Wadau: Ukosefu wa fedha mwiba mabadiliko tabia nchi

Anna Mbise kutoka Shirika la Friedrich Ebert Stiftung akizungumza wakati wa Warsha ya masuala ya Nishati, leo Mei 16 katika Hotel ya Protea by Marriott, jijini Dar es Salaam

What you need to know:

  • Wadau mbalimbali kutoka nchi za Ukanda wa jangwa la Sahara, wamekutana Tanzania, kujadili ni kwa jinsi gani nishati inaweza kuhama ilipo sasa hivi na inavyotoa suluhisho la matatizo mbalimbali, huku wakitafuta njia zinazoweza kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi.

Dar es Salaam. Wadau kutoka nchi mbalimbali wanaohusika na masuala ya nishati wamekutana jijini hapa, kujadili ni kwa jinsi gani nishati inaweza kuhama ilipo sasa na inavyotoa suluhisho la matatizo mbalimbali, huku wakitafuta njia zinazoweza kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi.

Akizungumza na mwananchi leo, Mei 16, jijini hapa, Mkurugenzi mtandao wa mabadiliko ya tabianchi, Dk Sixbert Mwanga amesema kumekuwa na ongezeko la ukame kwa baadhi ya maeneo katika nchi zinazopatikana ukanda wa jangwa la Sahara, huku kukiwa na ukosefu wa fedha ambayo ingeweza kusaidia kuhimili mabadiliko hayo.

“Lengo letu kubwa ni kujadili ni kwa jinsi gani uhamaji wa nishati utakavyo weza kumnufaisha kila mmoja.” Amesema.

Ameongeza na kusema, nchi mbalimbali zinazopatikana katika ukanda huu wa jangwa la Sahara, tukiwemo Tanzania bado wameendelea kukumbana na changamoto ya masuala ya nishati bora ambazo zingeweza kusaidia katika mabadiliko ya Tabianchi.

“Nchi zilizopo katika ukanda wa jangwa la Sahara zinahitaji kujadiliana kwa pamoja ili kuweza kutambua ni namna gani wanaweza kuhakikisha kuna kuwa na mahitaji bora ya nishati” Amesema.

Hata hivyo ameeleza kwamba kongamano hilo ni maandalizi ya kutafuta maoni ya pamoja ambayo watayapeleka katika mkutano mkuu, unahusu mabadiliko ya Tabianchi.

“Mkutano huo unatarajiwa kufanyika kuanzia mwishoni mwa mwezi Novemba mpka mwanzoni mwa mwezi Disemba, 2023 huko Dubai.” Amesema.

Kwa upande wake, Kenny Mogan, kutoka Afrika Kusini ambaye ni Afisa wa viwanda kutoka Kusini mwa Jangwa la Sahara yeye amesema watahakikisha watatatua migogoro itokanayo na masuala ya nishati.

Mratibu katika mtandao wa jinsia na mabadiliko ya Tabianchi, Maria Matui ameeleza kwamba, wao kama mtandao wameshirikishwa kuzungumzia upande wa wanawake huku akisema bado kuna changamoto ya wanawake kushirikishwa katika masuala yanayohusu nishati.

Naye, Anna Mbise kutoka shirika la Friedrich Ebert Stiftung ambao ndio waliandaa warsha hiyo amesema wao wamewakutanisha wadau kujadili mambo yanayohusika na masuala ya mabadiliko ya Tabianchi.

“Wadau ndio watazungumza ili kutambua mabadiliko hayo yanaitaji sera zipi,na hatua zipi ambazo zitawasaidia  wasiharibu mazingira huku wakiendelea kulinda haki na mslahi ya wafanyakazi” amesema

Wadau hao wametoka katika mataifa ya Zimbabwe, Zambia, Ghana, Nigeria, Afrika Kusini, Tanzania, Senegal, Botswana.