Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wadau: Mtoto hawezi kufaulu akiwa anajifunza kwa hofu

Muktasari:

  • Mazingira salama ya kujifunzia ni msingi muhimu wa elimu bora, kwa kuwa mtoto anayejisikia kulindwa huwa na uwezo wa kujiamini, kushiriki masomo, kuuliza maswali, kukuza vipaji na kujenga mahusiano mazuri na walimu pamoja na wanafunzi wenzake.

Dar es Salaam. Wakati juhudi za kuboresha ufaulu wa wanafunzi nchini zikiendelea kushika kasi, wadau wa elimu wameonya kuwa mafanikio hayo yanaweza kuwa ndoto iwapo shule zitaendelea kuwa mazingira yenye hofu, vitisho na ukatili kwa watoto.

Shirika la HakiElimu limesema mazingira salama ya kujifunzia ni msingi muhimu wa elimu bora, kwa kuwa mtoto anayejisikia kulindwa huwa na uwezo wa kujiamini, kushiriki masomo, kuuliza maswali, kukuza vipaji na kujenga mahusiano mazuri na walimu pamoja na wanafunzi wenzake.

Hata hivyo, shirika hilo limeeleza kuwa mtoto anayekumbana na vitisho, udhalilishaji, ubaguzi, ukatili au aina nyingine za unyanyasaji huathirika moja kwa moja katika mchakato wa kujifunza, hali inayoweza kushusha uwezo wake kitaaluma na kijamii.

Akizungumza jana wakati wa uzinduzi wa tathmini ya hali ya ujifunzaji salama nchini, Mkuu wa Programu wa HakiElimu, Godfrey Boniventura, amesema haki ya mtoto kupata elimu haiwezi kutenganishwa na haki yake ya kuwa salama.

“Tunaamini shule inapaswa kuwa sehemu ya matumaini, siyo hofu; sehemu ya malezi, siyo maumivu, na sehemu ya kumjenga mtoto, siyo kumvunja moyo,” amesema Boniventura.

Boniventura amesema changamoto za ukatili na ukosefu wa usalama shuleni zinahitaji ushirikiano wa wadau wote, akiwamo Serikali, mashirika ya kiraia, walimu, wazazi na wanafunzi wenyewe ili kujenga mazingira bora ya kujifunzia.

Amesema ubora wa shule haupaswi kupimwa kwa kuangalia majengo, madarasa au miundombinu pekee, bali pia kwa uwezo wake wa kumlinda mtoto, kumsikiliza na kumpa mazingira yanayomwezesha kujifunza bila hofu.

“Shule nzuri siyo ile yenye majengo pekee, bali ni ile inayomlinda mtoto, kumsikiliza na kumwezesha kujifunza bila hofu,” amesema.

Mtafiti Dk Hezron Onditi akiwasilisha matokeo ya utafiti uliolenga kuangalia ujifunzaji salama kwa wanafunzi shuleni.



Kwa mujibu wa Boniventura, matokeo ya tathmini hiyo yatatumika kama nyenzo ya kufanya uchechemuzikwa kushirikiana na Serikali na wadau wengine ili kuhakikisha suala la ujifunzaji salama linapewa kipaumbele katika sera, mipango, bajeti na utekelezaji wa programu za elimu.

“Utafiti huu unatukumbusha kuwa changamoto za usalama shuleni zinahitaji ushahidi, ushirikiano na hatua za pamoja. Kila mtoto anastahili shule salama, yenye heshima, inayomsikiliza na kumwezesha kutimiza ndoto zake,” amesema.


Ukatili wapungua, lakini bado upo

Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo, mtafiti kiongozi ambaye pia ni mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Hezron Onditi amesema tathmini ya Ujifunzaji Salama (UjS), inayotambulika kimataifa kama Safe to Learn (StL), imeonyesha mafanikio katika kupunguza ukatili dhidi ya watoto ndani na kupitia mazingira ya shule.

Hata hivyo, amesema bado kuna haja ya kuongeza juhudi katika kuimarisha mifumo ya ulinzi wa mtoto ili kuhakikisha mafanikio yaliyopatikana yanaendelea kudumu.

Amesema Serikali, watunga sera, washirika wa maendeleo, mashirika yasiyo ya kiserikali, watafiti na taasisi za kitaaluma wana wajibu wa kushirikiana kuhakikisha watoto wanapata mazingira salama ya kujifunzia.

Katika mapendekezo yake, utafiti huo umeitaka Serikali kupitia sheria na sera za elimu ili ziendane na viwango vya kimataifa vya ulinzi wa mtoto, ikiwamo kupiga marufuku kabisa adhabu ya viboko shuleni.

Pia, umependekeza mamlaka za wilaya zipewe uwezo zaidi kwa kupatiwa rasilimali na kuanzishwa kwa majukwaa ya kisekta yatakayosaidia kuratibu utekelezaji wa programu za ulinzi wa mtoto.

“Inapaswa kuamuru uanzishwaji wa miundo ya ulinzi wa mtoto shuleni, ikijumuisha walimu walezi waliopewa mafunzo, huduma za ushauri nasaha na mifumo madhubuti ya ufuatiliaji na utoaji wa taarifa za ukaguzi wa shule, badala ya kutegemea kwa kiasi kikubwa afua zinazofadhiliwa na wafadhili,” amesema Dk Onditi.


Tahadhari ukatili wa kidijitali

Mbali na changamoto za ukatili wa kawaida shuleni, Dk Onditi amesema kuna umuhimu wa kufanyika kwa tafiti zaidi kuhusu ukatili unaotokana na matumizi ya teknolojia.

Amesema tafiti hizo zinapaswa kuchunguza masuala kama uonevu mtandaoni, unyanyasaji wa kijinsia kupitia mitandao, tabia hatarishi za kidijitali pamoja na uelewa wa usalama wa mtandao kwa wanafunzi, walimu na walezi.

Amesema mabadiliko ya teknolojia yameleta fursa nyingi katika elimu, lakini pia yamefungua milango ya changamoto mpya zinazohitaji mifumo madhubuti ya ulinzi.


Walimu wakumbushwa mwongozo wa adhabu

Kwa upande wake, Mratibu wa Kitaifa wa Mpango wa Shule Salama, Dk Theresia Kuiwite amesema ipo haja ya kuchukua hatua dhidi ya walimu wanaoendelea kutumia adhabu ya viboko kinyume na taratibu zilizowekwa.

Amesema walimu wanapaswa kufuata mwongozo wa utoaji wa adhabu kwa wanafunzi na kuepuka kutumia viboko kama njia ya kawaida ya kurekebisha tabia.

“Mwalimu anayejielewa akiusoma vizuri mwongozo wa adhabu kwa mwanafunzi atajiweka mbali na viboko, kwa sababu umeelekeza adhabu hiyo inatakiwa kutolewa na nani na kwa utaratibu gani,” amesema.

Amesema wakati akiwa mwalimu katika Shule ya Sekondari ya Pugu aliweza kuishi na wanafunzi na kusimamia nidhamu bila kutumia viboko, jambo alilosema linawezekana kwa walimu wengine.