Wadau madini wataka hospitali Mirerani


Muktasari:

  • Machimbo ya madini Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, hayana huduma za afya ikiwemo zahanati, kituo cha afya au hospitali.

Mirerani. Wadau wa madini ya Tanzanite wa mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara, wameiomba serikali kujenga miundombinu mbalimbali ikiwemo ile ya afya katika machimbo hayo ambayo hayana huduma hiyo.

Mdau wa madini ya Tanzanite, Fatuma Kifunta, ameyasema hayo mjini hapa leo jumatano Juni 22 mwaka 2023 kwenye muendelezo wa mradi wa Tanzanite kwa uchumi imara wa mwanamke ulioandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la Civil Social Protection Foundation (CSP).

Kifunta amesema Serikali inapata fedha nyingi kupitia kodi ya madini ya Tanzanite hivyo ingerudisha kwa jamii kwa kujenga, zahanati, kituo cha afya au hospitali katika eneo hilo la mgodi.

Mdau mwingine Tausi Bakari amesema serikali inapaswa kuweka miundombinu rafiki kwenye machimbo hayo ikiwemo barabara zilizopo ndani ya ukuta unayozunguka migodi ya Tanzanite.

"Barabara ni mbovu, watu wanatumia pikipiki hakuna magari ya abiria, pia maji hakuna, serikali ivute maji kwenye machimbo kwani haya ya kupelekwa na magari yanauzwa kwa bei ghali," amesema.

Mwanasheria wa CSP, Eliakim Paulo amesema kongamano hilo la mradi wa Tanzanite kwa uchumi imara wa mwanamke linahusisha wanawake wadau wa madini hayo, wasaidizi wa kisheria na waandishi wa habari.

Paulo amesema mradi wa Tanzanite kwa uchumi imara wa mwanamke, unahusisha wanawake wajasiriamali wa madini hayo wa kata za Mirerani, Endiamtu na Naisinyai wanaofanya biashara zao ndani ya ukuta unayozunguka migodi ya Tanzanite.

"Lengo ni kusababisha uchechemuzi kwenye kongamano hili na pia waandishi wa habari wataingia ndani ya ukuta unayozunguka migodi ya Tanzanite ili kuona changamoto na mafanikio ya wanawake hao," amesema.

Kaimu ofisa mtendaji mkuu wa mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani (TEO) Isack Mgaya akifungua kongamano hlo la siku nne ameipongeza CSP ambayo imeandaa mradi huo wa Tanzanite kwa uchumi imara wa mwanamke.