Wachina waliofutiwa kesi na DPP watimua mbio mahakamani

Muktasari:

  • Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewafutia kesi ya uhujumu uchumi na kuwaachia huru wafanyakazi sita wa kampuni ya meli ya Sinota Shipping Company waliokuwa wanakabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la kukutwa na ndege mmoja aina ya tausi.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewafutia kesi ya uhujumu uchumi na kuwaachia huru wafanyakazi sita wa kampuni ya meli ya Sinota Shipping Company waliokuwa wanakabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la kukutwa na ndege mmoja aina ya tausi.

 Washtakiwa hao ambao wote ni raia wa China ni Jin Erhao (35), Chengfa Yang (49), Ren Yuangqing (55), Shu Nan (50), Chen Shinguang (45) na Gu Jugen (57) wote wakazi wa mtaa wa Sokoine, Ilala jijini Dar es Salaam.

Washtakiwa baada ya kuachiwa walitoka mahakamani huku wakikimbia na kupanda gari kisha kuondoka.

Wamefutiwa mashtaka yao na Hakimu Mkazi mwandamizi, Rashid Chaungu baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania( DPP) kuieleza mahakama hiyo kuwa hana nia ya kuendelea na shauri hilo dhidi ya washtakiwa hao.

Wakili wa Serikali, Kija Luzugana ameieleza mahakama hiyo wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

“Hakimu washtakiwa wote wapo mbele ya mahakama hii na DPP amesema hana nia ya kuendelea na shauri hili,"  amedai Luzugana.

Wakili huyo baada ya kuipa taarifa hiyo mahakama, Hakimu Chaungu amesema washtakiwa wamefutiwa mashtaka yao na kuachiwa huru.

Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 57/2020, washtakiwa walikuwa wanakabiliwa na mashtaka matatu yaliyowafanya wakose dhamana.

Katika shtaka la kwanza wanadaiwa Agosti 11, 2020 mtaa wa Sokoine kwa pamoja na kwa makusudi walisimamia genge la uhalifu lililopelekea kupatikana kwa ndege  huyo mwenye thamani ya Sh1,150,000.

Pia, siku na eneo hilo, washtakiwa kwa pamoja walikutwa na nyara ya Serikali iliyopatikana kinyume cha sheria ambayo ni ndege huyo.

Shtaka la tatu, siku na maeneo hayo kwa pamoja washtakiwa hao walikutwa na tausi  huyo huku wakijua kuwa kumiliki ndege huyo ni kinyume cha sheria.