwataka watu kuendelea kujitokeza zaidi Brela ili waweze kupata elimu sambamba na kusajili majina ya kampuni na biashara zao kwani gharama zake ni ndogo na nafuu kwa mteja.

Aidha amebainisha baadhi ya changamoto wanazokutanazo kutoka kwa wateja kuwa ni  pamoja na watu kutokuwa na emails (barua pepe) na kutokutambua vizuri usajili wa mtandaoni.

Wakizungumzia kwa nyakati tofauti  baadhi ya wananchi waliofika  kwenye banda hilo la Brela,  John Rodrick na Martha Samwel  wameeleza kuwa wanafurahishwa na namna wakala hao wanavyowahudumia wateja, kwani wamekuwa wakikumbana na changamoto nyingi kutoka kwa taasisi za kifedha pindi wanapohitaji mikopo ya biashara zao hivyo kushindwa kupata mikopo.

"Maonesho haya yametufungua kwani tumekuwa tukifanya kazi zetu kiholela bila kusajiri na hivyo kukutana na changamoto kadhaa pindi tunapohitaji huduma za mikopo kwenye taasisi za kifedha na kufanya biashara zetu zishindwe kuendelea, wameeza wananchi hao."