Wadau sekta ya maji waweka mkakati kulinda vyanzo

Mwenyekiti wa Jukwaa la Taifa la Wadau wa Sekta Mtambuka katika Usimamizi na Uendelezaji wa Rasilimali za Maji, Mhandisi Mbogo Futakamba

Muktasari:

  • Wadau wa usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji wamekutana Dar es Salaam na kutengeneza vikundi kazi vya watalaam vitakavyotoa ripoti ya utendaji wake mwishoni mwa mwakani

Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikiendelea kukumbana na upungufu wa maji, imebainika kuwa suala la usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji bado ni changamoto kubwa.

Kufuatia hilo wadau wa maji kupitia Jukwaa la Kitaifa la Maji linalohusisha sekta mbalimbali wamekutana jijini Dar es Salaam na kuunda vikundi kazi kwa ajili ya kuweka mikakati ya kutafuta fedha na usimamizi madhubuti wa rasilimali hizo.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Taifa la Wadau wa Sekta Mtambuka katika Usimamizi na Uendelezaji wa Rasilimali za Maji, mhandisi Mbogo Futakamba amesema pamoja na Watanzania kuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu umuhimu wa maji, wamekuwa hawashiriki kikamilifu kwenye utunzaji wa rasilimali zake.

Amesema hiyo ndiyo sababu ya kuanzishwa jukwaa hilo lililokuja na programu ya kushirikisha wadau wa sekta mbalimbali kuwa sehemu ya usimamizi na uendelezaji wa rasilimali hizo.

“Usimamizi wa rasilimali za maji hauko vizuri, yaani hadi sasa bado tunahubiri kuhusu kutunza vyanzo vya maji, mtu anafahamu kwamba kuingiza mifugo kwenye chanzo haitakiwi, kulima jirani na chanzo cha maji ni tatizo, lakini bado wanafanya.

“Halafu kazi hii haipaswi kuwa ya Serikali pekee ndiyo maana jukwaa hili likaundwa kuunganisha nguvu za wadau katika kuhakikisha rasilimali hizi zinasimamiwa na kuendelezwa,” amesema Futakamba.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji George Lugomela amesema jukwaa hilo linalenga kuongeza ushiriki wa wadau ikiwemo sekta binafsi katika usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji nchini.


Amesema, “Jukwaa hili limewekwa kisheria na maoni yanayotolewa hapa yanapelekwa kwenye bodi ya taifa ya maji hivyo ni sehemu ambayo wadau wa sekta zote wanaweza kutoa mawazo, utaalam na ujuzi wao katika kuhakikisha maji yanaendelea kupatikana nchini.”